Tulisaidiwa Na Watu Ambao Siyo Ndugu

TUMSIFU YESU KRISTO...
 
Nawashukuru Wazazi wangu kwa Malezi yao Bora
Wahenga wa fasihi ya Kiswahili husema, “Usilolijua ni kama usiku wa giza”. Je, ulishawahi kuwafikiria watu waliokusaidia, lakini wao kwa wao siyo ndugu? Je, hawa ni akina nani? Je, unatambua umuhimu wao? Je, unawathamini na kuwajali? Hawa ni watu waliotusaidia pasipokujali maslahi yao. Wakiongonzwa na dhamira ya upendo walitumia yote waliyonayo kwa ajili yetu. Hapa ndipo msemo wa walimwengu hutimia, “Tenda wema nenda zako”.

Hiki ndicho hawa ambao siyo ndugu walitufanyia sisi tukawa ndugu, wamekifanya, wanakifanya na wataendelea kukifanya mpaka tutakapooneka wa kufaa. Ni ukweli kwamba tunaishi katika ulimwengu ambao umejaa mahangaiko mengi. Ni ulimwengu ambao haujali utu wa watu, hasa waliokuwa dira na mwongozo wa maisha yao. Wamesahaurika!

Nilipokuwa nasoma Sekondari, mwalimu wa hesabu alitufundisha mada inayoitwa “Function”, na moja ya kipengele alichokieleza nakumbuka alisema: f(x):x=all children. Kwa maana ya haraka haraka tunaweza sema, ‘fakisheni’ ya f(x):x kwamba x inawakilisha Watoto wote. Kwahiyo, kila mwanadamu ni mtoto. Baba na mama ni Watoto wa Babu na Bibi zetu nakuendelea. Huu ndiyo ukweli kwamba, “mtoto ni mtu mzima anayekua, na mtu mzima ni mtoto aliyekua”[1]. Hivyo, wajibu wa hawa wasio ndugu ni kumwandaa huyu mtoto (ambaye ni mimi, yule au wewe) kuwa mtu mzima hapo muda wake utakapofika (Kanoni n.1055). Huu ndiyo msaada wa kwanza kwetu sisi watoto tulioupata toka kwa hawa wasio ndugu, kutujenga na kutuandaa kuwa watu wa kufaa katika jamii.

Hawa ambao si ndugu ni akina nani? Hawa ambao wao sio ndugu ni wazazi wetu, ni ukweli kwamba Baba na Mama hawajawahi, hawakuwa na hawatakuja kuwa ndugu na ndiyo maana wakaoana. Kisheria, ndoa si halali kati ya wale wanaohusiana undugudamu katika nyuzi zote za mstari wa wima, haijalishi wa kupanda au wa kushuka, wa kisheria au wa kiasili (Kanoni n. 1091-1092). 
 
Furaha ya Kuwa katika Familia
Hebu tujiulize, maisha yangekuwaje kama ingekuwa kila mmoja wetu angejizaa yeye mwenyewe duniani? Maisha yasingekuwa na ladha. Ni kweli kwamba, maisha bila Baba na Mama, hayafai. Yaani, wewe peke yako tu! Bila shaka kusingekuwa na Maisha, na kama yangekuwepo, yasingekuwa ya mfumo huu tulio nao. Kwa nini? Kwa sababu wanadamu tumeumbwa kutegemeana. Kwa asili tumeumbwa kuongezeana thamani. Hii ni kanuni ya asili ya uumbaji wa Mungu (Rej., Mwz 1). Je! tunaweza kuwakumbuka watu ambao waliwahi kufanya mambo mema katika maisha yetu na hatuwezi kuwasahau? Tujaribu kuwakumbuka hata baadhi yao. Bila shaka hao ni watu walioyaongezea thamani maisha yetu, ndiyo maana hatuwezi kuwasahau. Na raisi wa Marekani John F. Kennedy anakazia bila kumumunya maneno anasema, "Lazima tupate muda wa kusimama na kuwashukuru watu (wazazi) (walioleta au) wanaoleta mabadiliko katika maisha yetu". Kwa sababu hao walikuwa, wamekuwa na wataendelea kuwa baraka kwetu. Hawa si wengine bali ni wazazi wetu.

