Sherehe Ya Ekaristi Takatifu

Tumsifu Yesu Kristo...

Kuishi katika jamii fulani ni sawa na kuandika simulizi. Na wakati unapowadia wa kuiacha jamii hiyo mhusika hutazamiwa kuondoka na kuacha simulizi linalosimulika kwa kupambwa na maneno yanayoonesha mafunzo na picha za mafanikio. Ni ukweli usiopingika kuwa Kristo alipoishi hapa duniani, maisha yake yalikuwa simulizi tosha, ndiyo maana Injili iliandikwa. Katika kuishi kwake alituachia simulizi linalosimulika kwa maneno na matendo yenye mafunzo kwa wafuasi wake na picha za mafanikio katika utume wake, kipekee kupokea mateso, kifo na ufufuko wake. Kati ya masimulizi yote juu ya Kristo, simulizi la Karamu ya Mwisho ni simulizi la namna yake, na la kipekee; linadhihirisha kwamba Kristo alituachia simulizi la kweli la upendo lililojidhihirisha katika maisha yetu. Ni simulizi ambalo kila mara linaposimuliwa, huamsha tena ndani yetu uwepo wa Kristo katika maisha. Kristo kabla ya kuondoka aliwaachia mitume wake Sakramenti ya Upendo, yaani Ekaristi Takatifu.

Katika tamaduni nyingi, mtoto anaposimuliwa hadithi nzuri na ya kuvutia hupenda kuisikia mara kwa mara akutanapo na aliyemsimulia. Mtoto humwambia, naomba unisimulie tena ile hadithi. Watoto hupenda daima kusema, nisimulie tena!! Inaweza kuwa siyo simulizi au hadithi, mfano mzuri ni ile hali ambapo mtoto mdogo ukimchukua na kumrusharusha, utasikia anasema, fanya tena! Fanya tena! Hili ndilo linajidhihirisha katika simulizi la Karamu ya Mwisho. Kila mara simulizi hili linaposimuliwa waamini hupenda kulisikiliza. Aidha, karamu ya mwisho inapotendwa na kufanywa hai katika adhimisho la Misa Takatifu, waamini humwambia Padre “afanye tena”, yaani aadhimishe Misa kila mara wakutanapo kanisani kuabudu. Ndiyo nafasi ya kuipokea na kuiadhimisha Ekaristi Takatifu iliyo chemchemi na kilele cha Maisha ya ukristo wetu. Bila Ekaristi Maisha yetu si kitu, ni sawa na kumtoa samaki majini, matokea yake ni kufa. Ndivyo ilivyo kwa wakatoliki wasioishi maisha ya kiekaristi.

Mtakatifu Augustino wa Hippo anasema, “Wewe Bwana umetuumba kwa ajili yako, na Roho zetu hazitatulia isipokuwa katika wewe”. Zitatulia ndani yako pekee. Hii ni kweli maana Wewe uliye “Ekaristi Takatifu ni Chemchemi ya Uzima wetu.” Unatuwezesha kukua katika upendo, unatufundisha kujitoa unakuwa kwetu Bwana, Mwalimu, Rafiki, Chakula, Mponyaji na Amani yetu.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK, n.1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. 

Leo tunatafakari Maandiko Matakatifu katika adhimisho la Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana Wetu Yesu Kristo; Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu waamini wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu; wanapata fursa ya kufanya maandamano ya Ekaristi na hatimaye, kuhitimishwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu imeendelea kufafanuliwa na Mababa wa Kanisa katika historia, maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kuna uhusiano mkubwa wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu.  Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inakuza imani kuhusu uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.

Waamini wanahimizwa kujenga utamaduni wa kukaa kimya mbele ya Kristo Yesu, ili aweze kuzungumza nao kutoka katika undani wa sakafu ya maisha na mioyo yao, tayari kuziba utupu, wasiwasi na hofu zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Hasa leo hivi tunapopambana na mmonyoko wa maadili katika jamii. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti, kwa kuonesha na kushuhudia uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na watu wake. Hii ni chemchemi ya maisha mapya yanayorutubishwa kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Kumbukumbu rasmi ya kuwekwa kwa Ekaristi ni siku ya Alhamisi Kuu. Lakini kama tunavyofahamu ilivyo nidhamu ya maadhimisho ya Juma Kuu hasa zile siku tatu kuu za Pasaka, hatuwezi kuadhimisha siku hiyo kwa shangwe kuu pamoja na maandamano ya kutangaza ukuu wa fumbo hili ambalo Kristo ameliachia Kanisa. Ndiyo maana ikatengwa siku nyingine baada ya sherehe za Pasaka kwa ajili ya adhimisho hili kubwa la Ekaristi pamoja na maandamano ya hadharani ili kukiri wazi na kutangaza ufahari wa imani yetu hii kubwa juu ya Ekaristi Takatifu.

