Nini Chanzo Cha Maovu Katika Jamii


Katika jamii tunayoishi kumekuwapo na maovu mengi yanayoendelea kujidhihirisha licha ya watu kuendelelea kushangaa na kujiuliza kwanini yote haya. Nini hasa chanzo cha uovu katika jamii? Je,ni Mungu au mwanadamu?. Kama siyo Mungu au mwanadamu, je, kuna kiwepo kingine ambacho ndiyo chanzo cha hayo maovu? Ili kusudi tuwe na mang’amuzi ya kutosha juu ya hilo, ni vizuri tukaanza kwa kujibu swali hili, uovu ni nini? Na baadaye tutaweza kutafakari na kutafiti chanzo na chimbuko la maouvu katika jamii.

Uovu ni kutokufaa kwa kitu kwa ajili ya maelekeo asilia[1]. Hii ina maana kuwa chochote ambacho kinafanyika kinyume na asili yake kinavyotakiwa kufanyika huonekana kuwa kiovu mbele ya macho ya watu na jamii kwa ujumla. Hivyo uovu hujumuisha kukosekana kwa maadili mema. Maovu hujumuisha rushwa, uotaji mimba, uzinzi, uasherati, ushoga, imani za kishirikana ,mauaji kama vile albino, vikongwe na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Uovu ni kutokuwepo kwa kiwepo. Uovu hutokea pale ambapo kile kinachotakiwa kuwepo kinapokosekana. Uovu ni kutokuwepo kwa wema ambao ulitakiwa kuwepo[2]. Hii ina maana kuwa uovu siyo kitu kizuri, hakina wema ndani yake. Huu ufafanuzi wa uovu una msingi kutoka kwa Mt. Augustino aliposema kwa maneno mawili ya Kilatini “privatio boni” ambayo maana yake ni “kutokuwepo kwa wema au uzuri”[3]. Hili neno kutokuwepo lina maana ya kukanusha, ambalo ni kukosekana kwa wema ndani ya kiwepo au kitu.

Tukiwa na mtazamo kama wa Aristoto nasi twaweza kusema “hakuna athari bila sababu” hivyo hatuna budi kuangalia chimbuko na chanzo cha uovu katika jamii yetu na kwa namna ya pekee wakati huu ambapo maovu mengi yanaendelea kutokea na kunyanyasa nafsi za watu. Nini chanzo, asili, kisababishi au chimbuko la uovu?. Je, ni Mungu? Kama siyo Mungu, je ni mwanadamu? au kuna kiwepo kingine ambacho ndiyo chanzo cha hayo maovu?

Kwanza kabisa lazima tuelewe na tujue kwamba Mungu hawezi kuwa chanzo cha maovu. Kwa maana Mungu hakuumba uovu, hii ni kwa sababu vitu vyote alivyoviumba vilikuwa vyema “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana”[4]. Ni ukweli usiopingika kuwa Mungu siyo chanzo cha uovu maana kila alichokiumba kilikuwa chema. Tukiwa na mtazamo wa hapo juu tunaweza kuhitimisha kuwa, uovu husababishwa na viwepo vilivyoumbwa ambavyo hushindwa kufanya kile ambacho ni chema na kusababisha upungufu katika wema au uzuri wa kiwepo.

Lakini bado twaweza kujiuliza, je, Mungu anajua chanzo cha uovu? Kwa uhakika Mungu anajua chanzo cha uovu, kwa sababu Mungu ajua yote. Yeye huifahamu tabia ya kiwepo ya kutenda au kufanya mabaya au maovu, kwa sababu hiyo Yeye hufahamu yote na ni chanzo cha maarifa yote. Swali jingine, je, kiwepo kinahusika katika kutenda ovu? Je, kinauwezo wa kutofanya kile kilicho kiovu? Mt. Gregory wa Nyssa anasema “Mungu alimuumba mwanadamu huru na hivyo huheshimu uhuru wake, mwanadamu huchagua kufanya lililo ovu kwa uhuru wake, hivyo Mungu hamlazimishi kwa nguvu kwa sababu tu anaheshimu uhuru wake.

