Tumsifu Yesu Kristo...
![]() |
Hakuwa Mzuri Kiasi Kwamba Tumtamani (Is 53:2b) |
Wapendwa katika Kristo Bwana, tunaweza kujiuliza, ni nani huyo ambaye hakuwa mzuri kiasi kwamba tumtamani? Kwa nini alikuwa hivyo? Au ni kitu gani kilichopelekea yeye kupoteza uzuri wa umbo lake? Je, ni kwa sababu yake mwenyewe au kuna kitu kingine kilichopelekea yeye kuwa hivyo? Kama ni kitu, je, kitu hicho ni kipi? Tusafiri pamoja katika tafakari hii, ili uweze kujitajirisha kimaarifa na kiroho.
Katika historia ya uumbaji tunaona kuwa vitu vyote alivyoviumba Mungu vilikuwa vyote vizuri (Mwanzo 1:31). Na ni ukweli usiopingika kuwa dhambi ilipoingia ilitufanya, sisi wanadamu tupoteze ile hali ya neema ambayo Mungu alituumba nayo. Katika kitabu cha mwanzo sura ya tatu tunaona anguko la mwanadamu linatokea. Dhambi inaingia ulimwenguni, uovu unaathiri maisha ya walimwengu. Hali hii ndiyo iliyopelekea mwanadamu kupoteza uzuri aliojaliwa hapo mwanzo wa uumbaji.
Ni nani huyo ambaye hakuwa na uzuri kiasi kwamba tumtamani? Kwetu sisi waKristo, huyu ni Kristo Bwana, aliyesulubiwa, akateswa, akatundikwa msalabani na akafa juu yake. Kwa nini alikuwa hivyo? Alipoteza uzuri (hali ambayo kila mara inatudai kubadili mwenendo wa maisha yetu ya kiroho) wa umbo lake kwa sababu ya dhambi zetu; yaani sisi wanadamu. Hii haikuwa kwa ajili yake bali kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu, kumtoa katika utumwa wa dhambi.
Nabii Isaya alitabiri hayo yote juu ya mtumishi mwaminifu-Kristo “maana alikua mbele zake kama mche mwororo, na kama mzizi katika nchi kavu. Yeye hana umbo wala uzuri; na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani” (Cf. Is 53:2; 49:7; Zab 22:6; Mk 9:12). Kristo alipoteza uzuri wa umbo lake kwa ajili ya kuwakomboa watu wote kutoka dhambini. Tunaposema kuwa Kristo hakuwa na umbo wala uzuri wa kuvutia machoni na hapakuwa na aliyemtamani, ni mwaliko kwetu kuchuchumalia matakatifu na kuepuka nafasi za dhambi pamoja na kuvua kwa nguvu mioyoni mwetu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu urafiki na Mungu, hata ikitupasa kutoa sadaka kubwa. Kwa mateso makali Kristo alipoteza uzuri wa umbo, maana mwili wote ulikuwa umeloana na umejaa damu (cf. kitu cha njia ya Msalaba no. 9 na 10). Lakini Kristo alikuwa na uzuri wa nafsi (Roho) na utashi, ambao kila mmoja wetu anaalikwa kuutafuta, kwa kuishi kulingana na mpango, na mapenzi ya Mungu.
Binadamu huwa tunaona ule uzuri wa nje nasiyo ule uzuri wenyewe, yaani uzuri halisi (real beauty) ambao wanadamu hawakuweza kuuona katika mateso ya Kristo. Kristo alipoteza uzuri wa umbo lake la nje, aliteseka ili wanadamu wapate tena uzuri wa ndani waliokuwa wameupoteza kwa kumuasi Mungu na kugeukia lile lililo ovu. Hivyo, kwa kifo cha Kristo msalabani, ile hali ya neema ambayo wanadamu walioipoteza waliipata tena, neema ambayo inatupatia uzuri wa nafsi, wa kiroho ambao unaambatana na faraja, Amani, matumaini na ukombozi wa wanadamu. Maana Kristo licha ya yeye kuwa mwanadamu lakini hakutenda dhambi (cf. Heb 4:15). Hivyo alipoteza uzuri wa umbo lake si kwa ajili yake bali kwa ajili ya dhambi za wanadamu, na hivi apate kuwakomboa kutoka utumwa wa dhambi (cf. Heb 2:17).
Kwa hali ya kawaida ili kitu kiwe kizuri kwa umbo la nje, ambalo Kristo alipoteza; kwa kiasi kikubwa hutegemea sifa zifuatazo: kwanza, uwiano (harmony, proportionality or balance) wa kile tunachokiona na tukifaamucho; pili, ukamilifu (completeness or integrity) katika muonekano wake, yaani medani ya nje (external forum). Kwa mfano, tunategemea mtu wa kawaida awe na miguu miwili, macho au masikio mawili, na si vinginevyo. Tatu, uwazi (clarity), uzuri hauwezi kujificha, hujionesha. Sifa hizi Kristo alionekana kutokuwa nazo kwa sababu ya dhambi zetu, kipindi alipoteseka na kusulubiwa msalabani. Kwa nini hakuwa na sifa hizo? Kwa sababu ya dhambi zetu. Hivyo basi, dhambi zetu huwa hazitufanyi tupoteze uzuri tulionao bali huharibu pia uzuri wa wenzetu. Katika anguko la kwanza la mwanadamu, Adamu na Eva walipoteza uzuri wa nafsi, wa roho pale walipomuasi Mungu na kugeukia lile lililo ovu, wakapenda uzuri wa muda (apparent beauty); ambao ulipelekea kutofautiana na Mungu wao. Hawakuwa tena safi, wazuri kwa sababu ya dhambi zao. Laana iliwekwa juu yao na ikaathiri uzao wao wote (cf. Mwa 3:17-19).
