TUMSIFU YESU KRISTO...
Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu[1]. Mungu wetu daima anatuita sisi viumbe wake tuwe watakatifu na wakamilifu kama Yeye alivyo Mkamilifu. Ni vyema kila muumini atambue kuwa, ameumbwa ili siku moja awe mkamilifu kama Muumba wake alivyo. Tukiwa na mtazamo huo mintarafu maisha yetu ya kila leo; twaweza kujiuliza, je, watakatifu waweza patikana miongoni mwetu? Hawa watu wanakuwaje? Haya maswali yote yatapata majibu yake tukielewa mtakatifu ni mtu wa namna gani na wajibu wake ni upi. Karibu tusafiri pamoja katika tafakari hii ambayo itatufumbua na kuzibua macho na masikio ya mioyo yetu na kulitamani daima lile lengo msingi la wito wetu, kuwa watakatifu.
Mtakatifu ni nani? Mtakatifu ni mtu wa namna gani? Mtakatifu ni mtu wa kawaida. Huyu mtu wa kawaida ni wa namna gani? Mtu wa kawaida ni yule aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu[2]. Hivyo basi mtu ambaye si wa kawaida ni yule asiyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hana sura wala ufanano na Mwenyezi Mungu ndani yake. Ili kutimiza mapenzi ya Muumba wake, huyu mtu wa kawaida anatakiwa kutimiza wajibu aliowekewa tangu kuumbwa kwake. Wajibu wa mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni kumjua Mungu, kumpenda Mungu, kumtumikia na hatimaye kufika kwake mbinguni[3]. Huu ndio mwito wake anaoitiwa na Muumba wake. Ni katika kutimiza wajibu huo kiaminifu ndipo anapojiunda kuwa mtakatifu wa Mungu; yaani kuurithi ufalme wa mbinguni. Kutimiza huko hayo ndiyo moja ya namna ambayo huyu mtu wa kawaida anahesabiwa kuwa mmoja wa washindi wa ulimwengu huu na ujao, anaouendea. Hivyo basi, mtakatifu ni mtu wa kawaida kabisa na anayeishi zile tunu za kiutu na kikristu.
Kwa mtazamo wa hapo juu, nidhahiri kuwa, Utakatifu sio nafasi waliyotengewa wachache au kundi maalum la watu pekee bali ni nafasi ya wote ukiwamo na wewe unayesoma makala hii muda huu. Mungu ametuumba ili tuufikie utakatifu, yaani tuishi naye milele. Ndivyo katekisimu yetu inavyotueleza; Kwa nini Mungu ametuumba? -Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende na tumtumikie tupate kufika kwake mbinguni. Kwa mtu asiyekuwa wa kawaida kwake haya si kitu, maana hamjui, hampendi, na hamtumikii Mungu badala yake anamtumikia ibilisi, amemkumbatia na kumgeukia aliye muovu ambaye hawezi kumfikisha mbinguni; kwa Mungu.
Sanjari na yote hapo juu, Mtakatifu ni mdhambi aliyetubu (a confessed sinner). Mt. Yohane anasema “tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote”[4]. Hii inaendelea kututhibitishia kuwa mtakatifu ni mtu wa kawaida kabisa na anaishi katika mazingira ya jamii yetu ya kawaida na anakumbana na changamoto za kila siku. Lakini sasa, huyu mtu (mtakatifu) anakuwa na roho ya utayari ya kujirudi, kujuta na kutubu dhambi zake.
