Tumsifu Yesu Kristo...
Maisha ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu. Kwa hivyo, uhai ni wa muhimu, wa thamani na ni kitu kitakatifu. Wanadamu siyo ‘waumbaji wa uhai wao’, bali ni mawakili na walinzi wa uhai huo. Uhai ni mali ya Mungu, na ndiye mwenye mamlaka juu ya uhai wa kila mwanadamu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatueleza ukweli huu kwamba: “Uzima wa kibinadamu ni kitu kitakatifu kwa sababu tangu mwanzo wake unahusiana na tendo la Mungu la uumbaji na daima unabaki na uhusiano wa peke yake na Muumba aliye peke yake kikomo chake. Mungu peke yake ndiye mwanzo wa uhai, tangu mwanzo wake hadi mwisho wake” (KKK, n. 2258).
Ni katika mantiki hiyo tunamuona Yosefu (Yusufu) mume wake Bikira Maria, Mama wa Mungu kama mdau na mtetezi wa uhai: kielelezo cha baba wa familia anayewajibika kama ilivyodhihirika katika kuishi kwake. Hii inadhihirishwa na maana ya jina lenyewe, Yosefu maana yake “Bwana aongoze” na Maandiko Matakatifu hayafumbii macho hili yanapoeleza, namna alivyokubali kuongozwa na Malaika wa Bwana. “Mumewe Yosefu akiwa mtu mwadilifu, hakupenda kumwaibisha hadharani. Basi, akanuia kumwacha kwa siri. Alipokuwa akifikiri hayo, tazama Malaika alimtokea katika ndoto, akasema, ‘Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpokea Maria kuwa mke wako, maana mimba yake ameipata kwa uwezo wa Roho Mtakatifu” (Mt 1:19-20).
Alinuia kumuacha kwa siri kwa sababu, kwa mila za kiyahudi binti kupata mimba kabla ya ndoa ilikuwa ni kosa ambalo liliadhibiwa kwa kupigwa mawe mpaka kufa. Hivyo, kwa kuwa Yosefu ni mtetezi wa uhai hakutaka wala kupenda jambo kama hilo limpate mpendwa wake. Anaamua kumuacha kwa siri kama Maandiko Matakatifu yalivyobainisha katika aya iliyotangulia. Hata hivyo, Malaika anampa maelekezo yakufuata na anatekeleza. Utetezi wa uhai: kielelezo cha baba wa familia anayewajibika haukuishia kwa Maria tu bali ulienda zaidi katika kumlinda na kumtunza mtoto Yesu. Maandiko Matakatifu yameeleza bayana juu ya hili, pale ambapo Mwinjili Mathayo anapoandika: “Amka umtwae mtoto mchanga na mama yake, ukimbilie Misri…kwa maana Herode ataka kumtafuta mtoto mchanga amwangamize. Alipoamka alimtwaa mtoto na mama yake usiku akaondoka kwenda Misri” (Mt 2:13b-14)
Ni katika mtazamo huo tunamuona Yosefu kama mtetezi na mlinda uhai, kielelezo cha baba wa familia anayewajibika. Ni kweli na uhalisia kwamba, mambo yote ambayo aliyatenda kwa ajili ya mtoto Yesu ilikuwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mtoto na Mama wanapata salama ya roho na mwili katika maisha yao. Hii ilimvuta zaidi awe mtu wa haki, akiwa anajua kwamba Neno la Mungu limeweka wazi adhabu ya kila atakayesababisha uhai kupotea. Mwandishi wa Kitabu cha Mwanzo ana haya yakusema: “Hakika damu ya uhai wenu nitadai. Nitadai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitadai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake. Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimwumba mwanadamu” (Mwa 9:5-6).
Na Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaenda mbali zaidi kuelezea kuwa uhai wa mtu lazima utunzwe tangu kutungwa kwa mimba, “Kwa kuwa toka nukta ya kutungwa mimba lazima itendewe kama nafsi, kiini tete lazima kitetewe katika utimilifu wake, kitunzwe, kiponywe, kadiri inavyowezekana, kama mwanadamu yeyote” (KKK, n. 2274). Yote haya Mtakatifu Yosefu aliyatekeleza kwa nafasi yake kama Baba Mlishi wa Bwana wetu Yesu Kristo, akiwaonesha akina baba wote mfano wa kufuata na kuiga. Ni mfano wa baba mwema anayejali na kuwajibika.
