Sikukuu Ya Utatu Mtakatifu

TUMSIFU YESU KRISTO! 
Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu.

Utangulizi 
“Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…” Imani inatuambia kwamba nafsi hizo tatu za Mungu siyo Miungu watatu bali Mungu mmoja. Mungu mmoja katika Nafsi tatu! 

Karibu ndugu katika Kristo Bwana, katika tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Na kwa kuwa ni fumbo la imani, imani tu, imani tu, yaelewa. Kumbe lengo la tafakari katika sherehe hii siyo kuwaelewesha namna ambavyo nafsi tatu katika Utatu Mtakatifu zilivyoungana na kufanya Mungu mmoja. La hasha. Shabaha ni kujaribu kukufahamisha jinsi Utatu Mtakatifu unavyofanya kazi katika maisha yetu na kutukuza Utatu Mtakatifu ambao ni Mungu mmoja. Hili linajidhihirisha katika maadhimisho mbalimbali ndani ya liturujia na katika maandiko matakatifu na mapokeo ambako tutajaribu kudodosa uwepo wa nafsi hizi tatu, katika Mungu Mmoja. 

Ufafanuzi 
Nilipokuwa nasoma na kutafakari juu ya Utatu Mtakatifu, nimekutana na waandishi kadha wa kadha. Wengine walinikatisha tamaa na nikachoka sana. Hata hivyo sikukata tamaa niliendelea kusoma na kutafakari kila mara. Na hapo wingine wakanitia matumaini kuwa naweza elewa kitu kidogo juu ya sikukuu ya leo. Na hii ilinipa nguvu ya kuweza kuendelea kutafakari na kuja na mang’amuzi haya juu ya leo, kwamba utatu mtakatifu ni upendo ambao Mungu amependa kumfunulia na kumshirikisha mwanadamu. Na hili linajidhihirisha katika namna yetu ya kutenda katika maadhimisho mbalimbali ya Liturujia. 

Ndugu zangu, mara zote katika maadhimisho ya liturujia na sala nyingine za Kikatoliki tunaanza kwa kufanya ishara ya msalaba tukitamka maneno; “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu”. Maneno hayo yalitamkwa na Padre wakati wa; Ubatizo wetu: Padre anapombatiza mtu, anapommininia maji katika paji la uso anasema; "Nakubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu." Kabla yake huwa tunajibu “Nasadiki” kwa kujibu maswali matatu yanayotudai na kututaka kuungama Imani yetu kwa Baba, kwa Mwana na kwa Roho Mtakatifu. Imani ya wakristo ni juu ya Utatu (Rej., KKK, n.232-233). 

Wakati wa kupokea ondoleo la dhambi katika Sakramenti ya upatanisho Padre anasema: nami nakuondolea dhambi zako “kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu." Aidha, Mmoja anapoadhimisha Sakramenti ya Ndoa baada ya kuonesha ukubaliano wao mwanandoa anamwambia mwenzi wake kuwa: “Mwenzangu pokea pete hii iwe ishara ya upendo na uaminifu wangu kwako: “kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” 

Mtu anapokaribia kufa tunasali sala hii: “Ee, Mkristo, uondoke sasa duniani, katika Jina la Baba aliyekuumba, kwa Jina la Kristo aliyekukomboa, na katika Jina la Mungu Roho Mtakatifu aliyekutakasa.” Na Siku ya Mazishi: Padre au kiongozi wa ibada anapoweka msalaba juu ya Kaburi anasali: “Uandikwe ishara ya Msalaba mhuri wa ukombozi wetu upumzike kwa amani. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanaunda Utatu Mtakatifu. Hii ni imani juu ya Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu: Baba aliye Muumba, Mwana aliye Mkombozi, Roho Mtakatifu aliye mwalimu na Mfariji. 

UTATU MTAKATIFU NI NINI? 
Katika sikukuu ya leo tunaheshimu Nafsi Tatu za Utatu Mtakatifu. Leo kwa namna ya pekee, tunakumbuka Utatu Mtakatifu ambao ni Umoja Mtakatifu. Umoja usiogawanyika kamwe. Umoja unaofumbata Imani yetu. Ni kanuni na dira ya kutuongoza katika maisha yetu ya ufuasi kwa Kristo Yesu. 

