Tumsifu Yesu Kristo...
Askofu ndiye Katekista mkuu wa Jimbo |
Chozi, Chozi, Chozi! Chozi ndiyo nini? Chozi kasababisha nani? Na ni nani huyo anayelia? Nani atakayefuta chozi hilo? Chozi ni kiwakilishi cha maneno ambayo moyo hauwezi kuongea. Na ukiona maharage yametokota, ujue kuna mkaa umeteketea. Hahahaaa! Ama kweli, usilolijua ni kama usiku wa giza. Na mmoja wa wasomi aliwahi kusema, “Ujinga wa mguu hudhani kuwa ni kazi ya mkono kutoa mwiba pindi uchomwapo. Ni ujinga wa kinywa pia kufikiri kwamba ni kazi ya mkono kupeleka chakula mdomoni”. Hii ndiyo hali halisi ya maisha yetu ya kila leo. Maneno ya Isamil Haniyeh (+1963) yanatanabaisha ukweli huo kuwa “Baadhi ya watu hudhani ukweli unaweza kufichwa kwa kuuzuia kidogo au kuupamba. Lakini kadri muda unavyokwenda, kilicho cha kweli hudhihirishwa, na uongo hutoweka tu wenyewe”. Tunapotafakari juu ya katekista, picha gani inakujia ndugu msomaji kuhusu maisha yake? Leo hii ukiambiwa uchore picha ya katekista, unayemfahamu, ungechora picha gani? Je, ungechora picha ya katekista mwenye sura ya furaha, amani, au tabasamu? Au ungechora picha ya katekista aliyechoka, mnyonge, na amekata tamaa? Hali halisi ya hawa watumishi katika kanisa ikoje? Uhakika wa maisha baada ya utume wa katekista ukoje?
Maana ya Neno Katekista
Katekista ni muumini au mwamini aliyeitwa na Mungu, akateuliwa na Kanisa, kulingana na mahitaji ya Kanisa la mahali, ili afanye Kristo ajulikane, asadikiwe, apendwe na afuatwe na wale wasiomjua bado na hata na waumini wenyewe hasa katika hatua za msingi na za awali za ufuasi wa Kristo. Katekista ni mtangulizi au mfunguaji wa njia katika Kanisa na msingi mkuu katika imani ya Kanisa, yeye ni mtangulizi wa Padre, Askofu na wengine wenye kushika mamlaka katika Kanisa. Hujifunza Katekisimu kwa moyo na nguvu zote apate kuwafundisha wengine mafundisho hayo msingi ya Kanisa kwa uaminifu na juhudi ili wapate kuijua vema imani ya Kikatoliki. Baba Mtakatifu Fransisko katika Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 22/10/2019 alisema waziwazi kuwa:
“Makatekista ni kati ya mihimili ya uinjilishaji ndani ya Kanisa kwani jukumu lao kubwa ni kuwaandaa Wakatekumeni ili waweze kupokea vyema Sakramenti za Kanisa. Makatekista wengi wamekuwa ni mfano bora na mwanga kwa jumuiya zinazowazunguka. Kanisa linaendelea kuwashukuru Makatekista kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa, sasa wawezeshwe!”
![]() |
Baba Mtakatifu ni Katekista wa Makatekista |
Vilevile, Sheria Mkusanyo Kanuni kwa namna ya pekee inaweka wazi kuwa:
“Makatekista watumiwe katika kufanya kazi ya kimissionari; makatekista ni wale waamini Wakristo walei ambao wamefunzwa ipasavyo, ambao wanaonekana kuwa mifano kwa namna ya maisha yao ya Kikristo, na ambao wanajitoa wenyewe kufafanua mafundisho ya Injili na kusimamia shughuli za kiliturjia na kazi za upendo chini ya uongozi wa mmissionari (Rej., Kan. 785. § 1).
