Tunapotengana Mengi Hutokea

 Tumsifu Yesu Kristo...

Utoaji mimba unatutenga na ukweli wa thamani ya maisha

Maisha ni fumbo mithili ya kifo. Hakuna anayeweza kulifumbua au kulielezea kinagaubaga. Ni fumbo linalotafakarisha na kutuacha muda mwingine bila majibu. Hii yawezakuwa kwa sababu maisha ni mchakato endelevu, unahohitaji kujitathimini, kujichunguza na kung'amua kipi kipo sawa na kwa nini kinatokea. Ni ukweli kwamba katika maisha mambo mengi hutokea: mazuri kwa mabaya. Hayo huweza kututenga ama kutuleta pamoja. Pia, ni asili ya maisha kudai kila kitu kuwa katika umoja. Maisha bila wengine hukosa ladha. Ndiyo maana John S. Mbiti anasema, "Mimi ni mimi kwa sababu sisi tuko, na kwa kuwa sisi tuko, kwa hivyo mimi niko". Mantiki ya hapa ni ile dhana ya jumuiya ya kujaliana na kutambua ya kuwa bila wengine mimi au wewe au yule si kitu.  

Dhana hii inakita mizizi  katika ubinadamu kwa wengine na imani ya kifungo cha ulimwengu cha kushiriki kinachounganisha wanadamu wote. Kwa maana ya kwamba, muunganisho wa watu binafsi ndani ya jamii au jamii. Hali ambayo hudhihirisha utambulisho wa mtu, kuwepo kwake, na ustawi wake unahusishwa na ustawi wa wengine au kikundi cha pamoja ambacho ni jumuiya, yaani jamii ambamo mwanadamu anaishi. Ndiyo kusema, umuhimu wa mahusiano ya kijamii: huruma, na ushirikiano katika kujiunda sisi ni nani, kama watu binafsi na inapinga dhana ya ubinafsi, ambayo inamtenga mtu na jamii yake na kutengeneza utupu ambao huleta madhara makubwa kwa jamii na kwa mhusika.

Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa utambulisho wetu na thamani yetu inatokana na uhusiano wetu na wengine na michango yetu kwa jumuiya tunamoishi. Mchango huu ufifishwa na kujitenga na wengine. Maandiko Matakatifu yanatutanabaisha juu ya hilo katika bustani ya Edeni, wazazi wetu wa mwanzo walipotengana tu, shetani alipata upenyo wa kufanya yake, na hivyo kutokea yale tunayoendelea kuyashuhudia na kuyavumilia kama vile kifo, magonjwa, chuki, visasi, wivu, na mahangaiko mengine ya maisha (Mwz 3). Dhambi ilingia duniani na kumwangamiza mwanadamu. Tunapojitenga mengi hutokea. Wana wa Israeli walipojitenga na Mungu wao, mengi yalitokea, kutapa tapa na kukumbuka masufuria ya nyama, kutengeneza ndama wa shaba ambayo ilikuwa kinyume na amri za Mungu (Kut 16:3; 32:1ff; 20:2-21). Mwanampotevu alipojitenga na baba yake, yaliyompata ni mengi na ya hatari, kujishibisha kwa maganda ya nguruwe, kujifananisha na nguruwe, kukosa msaada na kujishushia hadhi (Lk15:11-32). Ni kweli tunapojitenga mengi hutokea. Kipindi cha Mateso, Petro alipojitenga na Kristo aliingia katika “msonono“ wa mawazo, na ilimpelekea kumkana mara tatu; na mara Yesu akamgeukia Petro na kumuangalia. Petro akatoka nje, akalia kwa uchungu (Lk 22:54-62). Mengi hutokea tunapojitenga.

Swali ni kwamba, inakuwaje tunapotengana mengi hutokea? Je, ni nani au akina nani ninapojitenga nao mengi yanatokea? Je, ni wazazi, ndugu, rafiki, mpenzi, mke, mme, mwajiri, au mwajiliwa? Ni ukweli kwamba tunapojitenga na wale tuwapendao mengi huighubika mioyo yetu. Wazazi wanapotutoka mengi hutokea, ambayo kwayo hata midomo na mioyo yetu haiwezi kueleza: kuzulumiwa milathi, kutengana, kulumbana hata kufikia hatua ya kuuana. Je, hii ni kweli kwamba tunapotengana mengi hutokea? Tunapojitenga na wazazi baraka na neema za Mungu hutupisha pia. Kwa nini inakuwa hivyo? Kwa sababu ya kudharau amri za Mungu hasa ile ya kuwaheshimu baba na mama (Kut 20:12).

 Usaliti katika maisha ya ndoa unatutenga na ukweli wa upendo kwa wenza wetu

Mke na mme wanapotengana, yatokanayo huwa ni maumivu na matokeo mabaya kwa wanandoa wenyewe lakini pia kwa Watoto. Utasikia tangu niachane na mke wangu mambo yangu hayaendi vizuri, biashara imedolora, au Sina tena furaha. Kwa upande wa mwanamke anaweza jisemea, sitakuja kuwa na mwanaume tena. Ni kweli wapendanao wanapotengana furaha, amani, utulivu wa roho na nafsi hutoweka, roho ya uasi huingilia kati, kama vile chuki, kisasi, mauaji na mengine yafananayo na hayo.