Lakini Utatu Mtakatifu maana yake nini? 
Katika Katekisimu tunajifunza kuwa kuna Mungu mmoja. Kwake kuna Nafsi Tatu, ijapo tofauti lakini Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu, Roho Mtakatifu ni Mungu [Mungu Mmoja]. Wote wana hekima sawa, ni wema sawa na wana uwezo sawa yaani siyo miungu watatu bali Mungu mmoja. Hii ndiyo imani yetu. Tunasadiki siyo kwa sababu ya utambuzi wetu bali Mungu mwenyewe ametufunulia hivyo. Imani hii ni Fumbo ambalo malaika na wanadamu hawawezi kulielewa kwa ukamilifu (Rej., KKK, n. 237). 

Kuna simulizi maarufu kumhusu Mtakatifu Augustino wa Hipo, Mwana Falsafa na Mteolojia mkubwa na Askofu wa Hipo katika Kanisa Katoliki, alikuwa mara nyingi anahangaika ili aweze kulielewa Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu, akilenga kulielewa tena kwa ufasaha. Mt. Augustino aliishi Afrika ya Kaskazini, alikuwa mtu mwenye hekima na mtakatifu na askofu wa jimbo la Hippo. 

Siku moja alikuwa anatembea ufukweni mwa bahari akitafakari juu ya Fumbo hili, akamwona mtoto mdogo akichimba kashimo kidogo, yule mtoto baada ya kuchimba lile shimo akawa anachukua maji na kikombe kidogo kutoka katika bahari ile na kukijaza kishimo chake alichotengeneza katika mchanga ule. 

Mt. Augustino alimtazama jinsi mtoto yule alivyokuwa akienda baharini kuchota maji na kumimina katika kishimo kile. Ndipo Mt. Augustino akamwendea yule mtoto na kumwuliza: “Unafanya nini wewe mtoto mdogo? Yule mtoto akamjibu: Ninataka kuihamishia bahari hii kuingiza katika kishimo hiki” Mt. Augustino akamhoji, unafikiri kwamba unaweza kutimiza hamu yako hii kuihamishia bahari katika kishimo hiki? Haiwezekani! Bahari ni kubwa mno na hiki ni kishimo kidogo. Mtoto akatabasamu kisha akamwambia, hilo ndilo unalolifanya Baba Askofu. Mungu ni zaidi ya bahari. Akili yako ni ndogo kuliko hiki kishimo. Unaweza kuelewa ukuu wa Mungu? Hutaweza kuelewa fumbo la Utatu Mtakatifu. Baada ya kusema hayo yule mtoto akatoweka. Hakuna anayeweza kumwelewa Mungu ila Mungu anaweza kujielewa mwenyewe. 

Fundisho kuhusu mahusiano ya ndani ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, kwamba wote wako sawa, na tena hakuna Mungu wa tatu ila Mungu Mmoja unabaki kuwa fumbo. Hakuna mwanadamu anayeweza kuelewa kikamilifu fumbo hili (Rej., KKK, n.253). 

Kama tukifikiri kwamba masomo ya leo yatatupa mafundisho na ufafanuzi makini kuhusu fundisho hili la Utatu Mtakatifu, hakika tunagundua kwamba hayafanyi hivyo. Fundisho la Utatu Mtakatifu katika Mungu mmoja, sawa katika Umungu, lakini tofauti katika nafsi, linaelezwa wazi katika Biblia. Ukweli ni kwamba neno Utatu” halipatikani katika Maandiko ila tunapata madokezo yakutosha juu ya fundisho hili msingi la Imani-halitajwi waziwazi. 

