TUMSIFU YESU KRISTO!
Nanyi Mtakuwa mashahidi wangu.
Mwaliko wa kumshuhudia Kristo Yesu aliyepaa mbinguni
Leo tunaadhimisha sherehe ya Kupaa Mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Ni sherehe tunayoadhimisha kila mwaka siku ya arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya pekee, kwani Bwana wetu Yesu Kristo alipokea tuzo kwa kazi nzuri aliyoifanya hapa duniani, yaani kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti.
Mama Kanisa anakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Sherehe Ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Ushuhuda Wa Fumbo La Imani. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba, kwenye uzima na furaha ya milele pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwa kupaa mbinguni, Kristo Yesu amemfungulia mwanadamu njia, ili akae na kuamini, kwamba, waamini ambao ni viungo vya mwili wake, amewatangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu (Rej. KKK 659-662).
Tunapoadhimisha sherehe ya Kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo, swali la msingi hapa lingekuwa kupaa maana yake nini? Ndugu zangu katika Kristo neno kupaa lina maana nyingi baadhi yake ni hizi: Kibiblia kupaa lina maana ya kuhama kwa mwili wa ufufuko wenye utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo, kutoka duniani na kuingia Mbinguni. Na maana nyingine ya kupaa ni hali ile ya kutukuzwa kwa Yesu ili apate kuwa mkuu na mmiliki wa vyote duniani na mbinguni. Hivyo basi Kupaa ni tendo au hali ya kurudia utukufu aliokuwa nao kabla hajachukua mwili kwa Mama Maria yaani umwilisho. Na si safari ya kuelekea angani kama tunavyodhani bali ni kutawazwa cheo cha juu ndani ya Mungu Baba.
Kristo ni mshindi ameshinda dhambi ambayo hupelekea kwenye mauti
Hata hivyo, mara nyingi tunajiuliza, kwa namna gani Yesu alipaa Mbinguni! Tukisoma kutoka katika Maandiko Matakatifu, mwinjili Luka anasema; wote wakiwa wanamtazama, Yesu aliinuliwa Mbinguni na wingu likamficha wasimwone tena. Kumbe Mwinjili Marko anasimulia kuwa; Bwana wetu Yesu Kristo alipokwisha sema nao, alichukuliwa Mbinguni akaketi upande wa kulia wa Mungu. Kwa hiyo ndugu zangu katika Kristo, jambo wanalokazia hawa Wainjili ni hili kwamba: Bwana wetu Yesu Kristo alipaa Mbinguni.
Yesu amepaa mbinguni kwanza, ili apokee tuzo kwa kazi nzuri aliyoifanya duniani, yaani kutukomboa sisi wanadamu kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Amekwenda kuvikwa taji ya ushindi. Kristo ni mshindi ameshinda dhambi ambayo hupelekea kwenye mauti. Amepaa kupewa taji aliloandaliwa baada ya ushindi huo mkubwa ambao kwa kupitia huo tumepewa uwezo wa kwenda kwa Baba [Mk 16:19].
Kama vile Yesu anavyoingia katika utukufu wa Baba yake na kupata tuzo, ndivyo itakavyokuwa kwa kila mmoja wetu siku ya mwisho iwapo alijifananisha na Kristo kwa kutimiza mapenzi ya Mungu Baba, kwa kuishi kulingana na Amri zake ndiye huyo atakayeshiriki pamoja na Kristo utukufu Mbinguni. Na nafasi ya kushiriki utukufu huo pamoja na Kristo iko wazi kwa kila mmoja wetu: tukianzia kwa watoto hadi kwa wazee, masikini kwa matajiri, kila mtu ana nafasi yake kushiriki utukufu huo, ambao Bwana wetu Yesu Kristo leo tunamshangilia kupata kwake.
Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kule tu kufufuka kwake, aliingia katika utukufu wa mbinguni (Yn 20:17). Alikwenda kuzichukua roho zilizokuwa kuzimu mara tu baada ya kifo chake. Kisha akalifungua pazia la Mbingu na kuingia pamoja na roho za watakatifu (Uf. 7:14; 14:2). Hivyo hakukuwa na wakati fulani uliopita kutoka ufufuko mpaka kupaa. Ndiyo maana mmojawapo wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja na Yesu alisema, “Ee Yesu nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako,” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” (Lk 23:42-43).
Hata hivyo, Bwana wetu Yesu Kristo alijitokeza mara nyingi kwa wafuasi wake na mitume kwa muda wa siku arobaini, na leo ndio siku arobaini tangu ufufuko wake, ili wapate kuamini kuwa amefufuka. Mitume walipaswa kuamini kwanza wao habari za ufufuko ili baadaye waweze kuwatangazia wengine juu ya ufufuko wa Yesu, ambao ndio ulikuwa msingi wa mafundisho na imani yao (1Kor 15:14). Pia aliendelea kuwatokea kwa lengo la kuwaimarisha katika imani yao dhaifu kabla hajawatumia Roho Mtakatifu.
