Korona: Filimbi Na Mwito Kwa Wote

Ukisikia la mgambo, ujue kuna jambo. Usemi huu unatanabaisha uwepo wa filimbi ambayo imekuwa mwito kwa watu wote. Je, filimbi hiyo ni nini? Filimbi imelilia wapi jamani? Nani kapuliza filimbi hiyo? Nani katengeneza filimbi? Filimbi hii ni kirusi. Kirusi gani ndugu zangu? Ni kirusi cha Korona. Korona ni filimbi ambayo ilitoa mwito wake mwezi desemba 2019, katika nchi ya China ambako imeua na kujeruhi watu wengi.

Korona ni filimbi ambayo mwito wake wasikika duniani kote. Mwito wake wapenya angani, majini na hata miisho ya dunia. Mwanadamu kila mara asikiapo filimbi hii husononeka moyoni hata rohoni pia. Korona umekuja kwetu kama baraka au laana? Umekuja kama tetemeko ili utuangamize au kutushtua? Je, umekuja kama radi ili utuue au ututakase? Maswali mengi yanamuijia kila mmoja wetu. Tafakari imekuwa juu yako wewe Korona, kwamba umekuja kwetu kama silaha ya kutuangamiza au kutuokoa? Ama kweli, Korona sasa umechukua nafasi ya kwanza katika maisha ya walimwengu. Kwani, mlio wako wasikika pote duniani. Hakuna asiyekujua wala kukusema wewe Korona. Vyombo vya habari, serikali hata viongozi wa dini makanisani na misikitini wanakuzungumzia wewe Korona. Ni nini lengo lako kwetu sisi, mbona umeifanya mioyo na roho zetu kutokutulia? Ni kweli kwamba sasa maneno ya Mt. Augustino yanatimia masikioni mwetu, “Ee Bwana Mungu, umetuumba kwa ajili yako, na mioyo yetu haitatulia isipokuwa katika wewe Mungu wetu”. Mioyo yetu imeshindwa kutulia sasa kwa sababu ya janga la Korona. Mlio wa Korona watikisa dunia nzima.

Hata hivyo, yaweza kuwa mlio wako kama filimbi umekuja ili kutukumbusha mahali tulipojisahau ili tuweze kurudi tena katika misingi ya kumuelekea Muumba wetu, yaani Mungu muweza wa yote, aliye Mganga wa roho na mwili. Filimbi wewe umekuwa sumaku na mnato wa kuturudisha kwa Mungu ambaye katika kutuumba alituachia majukumu na wajibu wa kutimiza ambao ni kumjua, kumpenda, kumtumikia na hatimaye kufika kwake mbinguni. Huu ndio mwito ambao Mungu wetu anatudai kuutimiza. Je, katika maisha yetu tumeyatimiza hayo? Je, Korona umekuja kutufanya tushituke na kumrudia Mungu? Kweli Korona umekuwa janga la ulimwenguni. Hata ukauunganisha ulimwengu kuwa kitu kimoja, bila kujali tofauti zetu.

Aidha, uwepo wako umewafanya walimwengu kuwa na kujiona kuwa ni kijiji kimoja. Kwani, kile kinachotokea Ulaya, Asia, Afrika, Amerika ya Kusini na Kaskazini, na Australia ni kimoja. Haya mabara yamekuwa kitu kimoja katika kulitafutia utafiti na uvumbuzi hili jambo. Mlio wake wasikika kwa watu wote, weupe na weusi, matajiri na maskini, wasomi na wasio wasomi, waamini na wasioamini. Sisi sote tumekuwa kitu kimoja kwa sababu yako Korona. Na umetuunganisha katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Kila mmoja wetu kwa lugha na dini yake anamlilia Mungu ili atunusuru nawe, uliye janga la ulimwengu huu, upite na utokomee. Hii ndiyo kiu na shauku ya kila mwanadamu. Mapesa mengi yamepotea kwa sababu yako Korona. Wataalam na wanasayansi wengi hawalali kwa sababu yako, wakitafiti namna na jinsi ya kujikinga nawe. Huku wakipiga magoti kumuomba Mungu awaangazie dawa au chanjo itakayowaokoa waathirika wa virusi vya Korona.

Vilevile, uhai wa watu mbalimbali umepotea, kwa sababu yako wewe Korona. Swali msingi linalomjia kila mmoja wetu ni kwamba, tufanye nini sasa ili tuweze kukuondoa wewe filimbi unayesikilika kila mahali? Wewe ambaye unasikilika kila mahali kama mwangwi unaotutahadharisha juu ya masuala yatuhusuyo sisi wanadamu?



