TUMSIFU YESU KRISTO!
Roho Mtakatifu Njoo Mfariji wetu
Tunasherehekea Pentekoste ambayo ni utimilifu wa ahadi ya Kristo kuwatumia Roho Mtakatifu mitume wake.
Leo ni Sherehe ya Pentekoste. Pentekoste maana yake ni “ya hamsini”. Ni siku ya hamsini tangu tulipo sherehekea Jumapili ya Pasaka yaani Jumapili ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Sherehe hii tunaadhimisha ujio wa Roho Mtakatifu, tunakumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wa Kanisa. Tena Kanisa limeiweka Sherehe hii kuwa ni Sherehe ya waamini walei wote. Aidha kwa njia ya sherehe hii fumbo la Pasaka linakamilishwa, hivyo tunahitimisha kipindi cha Pasaka.
Wapendwa katika Kristo, Sherehe ya Pentekoste ilisherehekewa tangu Agano la Kale. Sikukuu hii iliitwa pia Sikukuu ya Mavuno, pia iliitwa Sikukuu ya Majuma. Asili ya Sherehe hii haifahamiki kwa hakika, hata hivyo kwa hakika ilikuwa ni sikukuu ya wakulima ambao baada ya kuvuna mazao yao ya kwanza, walimshukuru Mungu kwa yale waliyojaliwa na papo hapo kumwomba awajalie tena mavuno mema msimu ufuatao. Ndiyo maana iliitwa sikukuu ya mavuno. Iliitwa pia sikukuu ya majuma kwa vile ilisherehekewa majuma machache tu baada ya Pasaka ya Wayahudi. Hivyo ina maana kwamba Sherehe hii ilianza baada ya kuwekwa rasmi tarehe maalumu ya Pasaka ya Wayahudi, kwani wahusika wa Sherehe hii walikuwa ni Wayahudi au Waisraeli.
Kwa vile Waisraeli mwanzoni walikuwa ni wafugaji na watu wa kuhamahama inaonekana walianza kusherehekea Sherehe hii baada ya kutulia Kanaani na kuanza kilimo. Huenda waliiga sherehe hii kwa Wakanaani ambao walikuwa wakulima. Kadiri muda ulivyoendelea, polepole sherehe ya Pentekoste ilipata maana mpya ambayo ni ya kidini. Waisraeli walianza kuadhimisha sherehe ya Pentekoste kukumbuka siku Musa alipopewa amri kumi za Mungu mlimani Sinai (Rej., Kut 24:12-18; Amri zipo Kut 20:1-17; Kumb 5:6-21). Ni siku hiyo ambapo Taifa la Israeli lilizaliwa kwa kupewa kanuni rasmi za kuwaongoza, yaani Amri za Mungu. Sherehe hiyo sasa ilichukua sura mpya ikiwakumbusha tukio kubwa na la maana sana kwao yaani kuzaliwa kwa Taifa lao la Israeli.
Siku ya Mavuno
Na Maandiko Matakatifu yanadhihirisha hilo, “Nawe utaiadhimisha sikukuu ya mavuno ya nafaka pamoja na mazao ya kwanza uliyopanda shambani, na hatimaye sikukuu ya mavuno ya mazao mwishoni mwa mwaka unapokusanya mazao ya mashambani” (Kut 23:16). Kwa hiyo kitabu cha Kutoka sura 23:16 kinaamuru waisraeli waiadhimishe sikukuu ya mavuno. Halafu kitabu cha Mambo ya Walawi 23:15-22 pamoja na Kumbukumbu la Torati 16:9-12 vinaeleza jinsi ya kufanya maadhimisho hayo. Kwamba, “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku baada ya sabato”. Mtahesabu siku hamsini hadi siku baada ya sabato ya saba. Mtaleta kutoka katika mazao yenu mikate miwili. Pia beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka mmoja, kuwa dhabihu ya sadaka. Naye kuhani atavitakasa pamoja na mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana, pamoja na wale wana-kondoo wawili.”.
Kwa sababu hiyo, sherehe hii iliwekwa kati ya sikukuu za hija ambapo siku ya Pentekoste, toka sehemu mbalimbali wakulima wa Kiyahudi na waongofu walimiminika mjini Yerusalemu wakiwa wamechukua makapu yaliyojaa mazao. Makuhani na Walawi walisimama nje ya hekalu tayari kuwapokea watu. Halafu wote pamoja waliandamana kuingia hekaluni. Wakulima walibeba makapu yao hadi ndani ya hekalu kwa nyimbo na vifijo. Humo hekaluni makuhani walipokea mazao na kusali sala ya kumshukuru Mungu. Halafu kuhani kwa niaba ya waamini alitolea na kuinua mikate miwili isiyotiwa chachu, iliyotengenezwa kutokana na nafaka ya mavuno mapya ya mwaka huo.