Ni kiu na shauku ya wengi kuwaona akina baba wanakuwa akina Yosefu kwa watoto wao na wenzi wao wa ndoa katika kutetea na kulinda uhai wao, yaani kuwa kielelezo cha baba wa familia anayewajibika. Upendo ndiyo msingi wa yote haya. Kama hauna upendo, huwezi ukatolea nguvu zako kwa ajili ya watu wengine. Yosefu ana moyo wa ajabu ambao akina baba wa siku hizi wanadaiwa kuwa nao, hasa kutunza na kulinda uhai. Yoseph alizingatia kwa imani kubwa maelekezo aliyopewa katika ndoto na malaika hata akarudi kwa Bikira Maria kutimiza yale aliyoambiwa na malaika katika ndoto kadiri ya mapenzi ya Mungu, yote haya yanafumbatwa katika maana ya jina Yosefu, yaani “Bwana aongoze” kweli aliiongoza familia akiwa baba mwaminifu na wa kujali mahitaji ya familia yake (cf., Mt 1:19-25).
Licha ya kwamba, Herode alikuwa anaitafuta roho ya mtoto kufa lakini bado Yosefu alikuwa makini sana akihakikisha usalama wa mtoto pamoja na mama yake (cf., Mt 2:20-23). Ni mwaliko wa kila baba katika familia siku hizi kujiuliza kwamba, ni mara ngapi kumetokea matatizo, shida, changamoto, mahagaiko ya maisha na yanayofanana na hayo nyumbani, ukakimbia mwenyewe ukimuacha mama na mtoto/watoto ili waangamizwe na Herode wa siku hizi ambaye ni njaa, magonjwa, mmomonyoko wa maadili, utoaji wa mimba, matumizi ya vithibiti mimba? Umekimbia peke yako umemuacha mama na mtoto/watoto. Wababa mmetelekeza familia zenu, hii siyo nzuri, mmempa nafasi Herode atawale familia zenu.
Ni mwaliko kwa kila Baba kumtazama Yosefu, yeye alimtwaa mtoto na mama yake wakakimbilia Misri, kwa akina baba wa siku hizi walio wengi hali imekuwa tofauti kabisa. Wao wamekuwa wakitwaa michepuko (nyumba ndogo) na kukimbilia baa, katika kumbi za starehe, fukwe za bahari kwenda kupata upepo mwanana huku mama na mtoto/watoto wakihangaika na kutangatanga katika dunia hii na nyumba za kulala wageni wamegeuza makazi yao ya kudumu. Kwanini akina baba tumethamini sana michepuko, nyumba ndogo, marafiki zetu na kumsahau mama na mtoto/watoto? Wahenga wanatuambia, “Mchepuko siyo dili, baki njia kuu”, maana yake tubaki na kutulia katika familia zetu. Kwanini tunahangaikia ambavyo si vya kwetu? Kwanini tunajipa majukumu na wajibu ambao sio wetu? Kuhudumia michepuko!! Siyo dili, tuwahudumie wale tuliowaahidi kuwavumilia katika taabu na raha, afya na magonjwa kama tulivyoahidi siku ya kufunga ndoa zetu. Je, tunayakumbuka hayo?