Hivyo Kanisa linapaswa kumthamini Katekista, ambaye ni msingi wa Kristo na Katekista ana kazi kubwa ya kuwapa mafundisho msingi ya Kanisa waumini, mfano mafundisho juu ya Masakramenti, kama vile Ubatizo, Kipaimara, Komunyo ya Kwanza (Ekaristi Takatifu), Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, ndoa na Upadre. Makatekista waume kwa wake, hustahili pongezi na sifa kweli kwani kazi ya kimisionari kati ya mataifa imeendelezwa nao sana. Jitihada zao kubwa zikiongozwa na roho ya kitume, zimesaidia kwa namna ya pekee na ya lazima katika uenezaji wa imani na wa Kanisa (Rej. Hati ya Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Ad Gentes, Kazi za Kimisioni za Kanisa, n.17)
Tunaona bila kupitia kwa Katekista (Yohane Mbatizaji) Yesu asingeweza kutambuliwa kwa haraka na wafuasi wa kwanza, mara tu baada ya kuambiwa, tazama mwanakondoo wa Mungu, wote wakamfuata na Kristo anawakaribisha. Katekista pia katika nyakati zetu hizi anafanya kazi ya Yohane Mbatizaji, anawaandaa watu kwa ajili ya kupokea Sakramenti na kujifungamanisha zaidi na maisha ya kumfuata Kristo. Huyu Katekista ndiye anayewaonesha wakatekumeni na waumini kwa Padre, anawatambulisha mbele yake ili awapatie huduma katika Kanisa. Hivyo, Katekista ni kiungo muhimu sana katika Kanisa.
Hali halisi ya Katekista
Twaweza kuendelea kujiuliza, nini thamani ya Katekista katika maisha ya Kanisa? Katekista ana thamani kubwa sana katika Kanisa kama ilivyoainishwa hapo awali. Pamoja na hayo, Katekista hufundisha mafundisho ya wakatekumeni, Komunyo ya Kwanza, Kipaimara na sakramenti nyingine katika Kanisa. Pia, hutayarisha chakula cha Kiroho kwa siku za Dominika, huwalisha waamini Neno la Mungu maeneo ambapo makuhani hawawezi kufika siku za Dominika. Husikiliza shida za waumini na kuzipeleka kwa Padre, mfano wanandoa wanapopata shida au pindi wanapohitaji mashauri ya Kiroho, taarifa juu ya wagonjwa, mazishi na mengine mengi yahusuyo utume wao, kama watangulizi wa Mapadre. Hutoa semina mbalimbali katika Kanisa, mfano kwenye vyama vya kitume kama Fatima, Viwawa, Wawata, Uwaka na vyama vingine vinavyopatikana katika mazingira yao ya utume. Aidha, Katekista huwaandaa waumini kwa Ibada ya Misa Takatifu, majitoleo, na kuhamasisha ushiriki hai wa kulijenga Kanisa la Kristo. Yote haya huyafanya katika muktadha wa Yohane Mbatizaji, akimwonyesha Kristo kwa waumini kwa kumtambulisha Padre. Aidha, kati ya waamini wengi wanaokuwa wainjilishaji, makatekista wamechukua nafasi ya heshima na ya pekee katika hili, hasa katika kuhakikisha lengo nuiwa la Mama Kanisa linatimia ndani ya maisha ya watu; kiroho na kimwili (Rej. Pope John Paul II, Enclical Letter, “Redemptoris Missio”, The Mission of the Church, (December 7, 1990), n.73-74)
Licha ya Katekista kufanya hayo yote, tujiulize, ni changamoto gani Katekista hukumbana nazo katika kutekeleza utume wake? Je, kudharauliwa, kunyanyaswa, kugombezwa, kwa ujumla lugha isiyo shirikishi toka kwa anaowahudumia ama wale anaowawakilisha? Ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya wanaohudumiwa na katekista ambao hawatambui umuhimu wake katika Kanisa. Hali hii siyo nzuri na inasikitisha mno pale ambapo Kanisa kupitia waamini wake linashindwa kuwatambua wahudumu hawa kuwa ni nguzo imara katika Kanisa na zaidi sana kutowatambua kama msingi wa imani, kwa kuwa waamini walio wengi wamepitia mikononi mwao.