Kumbe basi, katika hali hiyo ya sherehe na kusanyiko la mkutano huo mkubwa siku ya Pentekoste ya Kiyahudi, na Yesu akiwa ameshapaa mbinguni, Mitume kwa hofu ya Wayahudi walikuwa wamejifungia katika chumba, wakidumu katika kusali, wakisubiri ahadi ya Kristo, yaani ujio wa Roho Mtakatifu. Humo ndani ghafla kukaja upepo toka mbinguni, ukaijaza nyumba ile, zikatokea ndimi za moto zilizogawanyika zikiwakalia kila mmoja. Wote wakajawa Roho Mtakatifu, wakapata ujasiri wakatoka nje, wakaenda hekaluni kwenye kusanyiko wakaanza kuhubiri kwa nguvu habari za Yesu Kristo. Jambo la ajabu ni kwamba kila mtu aliyewasikia, alisikia na kuelewa kwa lugha yake aliyozaliwa nayo.
Katika mkutano huu lugha mbili tu zingetosha kusikika na kueleweka kwa watu wote waliokuwepo. Maana kwa uhakika Wayahudi waliokuwapo walifahamu Kiaramayo, tena wale waongofu walifahamu Kiyunani (Kigiriki) lugha ya Kimataifa ya wakati huo. Hivyo, Kiaramayo na Kigiriki zingetosha kueleweka kwa wote waliokusanyika. Hatujui Mitume waliongea lugha gani na ngapi. Hata hivyo, sisi tujue kuwa watu wote waliokuwepo toka sehemu mbalimbali waliwasikia Mitume na kuwaelewa kila mtu kwa lugha yake aliyozaliwa nayo. Maana yake ni kwamba, kwa mara ya kwanza katika maisha yao kundi hili la watu mbalimbali walisikia Neno la Mungu lililogonga moja kwa moja mioyoni mwao kwa namna ile iliyomfanya kila mmoja aelewe. Na mapato yake walibatizwa watu wapatao elfu tatu.
Kwa hiyo siku ya Pentekoste ya ujio wa Roho Mtakatifu kwa mitume ilikuwa ni rahisi kuwa na umati wa watu wengi na kushuhudia mitume wakiongea kwa lugha zao na kuelewana kwa sababu watu walikusanyika kwa sherehe ya mavuno wakitoka sehemu mbalimbali. Lakini kuanzia siku hiyo ikachukua sura nyingine siyo mavuno tena bali ujio wa Roho Mtakatifu siku ya 50 baada ya pasaka
Wapendwa katika Kristo, sisi Wakristo leo tunasherehekea Pentekoste ya Kikristo, yaani siku hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na ni siku chache tu baada ya Bwana wetu Yesu Kristo kupaa mbinguni. Ni siku ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume na mwanzo wa Kanisa la kwanza. Kama vile Wayahudi walivyosherehekea sikukuu ya mavuno ya kwanza, na baadaye kusherehekea sikukuu ya kupewa amri kumi za Mungu na kuundwa kwa Taifa lao la Israeli, vivyo hivyo na sisi tunasherehekea mambo matatu yanayofanana na hayo katika sherehe yetu hii:
Mosi, tunasherehekea mavuno makubwa ya Kanisa, ya wakristo waliobatizwa mara ya kwanza siku ile ya Pentekoste, watu wapatao elfu tatu. Aidha tunasherehekea mavuno ya Kanisa ya wakristo waliobatizwa Pasaka ya mwaka huu 2023. Wote hawa wamejazwa Roho Mtakatifu na wanatenda matendo makuu ya Mungu. Haibagui taifa, rangi, jinsia, Kabila na hata uwezo wa mtu kiuchumi au maendeleo.