Kama ilivyodokezwa hapo awali, ugonjwa wa Korona ni filimbi ambayo ilisikilika Desemba 2019, ukisababishwa na virusi aina ya Korona-(COVID-19). Ugonjwa huu umekuwa ukishambulia mfumo mzima wa hewa. Hivyo, huadhiri mfumo mzima wa upumuaji na hivi kusababisha ugumu katika kupokea na kutoa hewa mwilini. Na unaambukizwa kwa kugusana na unyevunyevu utokao katika mfumo mzima wa hewa au upumuaji wa mtu aliyeathirika. Yaweza kuwa kwa kukumbatiana na mtu aliyeathirika, kugusana mikono na mtu aliyeathirika na namna nyingine nyingi. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna dawa iliyopatikana inayotibu ugonjwa huu. Filimbi hii inaendelea kutukumbusha kuchukua tahadhari maana ni mwito wa kuwa makini. Maana tusipoangalia tutapukutika kama majani ya miti na mara tutatoweka.

Hata hivyo, ugonjwa wa Korona una nafasi pia katika historia ya mwanadamu. Kwa kuwa kila litokealo katika mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu huwa na maana yake na hutufunza kitu msingi katika mwenendo mzima wa kuenenda na kuishi kwetu kama wana wa Mungu. Historia ya filimbi hii haitasahaulika, imeanzisha na itaacha chapa katika maisha ya mwanadamu. Na itabakia kuwa historia na simulizi isiyoelezeka.

Je, kazi ya filimbi ni nini? Kazi ya filimbi ni kutaarifu, kutanabaisha, kutahadharisha, kuita, kutoa mwongozo wa kufuata na yanayofanana na hayo katika muktadha fulani wa maisha; yaweza kuwa katika matukio katika jamii (msiba, uvamizi, sherehe n.k), uwanja wa mpira ama katika tasnia ya muziki. Filimbi ni dira na mwongozo unaoita watu kufuata utaratibu fulani wa maisha. Korona kwetu sisi binadamu ni filimbi inayolia ikiashiria hali ya hatari, onyo kali juu ya namna yetu ya kuishi. Tukijifanya viziwi tusiisikie, itakula kwetu na tutabaki tukishangaana huku tukimalizika.

Korona ni vita inayomwathiri mwanadamu mzima, mwili na roho, mashambulizi yake ni zaidi ya mabomu katika uwanja wa vita. Ama kweli Korona wewe ni jemedari unayetishia kila nchi, wewe ni filimbi. Korona umesababisha tufunge shughuli mbalimbali za kijamii. Umetufanya tuone hakuna wa lazima katika maisha ya hapa duniani, ila kila mmoja ni wa muhimu. Hujali hadhi, kipato, elimu na mengine mengi yampayo binadamu heshima. Wewe wafyeka wote; watoto kwa wakubwa, matajiri kwa maskini, waelevu kwa wajinga, waaminio na wasioamini. Wote hawa unawafyeka. Kwani Korona umekuwa kama simba atafutaye mawindo kama Mt. Petro anavyotueleza na kutupa tahadhari, “Muwe macho, kesheni! Maana adui yenu, shetani [Korona], huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayo hayo” (1Pet 5:8-9). Korona ni simba atafutaye mawindo, tunatakiwa tuwe imara katika kusali na kumuomba Mungu atuoneshe namna ya kupambana na ugonjwa huu. Huku tukifuata mashauri yatolewayo na wauguzi na madaktari wetu. Kwani tusipofanya hivyo, simanzi na majonzi itakuwa sehemu ya kila uchao wa maisha yetu. Kwani hata sasa simanzi imetanda katika nchi nyingi duniani, kama China, Itali, Marekani, Hispania, Ufaransa, Iran, Ujerumani, Uholanzi na nchi nyinginezo duniani. Mashule na vyuo navyo vimefungwa, makanisa na taasisi mbalimbali zimesitisha huduma zake kwa sababu tu ya filimbi hii inayosikilika pote duniani; Korona, Korona korana!!!

Katekismu ya Kanisa Katoliki inaendelea kutuweka bayana na kutuzamisha zaidi katika kutafakari juu ya ugonjwa huu wa Korona kwa maneno haya:

“Ugonjwa na mateso yamekuwa daima kati ya matatizo mazito sana yanayoyaweka maisha ya mwanadamu katika majaribu. Katika ugonjwa mtu anapata mang’amuzi ya kutokuwa na uwezo, ya mipaka yake na kikomo chake. Kila ugonjwa unaweza kutufanya tuchungulie kifo. Ugonjwa waweza kutupeleka kwenye uchungu, kujihangaisha wenyewe, pengine hata kukata tamaa na kumwasi Mungu. Waweza pia kumkomaza mtu zaidi, kumsaidia kupambanua katika maisha yake kile ambacho si cha lazima ili kuelekea kile kilicho cha lazima. Mara nyingi ugonjwa huchochea kumtafuta Mungu na kurudi kwake” (KKK, nn. 1500-1501).