Mapadre ni walimu wa Dini, yaani ni Makatekista. |
Baba Mtakatifu Fransisko ameendelea kusisitiza kuwa:
“Makatekista wanapaswa kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kufundisha kwa umakini mkubwa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala, ili waamini waweze kupata neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Makatekista wanao wajibu wa kuwasaidia waamini kumwilisha imani yao katika uhalisia wa maisha kwa njia ya ushuhuda unaoleta mvuto na mguso. Ni watu wanaopaswa kuwasaidia waamini kujenga na kuimarisha moyo wa sala na ibada kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao”.
Hili ni changamoto, na halitiliwi mkazo, tuungane na Baba Mtakatifu kuwathamini na kuwajali walimu wetu wa dini, makatekista.
Makatekista wanaoneshwa upendo pindi wanapotimiza majukumu katika matukio mbalimbali katika Kanisa, mfano siku za Ibada kama vile Jumapili, na siku nyingine kama tegemeza jimbo, kuwapongeza Mapadre, mafundisho na kazi nyingine za kiuchungaji. Ni ukweli usiopingika kuwa, mara nyingi hakuna Katekista anayetambuliwa mara tu baada ya kazi hizo kumalizika. Wanaonekana si kitu, hawana thamani na umaana wao hupotea na kusubiriwa kwenye matukio mengine. Hii si sawa kwa hawa watumishi, kwani inawaumiza sana na pengine kukosa ladha ya maisha ya yule wanayemfundisha kwa watu, yaani Kristo Bwana. Kwa hali kama hiyo, msingi wa Kanisa upo wapi? Je, kwa watumishi wa Kiroho ambao wao huja kuoneshwa kundi na kutoa masakramenti? Je, vipi kuhusu waamini ambao huaandaliwa na watumuishi hawa?
Mtaguso wa II wa Vatikano umeweka bayana kuwa;
“katika nyakati zetu, ambapo makasisi ni wachache sana wa kuhubiri Injili kwa watu wengi hivi na kuzitenda kazi za kitume, wajibu wa makatekista ni wa maana kubwa sana. Kwa hiyo malezi yao lazima yawe kamili na tena maendeleleo ya ustaarabu, ili waweze kutimiza shughuli zao kama wasaidizi wa mapadre vema iwezekanavyo, hata ikiwa wajibu wao umeongezewa na mizigo mipya” (Rej. Ad Gentes, n.17)
Licha ya kufanya kazi hizo zote, bado kuna kosa kubwa linaendelea kufanywa na baadhi ya wanaohudumiwa, kama vile kuwanyanyasa, kuwadharirisha na kuwatukana hawa walimu wa dini, kitu kinachowakatisha tamaa walio wengi. Hawa wanapokosa kuwatambua makatekista hata jamii inayowazunguka inashindwa kuwatambua na kuwapa heshima wanayostahili. Baadhi ya makatekista nilioshirikishana nao juu ya suala hili nao wakatoa ya moyoni wakisema;
“Katika sikukuu za kijimbo wanaotambulika zaidi ni baadhi tu ya viongozi lakini katika mazingira yaliyo mengi Katekista husahaulika na hatambuliki wala kukumbukwa. Na ikitokea Katekista amekwenda kwenye sikukuu ya kijimbo mara nyingi huduma yake hupitia dirishani siyo mlangoni. Je, viongozi na Makatekista si wote waamini wa jimbo? Kwa nini hawaoni thamani yetu hata baada ya utume? Je, ni nani atakayefuta chozi letu? Ni nani atakayesikiliza masikitiko yetu? Yaweza kuwa hawatambui kuwa sisi ni watumishi katika shamba la Bwana”.