Pili, tunasherehekea ujio wa Roho Mtakatifu; siku ya Pentekoste, ambapo Roho Mtakatifu alionekana kuwashukia Mitume. Tusidhani kuwa Roho Mtakatifu alianza kuwepo siku ya pentekoste. La hasha! Yeye ni Mungu nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, hana mwanzo wala mwisho, ila tu siku ya Pentekoste alijidhihirisha kwa namna ya pekee. Kwa maana, Roho Mtakatifu yupo tangu hata kabla ya nyakati akitenda kazi katika umoja na Baba na Mwana. Utume wake huu hata hivyo ulibaki umejificha hadi ulipowadia utimilifu wa nyakati alipomininwa ulimwenguni. Roho Mtakatifu amekuwapo katika uumbaji akitulia juu ya uso wa maji (Rej., Mwa 1:2). Ameshiriki kumuumba mwanadamu pamoja na vitu vyote, tumfanye mtu kwa sura na mfano wetu (Rej., Mwa 1:26-27).
Hili linadhihirika wazi katika maneno ya Mt. Ireneo anaposema, “Mungu amemuumba mwanadamu kwa mikono yake mwenyewe yaani Mwana na Roho Mtakatifu na juu ya mwili ulioumbwa alitengeneza sura yake mwenyewe hivi kwamba kile kilichoonekana kilichukua sura ya Mungu” (Rej., KKK, n. 704). Ni Roho Mtakatufu aliyewaongoza waisraeli kutoka Misri kuelekea nchi ya ahadi, mchana akiwa mbele yao kama wingu na usiku kama mnara wa moto (Rej. Kut 13:21). Roho huyu ndiye aliyenena kwa vinywa vya manabii akiwafundisha kulishika Agano na kumtumainia masiha ajaye.
Tuwaombee wote waliojiweka wakfu katika Roho Mtakatifu wakatimize kazi yao ya wakfu kwa furaha na amani.
Hivyo basi, wote wanaoshukiwa nae hujazwa mapaji yake saba. Hivyo, Roho Mtakatifu, ndiye anayeliongoza Kanisa kuwachagua viongozi wa Kanisa, kuwapeleka anakopenda wakafanye utume wao, anawajalia hekima katika utume na kuwasaidia katika maamuzi, anawasaidia wahubiri wa Injili kuhubiri vema, na kuongoza usomaji wa Maandiko Matakatifu. Tena Roho Mtakatifu huwajalia watu vipaji mbalimbali kwa ajili ya Kanisa lote na kwa ajili ya wanakanisa wote, kwa ajili ya wokovu wa wote na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Vipaji hivyo ni kama vile hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu. Karama zingine ni kama vile unabii, Uponyaji, ualimu, kunena kwa lugha na nyingine nyingi. Hivyo basi, yatupasa kutambua karama hizo zote.
Leo hii kutokana na matatizo yatuzungukayo baadhi ya waamini wa Madhehebu mbalimbali, hata ndani ya Kanisa letu wanaonekana kukazia zaidi karama mbili tu yaani uponyaji na kunena kwa lugha. Roho Mtakatifu si fukara wa vipaji, anavyo vingi sana kama vile hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu. Vipaji hivyo na vingine vingi ambavyo hatujavitaja vipo kwa ajili ya kuhudumiana na kujengana, yaani kwa lugha nyepesi ni kufaidiana sisi wenyewe. Yatupasa kuvitambua vipaji hivyo vyote kuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu. Tukumbuke kuwa imani inayotegemea miujiza tu haina nguvu, tena ni imani isiyo ya kweli. Aidha, kuna hatari kubwa ya kuingiza utapeli katika ile tudhaniyo kuwa ni miujiza. Vipaji tulivyonavyo viwe kwa manufaa ya wote. Na tujue kuwa karama kubwa kuliko zote ni upendo. Basi sasa, mambo matatu yanadumu: imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu kati ya haya ni upendo (Rej., 1Kor 13:13).
Tatu, tunasherehekea kuzaliwa kwa Kanisa. Taifa la Israeli lilizaliwa siku ya kusanyiko mlimani Sinai, yaani siku ya mkutano. Siku ya mkutano wa kusanyiko la Yerusalemu Taifa la Mungu la Agano jipya, Israeli mpya yaani Kanisa lilizaliwa. Wote wakajazwa Roho mtakatifu wakatenda matendo makuu ya Mungu. Utume rasmi wa Kanisa ulianza.
Tukumbuke pia kuwa Roho Mtakatifu anakuja bado kwetu katika sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Roho huyo hutujalia vipaji mbalimbali. Tuzikimbilie sakramenti hizo na kutumia vema vipaji vyetu tulivyojaliwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya kufaidiana. Pia tuviheshimu vipaji vya watu wengine ambao nao wamejaliwa kuwa navyo. Kwa nini uwe na majivuno kwa sababu ya kipaji ulichojaliwa na Roho mtakatifu? Kwa nini udharau kipaji cha mwenzako? Kwa nini uwe na wivu mbaya kwa kipaji cha mwenzako ambacho wewe huna?