Adhimisho hili ni mwaliko pia wa kuiishi Ekaristi. Kufufua ndani yetu kiu na hamu ya kushiriki mara nyingi iwezekanavyo Misa Takatifu hasa siku ya dominika. Ni mwaliko kufufua ndani yetu kiu ya kuipokea Ekaristi Takatifu tena kwa moyo safi na kushiriki ibada za kuabudu, zile za pamoja na zile za binafsi. Katika mazingira ambapo tunajikuta tumejifungia kupokea Ekaristi, adhimisho la leo linatupa mwaliko tusiridhike na hali hiyo wala kukata tamaa bali tuendelee bila kuchoka kutumia misaada yote kanisa linayoweka mbele yetu ili kuurudia muungano wetu ndiyo komunio na Kristo. Ni mwaliko wa kukuza imani yetu kuwa Yesu yupo daima na sisi hata mwisho wa nyakati.

Imani ya Kikristo katika Sakramenti ya Ekaristi hutupatia nafasi ya kumpokea Kristo aliye hai. Maandiko Matakatifu yanabainisha hili: Yesu akawaambia. Amin, amin, nawaambieni, msipoula mwili wa Mwana wa Mtu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuiynwa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamufufua siku ya mwisho” (Yn 6: 53-54). Hii lugha ya kisakramenti haikueleweka: tofauti ni kwamba chakula cha kawaida tulacho mwili wetu hukibadilisha. Ekaristi hutabadilisha na kutufanya mwili wa Kristo. Adhimisho la Ekaristi hutupeleka mbele zaidi, baada ya mageuzo twaitikia, tunatangaza kifo chako na kutukuza ufufuko wako mpaka utakapokuja. Mtakatifu Thomas wa Aquino katika antifona (O Sacrum Convivium-ya kuabudu Sakramenti Kuu) anaeleza Ekaristi kama Sikukuu takatifu ambayo Kristo anapokelewa, kumbukumbu ya mateso husherehekewa, roho zinajazwa na neema, nasi tunapata ahadi ya utukufu wa milele ijayo.

Mwisho, Ni uhalisia kwamba, yapo mazingira ya kusikitisha ambapo mwamini anajifungia kupokea Ekaristi kwa sababu mbalimbali za binafsi zinazomwingiza katika vikwazo. Katika hali hii anashindwa kuudhihirisha muungano wake wa kikomunio na kanisa na muungano wake wa kikomunio na Mungu. Ni tendo la kusikitisha kwa sababu pia linaliumiza kanisa kama mama wa wanawe wote na ndiyo maana kanisa haliachi kila wakati kujishughulisha na wanawe walio katika vikwazo ili warudi. Ni mwaliko pia kwa kila mwamini anayeishi katika vikwazo kutumia nafasi mbalimbali na milango ya kanisa iliyo wazi daima kujitafakari polepole, kuondoa vikwazo hivyo na hatua kwa hatua kuirudia komunyo Takatifu. Na huu pia unakuwa ni mwaliko kwa mwamini aliye ndani ya komunyo Takatifu kujilinda dhidi ya kuteleza na kuanguka kama anavyotukumbusha mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho kuwa “yeye anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Kor 10:12). “Tuipokee na kuiabudu Ekaristi Takatifu”

 
OMBI
Jumuika pamoja nami kufanikisha uchapaji wa vitabu vitatu vya imani na uinjilishaji vilivyoandikwa nami, na Mungu atakubariki sana. Unaweza kutuma mchango wako kwa njia ya M-Pesa kwenda namba +255754985663 (Emmanuel Kimambo Nhanwa) au bonyeza HAPA.

Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.

©2023 Ekinopia Studies