Hata hivyo, hawakuishia kusema hivyo tu, waliendelea kujifunua zaidi waliposema:
“Mara nyingi makatekista wamesahauliwa malaloni au makaburini baada ya kutoa huduma za kuwazika wakristo, licha ya kutafutwa kwa bidii na kupelekwa kwa magari ya kifahari. Lakini cha ajabu, kisha kutoa huduma huonekana kuwa hana thamani, atajua namna ya kurudi kwake. Siyo hivyo tu, pia husahauliwa na kuachwa nje ya kumbi mbalimbali za sherehe za ndoa, Komunyo, Kipaimara na nyinginezo, licha ya wao kuwa ndiyo watayarishaji wa hizo sakramenti. Mwisho wao ni chombo cha kuzolea taka, thamani huisha na kurejea tena pindi shida ikijitokeza. Wakasema hayo ni baadhi tu, kuna mengi zaidi tunaweza kuongea yanayotusibu”
Tukimtazama Kristo, tunaona kuwa alikuwa karibu na mitume wake, mahali alipoingia nao pia waliingia, alikula pamoja nao, na alifanya kazi nao. Alitambua mchango wao katika utume, na aliwaaminisha mambo makubwa. Hivyo, tunatakiwa kutambua kuwa tunatakiwa kulijenga Kanisa pamoja tukiweka msingi imara katika fadhila za Kimungu yaani, imani, Matumaini na Mapendo. Pamoja na hayo, pia umoja na ushirikiano ni nguzo msingi wa kulisimamisha Kanisa. Hivi ndivyo alivyoandika Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, “Africae Munus” yaani “Dhamana ya Afrika”;
“Makatekista wengi wamekuwa ni mfano bora na mwanga kwa jumuiya zinazowazunguka. Kanisa linaendelea kuwashukuru Makatekista kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hili ni kundi ambalo linahitaji kupatiwa majiundo ya kina na endelevu, ili liweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa. Lakini, Makatekista wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa, kwani mfanyakazi mwaminifu katika shamba la Bwana anastahili kupata ujira wake. Makatekista wanaendelea kuchangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa ushuhuda wa imani tendaji kwa njia ya maisha na matendo yao adili, kwa kuwajali wote bila ubaguzi. Ni mwaliko wa kumwilisha Injili na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, ili kutoa Katekesi safi na ya kina kwa watu wao; wakiwaongoza kwa moyo wa Sala na Ibada. Kama sehemu ya viongozi wa Kanisa, Makatekista wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ujasiri, bidii, ari na moyo mkuu, ili kuchangia utakatifu wa maisha ya familia ya Mungu inayowajibika”
Licha ya kutokuwathamini makatekista, imekuwa vigumu pia kutoa fursa ya wao kwenda kupata elimu dini zaidi hali ambayo inapelekea kupata waamini ambao hawajaiva kiimani. Kwa maana, Katekista ndiye anayesimika msingi wa Mafundisho ya awali ya imani ndani ya Kanisa. Kama mkufunzi anauelewa mfinyu, vipi wale ambao anawaanda? Je, ni nani atakayefuta kilio chao cha elimu dini? Sheria ya Kanisa inasisitiza na kuweka mkazo juu ya suala hili;
“Walei wanaojitoa kwa namna thabiti au kwa muda katika huduma maalum ya Kanisa hawana budi kupata matayarisho yanayofaa ambayo yanatakiwa katika kutimiza wajibu zao inavyotakiwa na kuzifanya kwa uaminifu, bidii na uangalifu. Pamoja na kuzingatia Kan. 230 aya ya 1, wana haki ya ujira unaostahili kulingana na hali zao. Kwa ujira huu waweze kukidhi vizuri mahitaji yao na yale ya familia zao yakizingatiwa pia maelekezo ya sheria za nchi, kadhalika wana haki ya kupatiwa pensheni, hifadhi ya jamii na huduma za afya” (Rej. Kan. 231).
Hii itawasaidia kujiunda na kuwa walimu hodari wa dini.
Hata hivyo, hatuwezi kukataa kuwa kuna baadhi ya mapadre na waamini walei wanaowathamini makatekista wao, wanawajari na kuwatunza. Hawa tunawapongeza kwa kuakisi mtindo na mfumo wa Kristo kwa mitume na wafuasi wake. Tunawaombea kwa Mungu waendelee kuienzi na kuikuza kazi ya hawa walimu wa dini.