Tudumishe umoja katika Kanisa, sio sisi na Yesu Kristo tu bali hata sisi kwa sisi. Muujiza wa Pentekoste ulirudisha umoja uliopotea huko Babeli. Huko Babeli kwa sababu ya majivuno watu walitaka kujenga mnara mpaka ufike Mbinguni kwa Mungu. Mungu akawachafulia lugha yao wakashindwa kuelewana na hivyo hawakufanikiwa kumaliza kuujenga mnara (Rej., Mwa 11:1-9). Muujiza huu uwe mfano wa utume wetu katika dunia yote bila ubaguzi wa rangi, jinsia, kabila, utaifa, ukanda, ujimbo au parokia, ili watu wote wapate kulisikia Neno la Mungu, ili wapate kuliishi na kuokoka.
Familia ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji.
Wapendwa katika Kristo, kwa Ubatizo wetu na Kipaimara wote tumejazwa Roho Mtakatifu yatupasa kuongea lugha moja tu, lugha ya upendo kwa wote, lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Upendo haufifii kamwe kwani wadumu mpaka Mbinguni. Ni fadhila ya Kimungu iliyotofauti na nyingine kwani mwisho wake si hapa duniani. Hakuna mtu wa rangi, kabila, au taifa lolote ambaye haelewi lugha ya upendo. Roho Mtakatifu ni Roho wa ukweli, uhuru na upendo. Tupendane ili tuwe jamaa moja tukithibitisha umoja wetu na Mungu na sisi kwa sisi; kwani wote tumejazwa Roho Mtakatifu kwa Sakramenti za Ubatizo na Kipaimara. Tutoke nje na wote tutakaokutana nao leo tuwanenee neno la Mungu nao wapate kustaajabu nguvu tuliyonayo, waseme mbona tunasikia wayasemayo kwa lugha yetu.
Aidha, katika Sherehe ya Pentekoste Fumbo la Pasaka hukamilika maana ni katika sikukuu hii Roho Mtakatifu hulishukia Kanisa ili likaendeleze kazi ya Kristo bila woga, likiwa na nguvu za kimungu. Ni sikukuu ambayo kwayo Roho Mtakatifu huthibitisha muungano wetu na Mungu. Ujumbe wa Neno la Mungu unakazia katika Roho Mtakatifu kuwa sheria mpya na nguvu ya Wakristo, taifa jipya la Mungu lililoshikamana katika upendo na Mungu.
Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo wa Roho Mtakatìfu katika Kanisa na katika maisha ya waamini na ni siku ya kuomba kuimarishwa kwa mapaji yake saba na kujazwa na matunda yake ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi kama anavyofundisha mtume Paulo (Rej., Gal 5:22). Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu ya Mungu mmoja. Ni jina halisi la yule ambaye tunamwabudu na kumtukuza pamoja na Baba na Mwana. Kanisa limempokea Roho Mtakatifu kutoka kwa Bwana na linamuungama katika ubatizo wa watoto wake wapya. Licha ya jina lake hili halisi, Roho Mtakatifu anaitwa pia mfariji, msaidizi, mtakasa, Roho wa Bwana, kidole cha Mungu na Roho wa Mungu.
Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii tutambue kuwa ni wakati wakujitambua sisi ni nani na thamani tuliyonayo kama Kanisa Katoliki ambalo ndiyo Kanisa lililoanza rasmi siku ya Pentekoste. Hivyo tutambue kuwa kanisa hili linasifa au alama nne tofauti na makanisa mengine kama tunavyokiri kwenye Kanuni ya Imani ya Nicea. Ni Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Tumwombe Roho Mtakatifu atuimarishe ili tusimame imara na tusipeperushwe na kusahau misingi ya imani yetu. Kwa ubatizo tumefanywa kuwa wanakanisa. Hakuna sababu ya kuhangaika mara leo huku kesho kule. Kanisa Katoliki ndiyo mama na mlezi wetu.
OMBI
Jumuika pamoja nami kufanikisha uchapaji wa vitabu vitatu vya imani na uinjilishaji vilivyoandikwa nami, na Mungu atakubariki sana. Unaweza kutuma mchango wako kwa njia ya M-Pesa kwenda namba +255754985663 (Emmanuel Kimambo Nhanwa) au bonyeza HAPA.
Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa,
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.
©2023 Ekinopia Studies
------------------