Maana ya maneno hayo ni kwamba mwanadamu hajashinikizwa kufanya vitu kwa sababu yuko huru kuchagua ya kufanya, hivyo anaweza kuchagua kile killicho chema au kiovu. Na hivyo Mungu hawezi kulaumiwa kwa uwepo wa uovu maana alimpa mwanadamu akili na utashi. Tangu mwanzo Mungu alikusudia kuumba ulimwengu ulio bora tofauti na jinsi tuonavyo sasa. Na akamuumba mwanadamu ambaye ni kiumbe pekee ambacho Mungu alikijalia akili na utashi ili kichague ama jema au ovu; hivyo yupo huru kufanya anachopenda. Mungu hawezi laumiwa kwa sababu ya uovu unaoendelea kutokea katika jamii kwa maana mwanadamu aliuchagua.

Hili linajidhihirisha katika kitabu cha mwanzo sura ya tatu ambapo mwanadamu alipomuasi Mungu kwa kutumia vibaya uhuru aliopatiwa; akawa mwenye kiburi na kugeukia uovu na ndipo hapo anguko la kwanza la mwanadamu likatoke ambalo mpaka sasa linaendelea kujionesha katika maisha ya mwanadamu. Uovu hutokana na mwanadamu na siyo Mungu ambaye ni wema wenyewe, uzuri na upendo wenyewe, hakika Mungu hawezi kuwa chanzo cha uovu.

Uovu hutokana na mwanadamu na siyo Mungu ambaye ni wema wenyewe

Kwa hiyo, tunaweza ona kuwa chanzo cha uovu ni pale ambapo mwanadamu alishindwa kutumia vyema akili na utashi ambavyo Mungu alimpa. Mt. Augustino ana hili la kusema juu ya chanzo cha uovu “uovu hauna chanzo kingine zaidi ya mapenzi ya mtu ambao hufanya uamuzi ulio mbaya. Hivyo chanzo na kisababishi cha maadili maovu ni matumizi mabaya ya utashi kwa kufanya uchaguzi ulio mbaya au muovu…uovu wa utashi wenyewe ambao ni sababu na chanzo cha matendo maovu. Hivyo matumizi yasiyo sahihi ya utashi wake mwanadamu ndiyo chanzo cha maovu katika jamii. Maana Mungu alimpa Uamuzi huru "Freewill” wa kuchagua mema na mabaya(mwanzo 3:5). Lakini yeye kwa kiburi chake akageukia lililo ovu.

Kama mwanadamu alichagua uovu, je, inamaanisha kuwa mwanadamu hakuwa mkamilifu kimienendo au kimaadili tangu kuumbwa kwake?. Ni kweli mwanadamu hakuumbwa mkamilifu bali alipewa akili na utashi ili kwa kuvitumia apate kuwa mkamilifu. Ndiyo Katekisimu ya Kanisaa Katoliki inaelekeza na kufundisha kuwa

“uadilifu wa matendo ya kibinadamu hutegemea: kitu lilichochaguliwa, kusudi lililotazamiwa au nia; mazingira. Kitu, nia na mazingira huunda vyanzo au mambo yenyewe ya uadilifu wa matendo ya kibinadamu. Kitu kilichochaguliwa kimaadili hukibainisha kitendo cha utashi, kwa kiasi ambacho akili inavyokijua na kukihukumu kulingana au kutokulingana na jema la kweli. Kanuni sahihi za uadilifu huonyesha utaratibu wa kiakili wa mema na mabaya, zikithibitishwa na dhamiri…Tendo jema kimaadili latakiwa kwa pamoja kuwa na uzuri wa kitu, nia na wa mazingira. Nia mbaya huharibu tendo hata kama kwa lenyewe ni chema… kuna matendo ambayo kwa yenyewe na ndani yao, bila kujali hali ya mambo na nia, daima hayaruhusiwi kabisa kwa sababu ya nia yao, kama kumkufuru Mungu, kuapa uongo, kuua mtu na uzinzi. Hairuhusiwi kutenda uovu ili litoke humo jambo jema”[5]