Hawa ndiyo watu waliotusaidia katika maisha ili hali wao siyo ndugu, ni upendo mkubwa na wa ajabu. Huu ni ukweli unaopatikana katika tamaduni nyingi za kiafrika, kwamba mimi au wewe huwezi kumuoa dada au kuolewa na kaka yako. Kwa nini? Kwa sababu sisi watoto ni ndugu. Maandiko matakatifu nayo yaliweka bayana suala hili, “Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Rej., Mwz 2:24; Efe 5:31). Hii inadhihirisha kuwa wazazi wetu siyo ndugu kwa wao wenyewe. Maana kila mmoja alitoka kwao na kwa jamaa zake. Japo, sisi watoto ni ndugu. Wazazi ni watu wa muhimu sana katika Maisha yetu. Maana wao wamekuwa sababu ya sisi kuwa jinsi tulivyo.

Umoja wa Mataifa kwa kuona umuhimu wa hawa wasio ndugu, iliweka Juni mosi ya kila mwaka kuwa siku ya wazazi duniani, ni siku ya kuwaheshimu wazazi wote duniani kwa kutambua mchango na nafasi yao katika malezi ya watoto wao na jinsi wanavyojitoa kuwalea katika maadili. Ikiwa wazazi wanamchango mkubwa katika malezi na ulinzi kwa kila mmoja wetu, tunapaswa kuwaheshimu, kuwaenzi, kuwatunza na kuwajali katika hali zao[2]. Boniface mwaitege katika wimbo wake aliimba, “mzazi ni mziza (baba au mama) hata kama unamzidi elimu, kipato au uzuri”. Mwaliko wa kuwaheshimu wao ambao hawakuwahi kuwa ndugu ila kwa njia yao sisi tumefanyika kuwa ndugu ni dai la lazima.

Hata hivyo, siku ya wazazi ilianzishwa kama fursa ya kuwapongeza wazazi wote duniani kote na kuwashukuru kwa ajili ya jitihada zao mbele ya watoto na sadaka zao. Kuanzia miaka ya themanini familia ilianza kupata umuhimu mkubwa katika jumuiya ya kimataifa, hata katika uwajibikaji msingi wa elimu na ulinzi wa watoto na kuwafanya waendelee kukua binafsi kwa namna kamilifu na muungano[3]. Malezi bora mtoto huyapata toka kwa wazazi. Ndiyo kusema, “mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo” na “asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu”. Hivyo, kumbe ni muhimu na ni lazima kuwaheshimu hawa ambao wao siyo ndugu lakini wametufanya sisi tuwe kama tulivyo. Huu ndiyo mwaliko wa kuyaishi Maandiko Matakatifu kwamba, “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako” (Rej., Kut 20:12).
Malezi ndiyo msingi wa Maisha ya baadaye
Amri ya nne ya Mungu inatuamuru tuwaheshimu wazazi wetu. Na inaenda zaidi kwa kutuambia na kutuahidia kutuongezea heri na baraka kwetu sisi tunaoitii. Na hii amri haijawahi kubadilishwa licha ya sisi watoto wa leo kutokuiishi kwa kuwaheshimu wazazi wetu. Inasikitisha hivi leo inaposikika kwamba sisi Watoto tunapowadharau wazazi, tunapowasononesha kwa maneno, matendo au fikra zetu kwa kutokuwaheshimu, kuwaudhi na kuwa sababu ya masononeko na majuto katika maisha yao. Kwa hivyo, Amri hii inaendelea kutubana kwa kutupa mwaliko huo kama watoto ili kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kwamba, “Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana” (Rej., Wakolosai 3:20). Dai hili ni kwetu sote watoto, iwe ni vijana au wazee tuwaheshimu wazazi wetu kwa kuwatii (Rej., Lev 19:3; Meth1:8). Hata sisi watoto tunapokuwa na familia zetu, bado tunaendelea kudaiwa kuwapenda na kuwasaidia wazazi wetu. Tunatakiwa kuhakikisha kwamba wazazi wetu tunawatunza vizuri wanapozeeka, na hata kuwapa msaada katika Nyanja mbalimbali za kimaisha mfano msaada wa kiuchum (kifedha) inapohitajika. Kwani,

“Mungu alisema, ni lazima umtii baba na mama yako. Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe. Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu. Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo” (Rej., Mt 15:4-6; 1 Tim 5:4, 8). 

Hali hii hunikumbusha simulizi ambalo limekuwa likisimuliwa kila mara juu ya mama aliyeacha ujumbe kwa mtoto wake kabla ya kufariki. Yaani,
Barua ya mama kwenda kwa mwanaye, siku tatu baada ya mazishi ilisomeka hivi.

Mpendwa mwanangu. Nataka ujue kwa nini nilikufa nikiwa masikini wakati nina mtoto kama wewe. Mwanangu, nilitaka kukupa baraka zangu kabla sijafa, lakini sasa nimeondoka na baraka zangu. Chakula changu cha asubuhi, cha mchana na cha usiku kilikuwa miongoni mwa changamoto zangu nilipokuwa hai, lakini wewe umetumia pesa kupika kila aina ya vyakula, nyama, wali, pilau, na kununua aina mbalimbali za vinywaji siku ya mazishi yangu.