Na Maandiko Matakatifu yanasema “jiosheni, jitakaseni, ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya, jifunzeni kutenda mema…haya, njoni tusemezane asema Bwana. ‘Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”[5]. Huyu ni yule anayejisafisha uchafu (dhambi) wake kwa Sakramenti ya Upatanisho (Kitubio) na kurudisha uhusiano wake uliokuwa umepotea. Kwa sababu, Sakramenti ya Kitubio yatuondolea dhambi zetu na adhabu ya milele, yatakatifuza roho zetu na zaidi yatuthibitisha na yatuimarisha kutenda mema. Ni kwa kuikimbilia na kuijongea Sakramenti ya Kitubio, huyu mtu anajiandalia mazingira ya kuwa mtakatifu. Anakuwa katika hali ya neema ya utakaso ambayo ni uzima wa kimungu rohoni mwake. Neema ya utakaso inamfanya kuwa mtoto mpenzi wa Mungu na mrithi wa mbingu[6]. Njia ya kuelekea utakatifu ni njia ya kujitakasa kila wakati. Tusione haya kuijongea Sakramenti ya Kitubio, kama ni kuona haya basi tuone haya kuingia dhambini[7].
Kristu mwenyewe katika kuanza kazi yake ya kuihubiri Injili aliwaita watu wote watubu kwa kuwa ufalme wa Mungu umekaribia[8]. Hii ndiyo namna ya kuwa mtakatifu katika hali ya kawaida. Siyo lazima ufanye mambo makubwa haya madogo tu ndiyo yanampeleka mbinguni huyu mtu wa kawaida. Kristu pia anaendelea kutualika kuukimbilia utakatifu na ukamlifu ili tuweze kufanan na Mungu ambaye ni Utakatifu wenyewe[9]. Hivyo, hatuna budi nasi kufanana na Baba yetu. Kwa kuwa huo ndio mwito wa Mungu kwa kila mmoja wetu. Hii ni kwa sababu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Yafaa watu wamfahamu Baba yetu kwa kututazama sisi. Tunaona kuwa sisi tumechaguliwa kuwa watakatifu; tumeitwa kuwa wanaume na wanawake watakatifu. Tumeitwa kuwa kanisa takatifu na tumepewa neema ya kuwa watakatifu[10]. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wetu kila mmoja impasavyo na hivi mwisho wake tuweze kuurithi ufalme wa mbinguni.
Kuonesha umuhimu wa hili, Kanisa limeweka siku ya tarehe 1 November kila mwaka kuwa kwa ajili ya kuwaadhimisha Watakatifu wote. Tunafahamu kuwa ipo orodha rasmi ya watakatifu ambao Kanisa limewatangaza na limepanga maadhimisho yao katika siku mbalimbali ndani ya mwaka wa kiliturujia wa Kanisa. Pamoja na orodha hiyo, Kanisa linatambua pia wapo waamini ambao baada ya maisha yao hapa duniani wamepewa tayari tuzo la utakatifu huko mbinguni. Hawa ni maelfu kwa maelfu na miongoni mwao huenda wamo wazazi wetu, bibi na babu zetu, watoto wetu, ndugu, jamaa na wengine wengi ambao wameishi kwa kumtafuta Mungu na kutimiza mapenzi yake katika maisha yao[11]. Wote hawa ni watu wa kawaida tu, waliojitahidi kutimiza mapenzi ya Muumba wao. Siku zote tujipe moyo kwamba tunaweza kuwa watakatifu tukifuata mifano ya wanaume na wanawake wengi ambao wameweza kuwa watakatifu. Kwa nini sisi tushindwe?
Mwisho, mwito wetu kwa Mungu ni uzima wa milele, kuwa watakatifu. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kuwa mtakatifu tu akitimiza wajibu wake hapa duniani. Na cha zaidi kuishi katika neema ya utakaso. Hii itawezekana tu tukiweza kuziishi tunu za kiutu na za kikristu itupasavyo. Mt. Yohane Paulo II anasema “tusiuogope utakatifu” tuutafute maana tumewekewa na Mungu. Ni wajibu wetu kushirikiana na neema ya Mungu ili tuweze kufika huko kwake mbinguni. Hivyo basi mimi na wewe unayesoma makala hii tuna nafasi bado ya kutengeneza maisha yetu yajayo. Kwa kuwa wito wa kuwa watakatifu ni wa watu wote. Tupelekane wote kwenye utakatifu; yaani Mbinguni.