Hivyo mwanadamu amekuwa akifanya matendo fulani ambayo kwa yenyewe ni maovu kwa lengo na nia ya kupata kile kilicho chema na kizuri ili kimpatie furaha anayonuia. Mfano mzuri ni mwanadamu anayeweka nguvu zake katika kuwaua albino akiamini viungo vya albino ndiyo chanzo cha mali, fedha au utajiri. Kutumia shida za watu kujinufaisha wenyewe ikiwemo kunyanyasa wajane, yatima na wahitaji kwa kuminya fungu lililoelekezwa kutumika na kuwasaidia.

utoaji mimba ni uuaji, kinyume na Amri ya Tano ya Mungu

Ushoga, utoaji mimba, mauaji ya vikongwe yameshamiri na kupamba moto katika jamii. Hii ni mbaya sana kwa maana mwanadamu huyu amesahau kuwa Mungu ni chanzo cha yote mema na siyo hayo maovu. Hivyo inatakiwa kuinua mioyo na akili zetu kwake ili tuweze kupata kile kilicho chema na kizuri ambacho kina Baraka na neema za Mungu. Kwa hiyo, mwanadamu akitumia akili na utashi wake kuchagua lililo ovu kwa lengo la kupata chema amepotea, kwa kuwa anaenda kinyume na uadilifu unaomdai kufanya kila mara lililo jema. Maana huwezi kupata utajiri au furaha ya kweli kwa kutoa uhai wa mtu.

Katika kufikiri na kutafakari kwangu nimegundua kuwa licha ya mwanadamu kutotumia vema akili na utashi wake, malezi ya familia yamekuwa kichocheo cha haya yote kuendelea kutokea katika jamii pale wazazi wanaposhindwa kuwalea watoto wao katika maadili mema. Hasa kukosekana kwa familia takatifu[6] ambayo ni shule ya unyenyekevu, uti, sala, uaminifu, huruma na zaidi ya yote ni shule ya Upendo katika jamii ndiyo chanzo na mwendelezo wa maovu tunayoendelea kuyashuhudia hivi leo. Haya yote yatakoma tu kama jamii zetu zitajengwa juu ya tunu za familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ambayo ndiyo mfano wa kuigwa na familia zote za kikiristu na zile zenyenye mapenzi mema. Maana mwanadamu hupata msingi wa maadili yaliyo mema katika familia. Wahenga husema “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Mtoto aliyelelewa katika familia yenye maadili mema, yenye kumcha Mungu ni wazi atakuwa na maadili mema. Kinyume pia ni kweli, kama mtoto amekulia katika familia ambayo Mungu kwao si kitu, maadili, utu wema, upendo au unyenyekevu si kitu. Basi huyo mtoto hatakuwa na maadili mema maana dhamiri yake imejengwa juu ya hayo.

Sala yangu ni moja tu. Tushirikiane sote katika kutokomeza hayo maovu ambayo yanatufanya tushindwe kuipata furaha ya kweli katika maisha yetu ya sasa, hapa duniani na yajayo katika Utukufu wa Mungu aliye Mtakatifu, ambaye kila mara anatuita sisi sote kuwa watakatifu “mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi Bwana Mungu wenu ni Mtakatifu”[7] hii itawezekana tu tukinuia kukata mianya yote ya kutenda na kugeukia lile lililo ovu katika maisha yetu ya kila leo.

Fr. Emmanuel Kimambo Nhanwa,
Mwendakulima Seminari Kuu ya Kitaifa.

REJEA
KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI, Michael Mushi (Ed.), Pauline Publications Africa, Nairobi 2000.

BITTLE N. Celestine, ONTOLOGY: The Domain Of Being, Milwaukee: The Brace Publishing Company 1950.

McINERNY Q. D, Metaphysics, The Priestly Fraternity of St. Peter Elmhurst, Pennsylvania 2004.

BIBLIA TAKATIFU, Toleo La Iringa, Mpanda 1997.