Haya yanajidhihirisha katika nyakati zetu ambapo watu karibia wote wanasali ili Mungu atunusuru na janga hili la Korona. Ni kweli kwamba, kila ugonjwa unaweza kutufanya tuchungulie kifo.

KISIASA



Korona ni filimbi ambayo imekuja kumaliza tofauti zetu za kisiasa. Machafuko na mapigano yaliyokuwa yanatokea yamekoma. Hata kwenye vyombo vya habari, mauaji yaliyokuwa yanatokea huko Syria, Sudani, Iraq, Kongo na kwingineko hatusikii tena. Ghasia na matishiano ya vifaru, mabomu ya nyuklia na silaha kama ilivyokuwa kwa Marekani na Korea ya Kaskazini, havipo tena. Korona ni filimbi ambayo imekuja kutatua matatizo na kuondoa machafuko. Swali msingi la kujiuliza, kama hapo awali tulikuwa tunafurahia kuuana sisi kwa sisi kwa silaha, hatukuogopa kifo, kwa nini tunaogopa Korona ambayo imekuja kutusaidia kukamilisha nia yetu? Kwa nini Sudani, Kongo, Syria hawapigani tena? Korona imekuja kama baraka na njia tatuzi katika jamii tunamoishi. Kama Aristotle asemavyo, “Mwanadamu ni kiumbe jamii”, na huyu mwanadamu alikuwa amekosa Amani katika jamii anamoishi kwa sababu ya machafuko ya kisiasa. Lakini Korona imerejesha tena hali tulivu ya kijamii iliyokuwa imepotezwa na siasa chafu zisizojali matakwa ya wanajamii. Korona ni filimbi ambayo imekuja kutatua na kutoa suluhu ya kisiasa.

KIROHO



Mateso na mahangaiko ya maisha yetu hapa duniani yanaakisi tu mateso ya Kristo kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa kujua ukweli huu Kanisa linahimiza waamini kuvumilia mateso na magumu yanayotupata katika kumfuata Kristo ili tuufikie utukufu wa milele. Mateso tuyapatayo katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu yanatustahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni kama tukiyapokea kwa imani na bila kunung’unika. Kuna mateso yanayosababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambayo yanaleta mabadiliko ya tabia ya nchi yasababishwayo na ufidhuli wa mwanadamu. Kwa mfano: mafuriko na ukame, matetemeko, magonjwa ya mlipuko kama homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Korona nyakati zetu, wengine wanateseka kwa vita, umaskini, manyanyaso kazini, ugomvi wa kifamilia. Mateso haya, yasitufanye tukate tamaa bali yaimarishe imani yetu tukijua kuwa Kristo yupo kwa ajili yetu, anayajua hayo yanayotukabili na tukimwamini yeye, atatusaidia. Lakini tutambue kuwa majukumu yanayotukabili katika maisha ya kila siku sio mateso. Na ndiyo maana Korona imekuja kama alamu ya kutukumbusha juu ya maisha yetu ya kiroho, kusali, kufunga na kuwasaidia wahitaji.

Tutambue pia, mateso na mahangaiko tunayojisababishia wenyewe kwa kukiuka amri na maagizo ya Mungu, mateso yatokanayo na dhambi zetu wenyewe, hayawezi kutuletea wokovu bali yatatupeleka kwenye moto wa milele kwani yanazidi kumtesa Kristo Mfufuka, aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Leo hii waamini ni wagumu kujiosha na kujitakasa nafsi na roho zao kwa sakramenti ya kitubio. Lakini imekuwa virahisi kwao kujiosha mikono kwa vitakasa mikono (sanitizers), sabuni na maji wakiogopa Korona iuayo mwili, na kutokuogopa kile kiuacho mwili na roho. Korona ni filimbi inayotualika kutubu na kujipatanisha kwanza na nafsi zetu, pili na wenzetu na mwisho kujipatanisha na Muumba wetu kwa dhambi tulizotenda. Hii itafikia tu tukiweka Imani kwa yeye aliyetuumba. Leo hii Korona ingekuwa inaambukizwa kwa kufanya dhambi, je, tungeendelea kufanya dhambi? Mfano, ingekuwa ukisema uongo, ukizini, ukitoa mimba, ukiiba au ukafanya dhambi yoyote unapata Korona, dunia yote tungeacha dhambi? Na wala Korona isingesambaa kwa kiasi hiki.