Kama Mtakatifu Augustino, hatuwezi kuelewa jinsi ya utendaji wa Utatu Mtakatifu, lakini ni muhimu kuelewa kwa nini Mungu alitufunulia fumbo hili ijapo kwa kiasi fulani. Mungu alitufunulia fumbo hili kwa sababu sisi tumeumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu mwenyewe (Mw 1:26-27). Kwa hiyo jinsi tutakavyomwelewa Mungu, tutajielewa sisi wenyewe vizuri zaidi. Wataalamu wa mambo ya dini wanatuambia kwamba watu hutaka kufanana na Mungu wanayemwabudu. Watu wanaomwabudu Mungu ambaye ni shujaa na jemedari, hupenda kuwa watu wa vita, utawala na mamlaka. Watu wanaomwabudu mungu wa starehe, huwa ni watu wanaopenda sana kujistarehesha kwa gharama yeyote, Watu wanaomwabudu mungu aliye mwingi wa hasira wana tabia ya kulipa kisasi, Watu wanaomwabudu mungu anayependa, huwa ni wakarimu na watu wanaopenda. Kama Mungu kama muumini. Kwa hiyo swali la msingi la kujiuliza leo hii ni kwamba: Utatu Mtakatifu unatueleza nini kuhusu Mungu tunayemwabudu? Na hilo linatuambia nini juu ya imani yetu na jinsi tunavyopaswa kuwa? 

Tuone sasa dokezo la UTATU MTAKATIFU katika mapokeo na Biblia ili tuwe na uhakika na kile tukiaminicho kuwa kinamsingi wake katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya kanisa. 

AGANO LA KALE 
Katika agano la Kale kitu kinachooneshwa ni kivuli cha uhalisia wa kile kitakachokuja kudhirishwa katika Agano Jipya. Hapa tunapata viashiria vya utatu mtakatifu. Katika historia ya Uumbaji, Mungu anatumia maneno yanayoonesha nguvu ya uwingi, kwamba kuna zaidi ya nafsi moja, “Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa sura na mfano wetu, afanane nasi” (Mw 1:26). Aidha, katika kitabu hicho hicho andiko jingine la sema “kisha Bwana Mungu akasema: Tazama, mtu amegeuka na kuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya” (Mw 3:22). Pia, tunaposoma Mw 11:7 inasema, “haya, tushuke, tukavuruge lugha yao, wasipate kusikilizana wao kwa wao”. Nabii Isaya anapotaja zile mtakatifu mara tatu ni kielelezo na dokezo la utatu mtakatifu. Ndiyo maana Mt. Ireneo wa Lyion, yeye alizielewa hizi haya kuwa Mungu alipokuwa anasema katika uwingi alikuwa anawataja Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu (St. Irenaeus, Adv. Haer IV, 20, 1). 

AGANO JIPYA 
Hili linajidhihirisha bayana katika Agano jipya ambapo hizi nafsi tatu za Utatu Mtakatifu zinatajwa wazi wazi bila chenga. Hili linajitokeza katika mtukio kadha wa kadha. 

Tunaposoma simulizi la kupashwa habari Maria, Malaika anasema: “Roho mtakatifu atakushukia, na nguvu ya yule Aliye –juu itakufunika kwa kivuli chake. Kwa hiyo kitakatifu kitakachozaliwa kitaitwa mwana wa Mungu” (Lk1:35). 

Katika ubatizo wa Bwana Wetu Yesu Kristo, tunaona kuwa Mwana anabatizwa na mbingu zinamfungukia, na Roho Mtakatifu akamshukia kwa mfano wa njiwa. Na sauti ya Baba inamtangaza Kristo kwamba: Huyu ni mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye (Mt 3:16-17; Jn 1:32-34; Lk 3:22). 

Mwana anabatizwa, Roho Mtakatifu anashuka kama njiwa na Baba anasema

Katika mlo wa mwisho Kristo aliwaambia wafuasi kwamba, “Nami nitamwomba Baba, naye atawapelekea mtetezi, msaidizi mwingine, ili awepo kwenu hata milele (Yn 14:16). Na katika aya 26 majina yanatajwa waziwazi, kuwa “Lakini mtetezi, ndiye Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisha na kuwakumbusha yote niliyowaambia mimi (Yn 15:26). 

Vilevile, pindi Yesu alipokuwa anawapa mamlaka mitume nafsi zote tatu zinatajwa, “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatatifu” (Mt 28:19). Hizi aya zote zinadhihirisha uwepo wa Utatu Mtakatifu katika Maandiko Matakatifu. 