Ninapojitenga na marafiki nini hutokea? Kukosa kampani (kujihisi mnyonge, nimepitwa na wakati, au mpweke). Vipi kuhusu binti au kijana uliyempenda mkajitenga naye (yaani uchumba, urafiki), nini hutokea? Kukata tamaa, kusononeka, kughadhabika, kukasirika na hata kufikia kujinyonga, kutafuta mpenzi mwingine, kuchukia jinsia hiyo au nini hutokea kwako? Mengi hutokea tunapojitenga.

Ni ukweli kwamba, kuna watu, vitu au mambo tukijitenga nayo mengi hutokea, lakini hayo huwa ya kawaida na ya hapa duniani, japo kuwa, huziumiza roho na mioyo yetu. Lakini Kuna kitu kimoja tu tukiachana nacho mengi hutokea zaidi. Kujitenga na Kristo (Mungu kweli na Mtu kweli), mengi hutokea zaidi ya kujitenga na wazazi, marafiki, ndugu na wengineo. 

Ni kweli kwamba, tunajitengaje na Kristo kwa namna mbalimbali:

Kutokuiungama imani waziwazi. Ni kujitenga na Kristo.  Hili ungamo siyo tu suala la kutamka maneno bali lazima liguse maisha ya ndani ya kila mmoja wetu.  Wale ambao huikiri imani hewani hewani, hawaioneshi kwa mawazo, matendo, na maneno, sio tu hawataokoka, bali watahukumiwa vikali kwa maana wapo kinyume na imani aliyotuachia Kristo Bwana. Kwa maana wametengana naye kwa Maisha yao yasiyofaa. Na Kristo mwenyewe anasema “mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu” (Mt 12:30). Kujitenga na Kristo Mengi hutokea.

Kwa kutokupokea Sakramenti zake. Sakramenti ni alama wazi iliyowekwa na Yesu Kristo ili kutuletea neema ya wokovu (Mdo 8:17). Sakramenti zatuletea neema kwa nguvu zilizowekwa ndani yake na Kristo Yesu mwenyewe. Anayepokea Sakramenti katika hali mbaya anatenda dhambi kubwa ya kukufuru, wala hapati manufaa ya Sakramenti hizo. Kwani kwa kuwa na dhambi tayari amejitenga na Mungu. Dhambi hututenga na Mungu na wenzetu; pia nafsi ya mdambi hutafakuriana na uhalisia wa Maisha. Hivyo basi, ni katika hali ya neema tu utaweza kupata thawabu iliyopo katika Sakramenti hizi. Kwa hiyo, ni kwa njia ya Sakramenti tunapata nafasi ya kujipatanisha na kukutana na Mungu; hasa tunapokuwa katika hali ya neema. Kristo ameweka Sakramenti saba, nazo ni: Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Ndoa na Daraja Takatifu ya Upadre. Hizi ndiyo password za kutokujitenga na Mungu. Lakini lazima tuwe katika hali ya neema. Kwa kutokupokea sakramenti za kanisa, tayari tunakuwa tumejitenga na Kanisa, yaani Kristo.

Kwa kutoheshimu mamlaka ya Kanisa. Hiki nacho hututenga na Mungu tunapowadharau mawakala wake. Ni kweli kwamba, kila mbatizwa mkatoliki anatakiwa kuheshimu uongozi wa Kanisa, tukianza na: Baba Mtakatifu, Maaskofu, Mapadre na viongozi wengine ambao kwayo Kanisa limewaweka ili waweze kuitimiliza kazi ya Kristo. Kushindwa kufanya hivyo ni kujitenga na Kanisa. Kwa hulka yake Kanisa huwa halimtengi muumini wake au mtu yoyote, mtu au muumini mwenyewe hujitenga na Kanisa.

Ndiyo maana Mt. Paulo anapowaandikia Warumi anawauliza, nini kitakachoweza kumtenga na upendo Kristo?

“Ni nani atakayetutenganisha na upendo wa Kristo? Ni shida? Au taabu? Au mateso? Au njaa? Au umaskini? Au hatari? Au Kifo? Hapana. Kama Maandiko yasemavyo: Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo yote haya sisi ni washindi, naam, na zaidi ya washindi, tukiwa ndani yake yeye aliyetupenda. Kwa maana nina hakika kuwa, si kifo wala uzima; si malaika wala mashetani; si mambo ya sasa wala mambo yajayo au mamlaka nyingineyo yote; si mambo yaliyo juu wala yaliyo chini sana; wala hakuna kitu kingine chochote kati ya vitu vyote alivyoumba Mungu kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio ndani ya Kristo Yesu Bwana wetu” (Rum 8:35-39).