Licha ya kuwa tunaambiwa juu ya dhambi hatusikii wala kuelewa kwa sababu ya kiburi, majivuno na ukaidi tunajikuta tuna matatizo na masumbuko mengi na watu waliowajanja wanaongozwa na Ibilisi wanayatumia matatizo yetu kujinufaisha wao wenyewe na kutufanya tuasi imani yetu. Dhambi ni mateso ya kujitakia wala Mungu hahusiki na haya wala hayatuletei wokovu bali yatatupeleka katika moto wa milele aliyetayarishiwa ibilisi na malaika zake tangu awali (Mt 25:31ff). Hivyo, Korona kwetu sisi imekuja kuyarekebisha mawazo yetu, maneno yetu, matendo yetu maovu kuwa mema, na kutualika kutimiza nyajibu zetu za kikristo. Tunaposhindwa kuyatimiza hayo, dhambi zetu zinakuwa zinaongeza mlio wa filimbi kuwa mkubwa. Hapa Baba Mtatakatifu Fransisko amesema, tunaweza tukawa tunakwepa kirusi cha Korona, lakini tukaongeza na tukaangukia kwenye kirusi kingine ambacho ni kibaya zaidi, yaani ubinafsi.

KIMAADILI

Kimaadili, Korona imekuja kama mwongozo wa kimaadili unaotudai kubaki katika miongozo na kanuni za kimaadili. Korona ni filimbi inyotualika kuachana na maovu yanayoendelea kuharibu maadili ya jamii. Kwa mfano, wizi, kutoka nje ya ndoa, kijana hujaoa au hujaolewa umekamatwa katika uasherati, matumizi ya madawa ya kuzuia mimba ambayo yana madhara katika miili yetu yanaharibu mfumo wa uzazi, mfano, kushindwa kupata mtoto utakapomhitaji na tena ni dhambi na chukizo kwa Mungu yanapinga kazi ya Mwenyezi Mungu, kutoa mimba ni dhambi na chukizo kwa Mungu, kupiga ramli (Imani za kichawi na kishirikina), ulevi, uvivu, uzembe kazini unasababisha kufukuzwa kazi, rushwa (mali, ngono, madaraka) ni mbaya utafia gerezani, imani na sera za freemasons kama kutoa kafara za watu, sio tu ni dhambi na chukizo kwa Mungu bali pia yanatuletea shida na matatizo katika maisha yetu. Korona imekuja kuyatatua. Hivi, leo tungeambiwa ukipokea ama kutoa rushwa unapata Korona, je, tungeendelea kutoa na kupokea rushwa? Je, TAKUKURU ingeendelea kufanya kazi zake? Ni wazi hapana, kama watu wameambiwa ilikujikinga na Korona inatakiwa kutumia sabuni na maji yanayotiririka na wanafuata maagizo hayo. Kwa nini hatuachi kuzini, kuiba, rushwa, n.k?

Tusikatishwe tamaa au kukwazwa, na kurudi nyuma, bali mahangaiko ya magonjwa na mateso tunayoyapata yatuimarishe na kutuunganisha zaidi na Kristo aliyevumilia mateso kwa ajili yetu sisi wadhambi ili mwisho wa yote tukamsifu Mungu pamoja na malaika zake huko mbinguni milele yote.

Hivyo, tuungane kwa pamoja katika kusali, kufunga na kufanya toba ya ndani ya roho, yaani kunuia kuacha dhambi na kutenda mema. Tuisikilize filimbi hii kwa moyo wa majuto. Tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii kama nabii Isaya alivyosema “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi…huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao” (Rej. Is 50:4-11). Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuwe watii. Tujipatanishe na Mungu ndipo tutakapokuwa na sababu ya kufurahia maisha mapya na tunuie kutorudi nyuma tena mpaka tutakapomaliza safari yetu na kufurahi milele katika maisha ya umilele mbinguni. Kwani, Korona ni filimbi na mwito wa kuturudisha tena katika njia ya uzima wa milele.

Fr. Emmanuel Kimambo Nhanwa,
Jimbo Katoliki Shinyanga,
Mwendakulima Seminari Kuu ya Kitaifa


REJEA:

BIBLIA YA KIAFRIKA, Titu Amigu et Alii (Trs & Eds), (Nairobi: Pauline Publications Africa, 2010).

KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI, Michael Mushi (Ed.), (Nairobi: Pauline Publications Africa, 2000).

POPE FRANCIS, Life After The Pandemic, Preface by Card. Michael Czerny SJ, (Rome: Vatican Press, 2020).

St. Augustine of Hippo, The Confession of St. Augustine, Trans. & Annotated. Silvano Bruso, Pauline Publications Africa, 20142.