Hata hivyo, Mungu hakumwacha huyu mwanadamu aendelee kupotea na kumuasi. Aliendelea kumtumia viongozi waweze kumsaidia kurudi katika njia iliyo njema. Akamtumia mababu, manabii, waamuzi, wafalme na wengine wengi. Hata hivyo haikuishia hapo, wakati ulipowadia alimtuma mwanae wa pekee (cf. Gal 4:4), Kristo Bwana ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi. Katika kutimiza hilo, Kristo alionekana kama kituko. Maana aliteswa, alitemewa mate, alitundikwa msalabani na mwishoe akafa juu yake. Lakini bado hawa wanadamu hawakuweza kutambua upendo wa Mungu kwao, kama Mwinjili Yohane anavyobainisha: “kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu upate kuokolewa katika Yeye” (cf. Yn 3:16-17).
Sisi sote tumekombolewa kwa damu azizi ya Kristo. Tunapoendelea kutenda dhambi tunaendelea kutonesha madonda ya Kristo msalabani na kurudisha maumivu aliyoyapata pale alipoteswa. Kwa kutenda dhambi tunazidi kuongeza tena uzito wa msalaba badala ya kupunguza kwa kuacha dhambi. Vituo vya njia ya msalaba, cha tatu, saba na tisa vinaeleza jinsi dhambi inavyochosha na kumpelekea Kristo kuchoka, hata kuanguka. Katika kituo cha tatu, Yesu anaanguka chini ya msalaba kwa ajili ya udhaifu – tunaalikwa kumuomba Kristo asituache tukabaki katika tamaa tukaanguka dhambini, tusimame mara moja na kumfuata yeye, ili uzuri wa kiroho alionao nasi tuwenao. Kituo cha saba,Yesu analegea mno kwa mateso makali…kwa ajili ya udhaifu wa mwili, anatuonya kwamba hata sisi tunaweza kurudi dhambini kwa udhaifu wa moyo. Tunavutwa kuomba neema ya kuepuka nafasi za dhambi na visa vyenye kutukwaza na kuturudisha dhambini. Lakini kituo cha tisa, Kristo anaonekana amedhoofika kwa mateso anaanguka mara ya tatu apate kutustahilia neema ya kuitisha miili yetu na kuisulubisha, licha ya kuepuka nafasi za dhambi (Cf., Kituo cha Njia ya Msalaba no. 3; 7 na 9). Hayo yote yalitokea ili kutufundisha daima kuchuchumalia wito msingi, yaani kuwa watakatifu. Kwa mwili wote wa Kristo kuchoka na kuloana damu ni kiashiria na mwaliko tosha kwetu kuacha njia ya dhambi na kugeukia lililo jema. Hivyo, tukishupaa katika dhambi au uovu, tunaendelea kumfanya Kristo asiweze tamanika kwa yeyote. Bali, matendo yetu mema ndiyo mafunzo tosha kwa kuwavuta wengine kwa Kristo na kupunguza uzito wa msalaba wake.
![]() |
Sakramenti ya Kitubio ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo. |
Wajibu wetu kama wakristo ni kuendelea kujitakatifuza zaidi na zaidi kwani sisi ni wachafu, wadhambi tangu tumboni mwa mama zetu kama Mzaburi anavyotueleza, “Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu, mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu” (cf. Zab 51:5; 35:1ff). Mwito wetu ni kuacha dhambi na kutenda mema. Kwa mfano, Kristo kama Baba anayeteseka kwa ajili ya mwanae, je, mwanae anaweza kuendelea kutenda dhambi iliyo chanzo cha mateso kwa Babae? Je, mwana aweza kuendelea kutenda dhambi? Kama siyo, kwa nini wakristo tunaendelea kutenda dhambi, ili hali Kristo ametufia msalabani? Au Kristo alipokufa msalabani, je, hakufa kwa sababu ya dhambi zetu? Ni changamoto kwetu sote kufanya mabadiliko ya kweli ili tusiendelee kuupoteza muunganiko wetu na Kristo, aliye Bwana na Mungu wetu.
Na hii inawezekana kwa kupokea sakramenti za Kanisa, kwa namna ya pekee Sakramenti ya Kitubio katika mkutadha huu. Kwani, Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti hii, mwamini hupata msamaha na amani rohoni mwake, baada ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake. Lengo kuu la Sakramenti ya Kitubio ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; hapa ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo kujimamanisha na Kristo kwa kubaki kwake licha ya mahangaiko yetu ya kila leo. Pia, ni nafasi ya kujimamanua kutoka katika malimwengu yanayoendelea kutonesha madonda ya Kristo Bwana.