Ikumbukwe pia, kuna makatekista ambao sio waaminifu, wanatumia vibaya wajibu waliokabidhiwa katika kanisa. Wanapokea rushwa kwa waamini ili waweze kuwapatia huduma au kufunika na kufanikisha kile ambacho hakifai. Mfano, siku hizi ili mtoto wa komunyo ya kwanza au Kipaimara apate sakramenti moja ya hizo, lazima afanye mtihani na afaulu. Baadhi ya wazazi wanahonga ili watoto wao wafaulu, na makatekista nao wanapokea rushwa tu. Kitu hiki ni kibaya sana na kinapoteza thamani ya kile wanachoenda kukipokea. Ndiyo, maana katekesi ya siku hizi imekuwa kufaulu mitihani, na siyo kuifanya katekesi iwe sehemu ya maisha ya mkatekumeni au mtoto wa mafundisho. Makatekista na wazazi wa mtindo huu muache mchezo huu. Makatekista pendeni, jalini utume wenu na msipeperushwe na malimwengu, bali lengo, kiu na shauku yenu iwe katika kuyatimiza yale mliyopewa kutimiza na kjishikamanisha na yale ya mbinguni. Fundisheni imani na dini ya Kristo na si vinginevyo. Ili muamini apate kuamini, na kuwa tayari kumwaga damu kwa ajili ya Kristo; yaani, Kufa nife, lakini siyo kutenda dhambi na yanayofanana nayo. Hii ndiyo katekesi, kuikiri na kuiishi imani.
Makatekista watunze heshima na wadhifa waliopewa na Mama Kanisa kwa kuwa kweli chumvi na mwanga katika giza la ulimwengu wetu wa sasa. Masuala kama unywaji wa pombe uliokidhiri, uongo, uchonganishi, na mambo mengine yahusuyo maadili. Haya yote na ya mlengo huo yanapoteza imani na heshima kwao kama walimu wa dini. Kwa ufupi, ni kujiepusha na nafasi za hayo yote yanayowakosesha hadhi na haiba yao kama makateksta.
Mwaliko kwa waamini wote
Mwaliko wangu kwa Mababa Mapadre na waamini walei wote ni huu, kwanza kuenzi utume wa Katekista katika Kanisa, kwa kuwa yeye ni chombo imara cha kufundishia imani katika hatua za mwanzo. Maana, hakuna mtu mwingine atakayefuta chozi la Katekista tofauti na waamini walei aliokabidhiwa nao, kundi lake alilokabidhiwa kuliongoza katika kigango, kwa maongozi ya mapadre anaofanya nao kazi kwa ukaribu zaidi. Kwa nafasi ya kwanza, waamini wanayo nafasi ya kumfuta katekista chozi. Swali la msingi ni, je, waamini hawa wanafahamu wajibu wao huo kwa kiongozi wao? Kama ni ndiyo, wautimize; kama hapana, wafundishwe ili wajue na watimize wajibu wao.
Pili, mapadre na waamini kwa pamoja wawatambue makatekista kuwa ni msingi wa Kanisa katika kuandaa miito mbalimbali katika Kanisa, lakini zaidi wito wa kwanza wa kuwa Wakristo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa bila Katekista, Maaskofu, Mapadre, Watawa na wanandoa hawatakuwepo maana wote wametoka katika mikono ya Makatekista, wamepata mafundisho ya awali kutoka kwa hawa.
![]() |
Makatekista ni wasaidizi wa Karibu wa Padre |
Tatu, Baraza la walei linaalikwa na kushauriwa kuwasikiliza na kuwaheshimu viongozi hawa na siyo kuwapuuza na kuwawekea maneno na mambo ambayo siyo yao. Hivyo, wanaalikwa kuuona mwanga wa Kristo kwa hawa watumishi, wawatendee inavyotakiwa na si vinginevyo. Maana, mahali pengi kumekuwa na mvutano kati ya pande hizi mbili. Ni wito wa kufanya utume pamoja kama jumuiya ya mwanzo kuhakikisha imani inakua na waamini wanaiishi kwa furaha licha ya mahangaiko ya Maisha.