Kwa maneno mengine siku arobaini zinamaanisha muda wa kutosha wa maandalizi kumpokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste na Mwinjili Yohane anakazia hoja kusema Yesu alipaa mbinguni siku ileile ya Pasaka (Yoh 20:17). Kwa hiyo Yesu mfufuka aliishi mbinguni na kutoka huko aliwatokea wafuasi wake.
Hivyo tunaposema Yesu mfufuka alipaa mbinguni siku ya arobaini, tunakuwa na maana kwamba ndiyo siku ambapo alionana ana kwa ana na wanafunzi wake kwa mara ya mwisho mpaka atakapokuja mara ya pili katika utukufu wake. Na siku arobaini zinazotajwa hapa zisituchanganye, kwani zina maana ya muda wa kutosha kwa maandalizi ya kumpokea Roho Mtakatifu. Kwa Wayahudi huu ndio ulikuwa mtindo wa kuongea kwa njia ya namba kuwasilisha ujumbe fulani. Ndio maana namba arobaini (40) ingekuwa ya kimahesabu basi ingekuwa ngumu kuaminika kwamba Musa alikaa muda wa siku arobaini usiku na mchana bila kula wala kunywa maji kule mlimani Sinai alipofanya Agano na Mungu (Kut 34:28).
Ndugu zangu katika Kristo, Bwana wetu Yesu Kristo amepaa mbinguni ili kupokea tuzo kwa kazi aliyoifanya duniani, yaani kutukombo mimi na wewe kutoka utumwa wa dhambi na mauti na pili amepaa mbinguni ili kumtuma Roho Mtakatifu atukumbushe yote aliyotufundisha, atuimarishe katika imani na kutuongoza kama wafuasi wake. Na tatu amepaa mbinguni kwenda kutuandalia makao kwenye nyumba ya Baba (Yn 14:2-3).
Ndugu zangu katika Kristo, changamoto tunayopewa leo ni kwamba, maisha ya hapa duniani siyo ya umilele, tuna maisha ya umilele mbinguni Kristo aliko, hili ndilo tumaini letu. Kama ndivyo hivyo, tufanye nini tuweze kujifananisha na Kristo ili siku moja baada ya maisha haya tuweze kushiriki utukufu pamoja naye mbinguni?
Kwanza yatupasa tufuate agizo la Bwana wetu Yesu Kristo kwa wanafunzi wake la kwenda ulimwenguni kote kuhubiri injili kwa kila kiumbe (Mt 28:16-20). Kwa sababu sisi nasi kwa Ubatizo ni wafunzi wa Yesu, tulipokea neema ya utakaso na kutufanya tujiunge na Waamini wenye nia moja yaani kuwa watangazaji wa Habari Njema ya wokovu, na hivi leo tunatumwa kutekeleza wajibu huu. Tusiwatangazie wenzetu kwa maneno kisha matendo yetu yakapingana na kile tunachokisema. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatekeleza agizo la Yesu na hapo hapo kujifananisha naye. Na matokeo yake ni kupata tuzo baada ya maisha haya.
Kazi ya kuihubiri Injili, kubatiza inatekelezwa na Maaskofu wakishirikiana na wasaidizi wao Mapadre na Mashemasi
Pia tukiishi kulingana na amri za Mungu na za Kanisa hasa amri ya mapendo, tutajifananisha na Kristo aliyepaa mbinguni na hivyo kuwa na matumaini ya kushiriki pamoja naye utukufu mbinguni baada ya maisha haya. Hapa tutakuwa tunatimiza lile agizo la kuwa mashahidi wa Injili kwa kuishi amri za Mungu.
Na mwisho tukiishi kwa kupokea Sakramenti mbalimbali, mfano Sakramenti ya ndoa (uchumba miaka nenda miaka rudi ni hatari kwa afya ya kiroho) na Kitubio tutajifananisha na Kristo na siku ya mwisho tutakuwa na tuzo mbinguni. Nanyi wapendwa watoto, Yesu amepaa mbinguni, kuwaandalia sehemu ya kukaa na kufurahi, anasema: muwe na heshima, mfanye kazi, msiwe waongo, wachonganishi na wasababisha mafarakano katika jumuiya.
Ndugu zangu katika Kristo, Yesu Kristo amepaa mbinguni kwenda kututayarishia makao; tujiulize: Mimi kama mtu wa familia, mimi kama kijana ninayesoma, mimi kama mwalimu, mimi kama mlezi, mimi kama mtawa, mimi kama frateri mimi kama daktari, mimi kama shemasi, mimi kama Padre, nimejifananisha kiasi gani na Kristo ili siku moja baada ya maisha ya hapa duniani nishiriki utukufu pamoja naye mbinguni? Ni kwa muono huo tuinue macho juu kuomba huruma, tuinue mikono juu kupeleka sala na maombi yetu mbalimbali tukipaza sauti zetu juu kwa kuimba, kusifu na kushukuru ukuu wa Mungu unaotuangazia na kutuongoza kutoka juu.
Niwatakie Sherehe Njema ya Kupaa Yesu Mbinguni
Pd. Emmanuel KIMAMBO Nhanwa,
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu cha Navarra, Pamplona, Hispania.
© 2023 Ekinopia Studies
__________________________