Ni kweli tunapojitenga na Kristo mambo mengi hutokea ambayo huingia kwa njia ya dhambi, ambayo ndiyo chanzo cha kututenga na Mungu ambaye ni chanzo na kikomo cha Maisha yetu. 

Dhambi ni nini? Dhambi ni kosa la kiumbe hai mwenye hiari (akili na utashi) dhidi ya uadilifu unaompasa. Hii hutendeka kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu. Dhambi ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu (Amri za Mungu na za Kanisa). Mwanadamu kwa kutafuta uhuru wake nje ya mapenzi ya Mungu hujikuta anajitenga na Muumba wake, jamii yake na hata utu wake kwa machaguo anayoyafanya. Kwani hivi leo Kuna kasumba kubwa ya mwanadamu wa karne hii ya 21 kujifananisha na wanyama. Hata hivyo, wanyama hawabanwi na kifungo hiki cha maadili kwa sababu wao hawana akili na utashi (they are amoral). Bali sisi wanadamu tulioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwz 1:26), ndiyo wenye uwezo wa kujitenga na Mungu. Kitabu cha Mwanzo kinaelezea hilo kwamba tunapojitenga na Mungu hutokea mengi: magonjwa, hofu, kifo, na mahangaiko mengine ya maisha. Adamu na Eva walipojitenga na Mungu mengi yalitokea. Wanawaisrael walipojitenga na Mungu amani na furaha ilitoweka, mwanampotevu alipojitenga na familia yake mengi yalimtokea.

Je, tufanye nini sasa ili tuweze kurudisha ule uhusiano uliopotea kwa kujitenga kwetu? Kwanza, ili muumini uwe katika muungano na Kanisa kuna mambo matatu muhimu ya kuangalia kama Mkusanyo Sheria Kanoni unavyobainisha: “Walio kikamilifu katika ushirika wa Kanisa Katoliki hapa duniani ni wale waliobatizwa ambao, wameunganika na Kristo katika mpangilio wake uonekanao, yaani kwa vifungo vya ungamo la Imani, Sakramenti, na uongozi wa Kanisa” (Kanoni, n. 205)

 Tumrudie Kristo kwa moyo wa toba: Na ingekuwa heri leo msikie sauti yake (Zab 95:7b)

Kwetu sisi tunaomwamini Kristo, sheria ya Kanisa inaendelea kutuweka bayana kuwa, “Kwa ubatizo mtu anaingizwa katika Kanisa la Kristo na kufanywa kuwa nafsi katika lenyewe, akiwa na wajibu na haki, ambazo kulingana na kila hadhi ya mtu, ni za kufaa kwa kila Mkristo, kwa kadiri walivyo katika muungano wa kikanisa na isipokuwa kama kikwazo halali kimeingilia” (Kanoni, n.96). Aidha, Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano wanasisitiza kitu kilekile: “…basi wanaingizwa {waamini} kikamilifu katika jumuiya ya Kanisa wale ambao, wakiwa na Roho wa Kristo, wanakubali muundo wake mzima na njia zote za wokovu lilizopewa. Tena katika mpangilio wake uonekanao, wanaunganika na Kristo-aliongozaye Kanisa kwa njia ya Baba Mtakatifu na Maaskofu - kwa vifungo vya ungamo la Imani, sakramenti, uongozi wa Kanisa na ushirika. Lakini yule ambaye hadumu katika upendo na akaa ndani ya Kanisa kwa mwili na si kwa moyo, ijapo ameingizwa katika Kanisa, hataokoka…” (Lumen Gentium (Fumbo la Kanisa), n.14).

Tunajitenga na Kanisa tunaposhindwa kutimiza wajibu zetu na hivi kushindwa kupata haki zetu kama waamini. Hivyo basi ili tuwe katika muungano na Kanisa lazima tuwe na imani kwa Kristo, imani katika sakramenti zote saba na utii kwa mamlaka ya Kanisa. Ndiyo mwaliko sasa, kwamba tuiishi imani yetu inavyostahiri, kupokea sakramenti za Kanisa, na kama kuna kizuio chochote; tufanye juhudi na kutafuta msaada kutoka kanisani ili tusiendelee kujitenga na Mungu wetu. Mwisho, Utii na Heshima kwa Uongozi wa Kanisa, unaomwilishwa katika matendo mema na dhamiri njema ya waamini kwa wachungaji wao. Nia njema iwe dira yetu.

Fr. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Catholic Diocese of Shinyanga, University of Navarra, Pamplona, Spain.


OMBI
Jumuika pamoja nami kufanikisha uchapaji wa vitabu vitatu vya imani na uinjilishaji vilivyoandikwa nami, na Mungu atakubariki sana. Unaweza kutuma mchango wako kwa njia ya M-Pesa kwenda namba +255754985663 (Emmanuel Kimambo Nhanwa) au bonyeza HAPA.

Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa, 
Jimbo Katoliki Shinyanga, Chuo Kikuu Navarra, Pamplona, Hispania.

©2023 Ekinopia Studies