Nne, wito ni sadaka, lazima makatekista watambue hilo. Chanzo cha kudharauliwa kwao kinaweza kuwa kukosa nguvu ya maadili, hali duni ya maisha elimu ndogo kwa upana wake na yafananyo na hayo. Inatakiwa watambue kuwa chozi la kweli, litafutwa na yule aliyewaita kumtumikia, aidha hapa duniani ama mbinguni. Hapa, duniani kupitia kundi ambalo amekabidhiwa, yaani waamini. Hata hivyo, ni mwito kwa makatekista wote kutimiza wajibu na majukumu yao katika kanisa bila ya kuchengesha kitu chochote. Maana, kona kona katika utumishi zinaweza zikawaondolea uaminifu na hivi kudharauliwa, kusemwa na hata kukatishwa tamaa katika wajibu wao. Usemi wenu uwe ndiyo, ndiyo; siyo, siyo yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu (Mt 5:37). Matendo yenu yawe kielelezo cha kuwavuta waamini kwa Kristo, na kupitia hilo wawakirimu kama jinsi walivyofanya kwa Kristo Mwenyewe na mitume wake; kwa hali hiyo watawafuta machozi yenu. Baba wa taifa Mwl. Julius K. Nyerere alisema “inawezekana ukitimiza wajibu wako”.
Tufanye nini sasa?
Makatekista wanapaswa kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kufundisha kwa umakini mkubwa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala, ili waamini waweze kupata neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho yake ya kila siku. Hivyo, kamati tendaji ya parokia au jimbo watengeneze mfumo ambao utawafanya makatekista hawa wapate mahitaji yao ya kila siku katika maisha na hivi waweze kuwa huru katika kulitumikia kanisa. Na walimu wetu wa dini watafanya kazi bila manung’uniko bali kwa furaha, amani na zaidi kwa upendo. Na hivi, kazi ya ukombozi itaendelea, Mungu atatukuzwa na mwanadamu atatakatifuzwa.
Hitimisho
Mwisho, katekista ndiye mwanga wa mwanga wa mwanzo kumulika mbele katika imani. Tuwaheshimu, tuwaenzi, tuwasaidie na tuwajali katika karama na kazi wanazozifanya; ili waone furaha katika kumtumikia Mungu katika hali zote na katika uzee wao waenziwe. Pia, mapadre na waamini tunaalikwa kuwafuta machozi hawa watumishi kwa kuwapatia iliyo haki yao, unyenyekevu wao isiwe njia ya kuwanyanyasa, kuwatukana na kuwadharirisha bali wawaelekeze na kuwafundisha kwa upendo ili kazi ya Kristo ambayo sote tumeitiwa tuweze kuitimiza kila mmoja kulingana na nafasi yake katika Kanisa la Kristo. Kwa maana “hakuna tena Myahudi wala Mgiriki, mtumwa wala mtu huru, mwanaume wala mwanamke, kwa maana ninyi nyote mmekuwa katika Kristo Yesu. Lakini kama ninyi ni wa Kristo, basi mmekuwa wana wa Abrahamu na warithi wa ahadi” (Gal 3:28-29). Mungu atubariki sote.
REJEA
BIBLIA YA KIAFRIKA, Titu Amigu et Alii (Trs & Eds), Nairobi: Pauline Publications Africa, 2010.
Dodoso na Mahojiano na Baadhi ya Makatekista.
HATI ZA MTAGUSO MKUU WA II, Ndanda Mission Press, Mpanda (Iringa) 2001.
Katekisimu Ndogo ya Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Songea, Songea: Peramiho Printing Press, 1998.
Mahubiri ya Papa Fransisko, Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019: Utume wa Makatekista: https://www.vaticannews.va/sw/pope/news/2019-10/siku-kimisionari-ulimwenguni-2019-dhamana-utume-makatekista.html, (Imepakuliwa Tarehe 21 Julai 2023).
Mazungumzo na mahojianao na baadhi ya Makatekista toka parokia mbalimbali ndani ya Jimbo Katoliki Shinyanga.
Pope Benedict XVI, Post-Synodal Apostolic Exhortation: “Africae Munus”, 19 November, 2011.
Pope John Paul II, Enclical Letter: “Redemptoris Missio”, The Mission of the Church, December 7, 1990.