Akina baba tunakumbushwa tuwe kama Yosefu, kumbeba mama na mtoto tukimbie kwa pamoja hasa kipindi ambapo katika jamii zetu tunakumbana na matatizo. Wakati huu kuna janga la Korona, baadhi ya akina baba wameacha familia zao na kuzikimbia kwa sababu ya korona. Huu ni uuaji kabisa, kwani mahitaji msingi ya familia hayatapatikani kwa sababu nguzo moja ya familia haipo tena. Mama ameachiwa majukumu yote, hii si sawa katika maisha na malezi ya watoto. Katekismu ya Kanisa Katoliki inaendelea kutujuza na kutupa mwongozo kwamba “Wazazi ndio wa kwanza walio na wajibu wa malezi ya watoto wao. Wanashuhudia wajibu huo kwa kujenga familia ambamo utu wema, msamaha, heshima, uaminifu na huduma isiyojitafutia faida huwa ndio kanuni. Nyumbani ni mahali panapofaa kwa mafunzo ya fadhila. Ni mahali pa kujifunza kujikatalia, hukumu sahihi, kujitawala-masharti ya kwanza ya uhuru wote wa kweli. …wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwapa watoto wao mifano mizuri” (KKK, n.2223). Akina baba tumuige Yosefu katika kutimiza wajibu zetu katika familia, jamii na kanisa kwa ujumla. Baba Mtakatifu Fansisko katika Barua yake ya Kitume “Patris Corde” amemdadavua Mtakatifu Yosefu kwa kumpa sifa kede wa kede kama “Baba mpendwa, Baba mpole, na mwenye upendo, baba mtiifu na mnyenyekevu; baba ambaye ana ujasiri wa ubunifu na Baba anayefanya kazi kwa kujituma akiwa ndani ya vivuli” (Patris Corde, nn. 1-7). Sifa hizi ndizo akina Baba wa leo wanadaiwa kuwa nazo. Zinatakiwa ziwe sehemu ya maisha yao, watoto na wenzi wa maisha yao wazione sifa njema hizi ambazo Baba Mtakatifu katika kutafakari kwake ameziona ndani ya Mtakatifu Yosefu. Tunaweza kuwaonesha wapendwa wetu sifa njema hizi kwa kutimiza wajibu na majukumu yetu.
Labda tujikumbushe kidogo kuhusu wajibu na majukumu ya Baba mwema katika familia. Hili limewekwa bayana na Pd. Eugene Kawau katika kitabu chake, chenye anwani “Uwajibikaji Sahihi: Dawa kwa Changamoto katika familia na Jamii”, akitaja baadhi ya wajibu za Baba mwema anaandika: “Baba ni kiongozi wa familia yake, humpenda mkewe na watoto. Anapaswa kumpa mkewe heshima kama binadamu kwani mke wake sio mtumwa wake. Pia, baba ni mlishi na mlinzi wa familia yake, anawapatia mke na watoto mahitaji ya lazima kulingana na hali yake ya maisha. Aidha, baba anapaswa kuwa mwaminifu katika ndoa yake, sio mtu wa kuwaka tamaa ovyo; na anatumia mali kwa manufaa ya wote, kwa kutokubagua yeyote katika familia. Sanjari na hilo ana wajibu wa kuwalea watoto wake akishirikiana na mke wake. Na anatakiwa kuwa na uhusiano mwema na majirani, ndugu, jamaa na marafiki, kwa kushirikiana nao katika hali zote, huzuni na furaha. Kwa ujumla, Baba anawajibu wa kuwa raia mwema na mwenye bidii ya kufanya kazi; mcha Mungu na atimize wajibu wake kwa Mungu na kwa jamii anamoishi”. Haya aliyatimiza Mtakatifu Yosefu, “amekuwa mfano mzuri sana wa uwajibikaji katika familia. Akina baba wanapaswa kuwajibika ipasavyo kwa ajili ya kuzitunza familia zao” ndivyo Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), linavyotutanabaisha katika ujumbe wake wa “Maadhimisho ya mwaka wa Mtakatifu Yosefu (cf., uk 6-8). Ni ukweli na uhalisia kwamba, sasa ni zamu ya akina baba wa leo nao kuyatimiza haya na mengine mengi yanayotuelekeza katika utakatifu.
Daima maneno ya sala kwa Mtakatifu Yosefu yabaki katika mioyo na roho zetu tukisali kila mara kwamba, “Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo. Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufuate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele”. Kama familia lazima tusali kwa ajili ya akina baba wote kupata baraka na neema inayofumbatwa katika sala hii. Akina baba kwa pamoja tunaweza. Maana BABA NI NGUZO IMARA YA FAMILIA NA KANISA.