Katika mapokeo, Utatu Mtakatifu unajidhihirisha katika Kanuni ya Imani ambapo, Mungu Baba anaumba, Mungu Mwana anakomboa na Mungu Roho Mtakatifu anatakatifuza, analeta uzima wa kimungu ndani yetu. Hii inaendelea kudhihirisha kuwa fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo fumbo la msingi la Imani na la maisha ya kikristo. Ni fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hiyo ni chanzo cha mafundisho mengine yote ya Imani, nuru inayoyaangazia. Ni fundisho lililo la msingi na la lazima katika hierakia au ngazi ya kweli za Imani. Historia yote ya wokovu siyo kitu kingine ila ni historia ya njia, na jinsi ambazo Mungu wa kweli na wa pekee, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, anavyojifunua mwenyewe, anavyowapatanisha, na kuwaunganisha naye watu waliojitenga naye kwa dhambi (Rej., KKK, n.234). 

Imani tu Yatosha, Imani tu yaelewa 

Ni wazi kwamba hakuna lugha ya wanadamu inayoweza kueleza maajabu na maisha ya kimungu katika Nafsi Tatu za Mungu. Hata hivyo cha maana siyo sisi kutaka kujua kinachoendelea katika Utatu mtakatifu, cha msingi ni sisi kutambua kuwa sisi nasi tumeitwa kushiriki maisha ya kimungu katika fumbo la utatu mtakatifu. Chanzo cha maisha haya ni Sakramenti ya Ubatizo, inayohuishwa na kutegemezwa katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Kipaimara na Upatanisho. 

Tunapokuwa hapa duniani tunashiriki maisha haya ya Kimungu kwa kiasi fulani tu. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuandaa tuweze kushiriki maisha hayo ya Kimungu katika ukamilifu wake tutakapofika mbinguni. Kwa maneno mengine, wakati tunaishi hapa duniani, Roho Mtakatifu anaendelea kutufundisha kwa uvumilivu mkubwa namna tunayopaswa kumpenda Mungu na ndugu zetu. Tunapaswa kupenda kama Mungu anavyopenda, pasipo kuhesabu gharama. 

Kwa namna hii, Roho anaendelea kutufunza hatua kwa hatua ili tuwe watoto wapendwa katika familia ya Mungu, kuliko kuwa watoto watukutu, wagomvi, wasio na maadili na watenda dhambi kama inavyoonekana mara nyingi. 

MWISHO 
Fundisho la Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya kikristo. Ni fumbo asili la imani na maisha ya Kikristu. Kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa huruma, wema na upendo ambavyo ni asili ya Mungu. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa hata ukombozi kwa njia ya Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu, ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na yule aliye upendo wenyewe, yaani Mungu Baba (Rej., 1Yn 4:7-8).

Mtakatifu Thomaso wa Akwino aliyejaliwa uelewa mkubwa na wa hali ya juu wa mambo yamhusuyo Mungu katika wimbo tunaouimba wakati wa kuabudu Ekaristi Takatifu anasema; “waficha Umungu msalabani, na ubinadamu altareni, mafahamu yangu yadanganya yanapokuona, nami nasadiki bila haya”. Mtume Paulo naye anasema: “Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtumpu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Maandiko yasema, nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Lakini sisi tunayo akili ya Kristo (1Kor.2:13-16). Mt. Thomaso wa Akwino anashauri kwamba: “ukikutana na lolote ambalo hulielewi ama katika Biblia au katika mafundisho ya Kanisa usiseme mambo haya hayaeleweki au yamekosewa bali useme akili zangu ni ndogo kuelewa ukweli huu.” Fanya juhudi kuelewa utakavyoweza. Yatakayokushinda “Inamisha kichwa mpaka nchi na kusema pamoja na mtakatifu Hipoliti kuwa; “nasadiki kwa kuwa sina uwezo wa kueleza”. 

Imani katoliki ndiyo hii: tumwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo: kwani ni nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana, nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja, wa Baba, wa Mwana na wa Roho Mtakatifu, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja milele (KKK, n.266). Amina. 

OMBI
Jumuika pamoja nami kufanikisha uchapaji wa vitabu vitatu vya imani na uinjilishaji vilivyoandikwa nami, na Mungu atakubariki sana. Unaweza kutuma mchango wako kwa njia ya M-Pesa kwenda namba +255754985663 (Emmanuel Kimambo Nhanwa) au bonyeza HAPA.

Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.

©2023 Ekinopia Studies