Mwanangu, ulichagua kuupaka mwili wangu uliokufa kwa kutumia mafuta mazuri na manukato yenye kunukia wakati nilipokuwa hai nilitumia mawese kujipaka kwa kukosa mafuta. Umeivika maiti yangu kwa nguo ghali wakati ulishindwa kuninunulia hata khanga nilipokuwa hai.

Maiti yangu ilipokuwa mochwari ulikuja kunitazama mara kwa mara, kwa nini umeijali maiti yangu wakati ulishindwa kunijali nilipokuwa hai? Kitu kinachoniuma zaidi ni jeneza la bei kubwa ambalo umeuweka mwili wangu ili hali nilipokuwa hai kwa maumivu makali niliishi katika nyumba mbovu ambayo haikumaliziwa kujengwa.

Ulipokuwa mdogo nilikaa na njaa ili wewe ule na kushiba, nilivaa nguo kuukuu ili upate nguo za kutosha. Nilidhani utanitunza nikizeeka. Wakati wa mazishi yangu ulimalizia nyumba, ukaipaka rangi na kuusafisha uwanja ndani ya wiki moja ili tu upate kuadhimisha mauti yangu. Sasa umeniandikia tanzia ukisema "Mama, nakupenda sana, pumzika kwa amani" ili hali nimekufa nikiwa na maumivu moyoni.

Mwisho kabisa, mwanangu, nimekuandikia kukukumbusha kuwa hakuna mtu anayempenda mtoto kama mama yake. Mungu akusamehe yaweza kuwa hukujua lile ulilokuwa unalitenda.

Mkazo katika simulizi hili ni kuwajali wao ambao hawakuwa ndugu wakiwa hai badala ya kuwajali wakiwa wamekufa. Tuwajali sasa wazazi wetu wakati wote wakiwa hai na hata baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa maana kazi yetu sote ni kupeana thamani tungali bado tunaishi. Inashangaza tunapoweka nguvu nyingi katika mazishi na kutokuwajali hawa wasio ndugu wanapokuwa katika mahangaiko yao hapa duniani. Tutaulizwa na tutatakiwa kujibu kama mwinjili Mathayo anavyotuhabarisha: 

"…Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia? Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi. Ndipo watu hawa watakapoondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele” (Mt 25:31-46). Wajibu wetu ni kupeana thamani katika maisha.

Nirudie tena kusema kwamba, “mtoto ni mtu mzima anayekua, na mtu mzima ni mtoto aliyekua”[4]. Kwamba, sisi watoto ambao sasa ni watu wazima tuna jukumu muhimu la kuhakikisha kwamba wazazi wetu walio katika utu uzima au uzee wanahitaji tuwatunze, kuwajali, na kuwapatia faraja. Maandiko Matakatifu yanatutanabaisha kuwa tunatakiwa kujifunza kutimiza wajibu wetu wa kidini kwa jamaa zetu wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wetu kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele za Mungu (Rej.,1 Tim 5:4).

Mwisho, Kila kitu alichokiumba Mungu alikipa uwezo wa kutoa kitu kingine ambacho kina manufaa katika uumbaji wake (Rej., Mwz 1). Hii ni kanuni ya asili ya uumbaji wote wa Mungu. Kila kitu kiliumbwa ili kikiwezeshe kingine kuufikia ukamilifu wake yaani kila kitu kiliumbwa kiwe baraka kwa kingine. Hii ndiyo maana halisi ya kwamba, Tulisaidiwa na watu ambao siyo ndugu, yaani wazazi wetu. Tuwapende, tuwadhamini, tuwaenzi, tuwatunze, tuwalinde na tuwahudumie wazazi wetu. Hawa, waliojisadaka katika maisha yao kuhakikisha kwamba sisi tunapata maisha mazuri na kuwa sababu ya furaha kwao na kwa wote tunaokutana nao katika maisha yetu. Upendo wetu kwao ndiyo zawadi pekee kubwa.
 
Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.

OMBI
Jumuika pamoja nami kufanikisha uchapaji wa vitabu vitatu vya imani na uinjilishaji vilivyoandikwa nami, na Mungu atakubariki sana. Unaweza kutuma mchango wako kwa njia ya M-Pesa kwenda namba +255754985663 (Emmanuel Kimambo Nhanwa) au bonyeza HAPA.

Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.

©2023 Ekinopia Studies