TUMSIFU YESU KRISTO...
Kati ya masomo niliyokuwa nayependa kipindi nasoma ni hesabu na uchumi. Nakumbuka nilipokuwa darasa la kwanza, mmoja wa wanafunzi wenzangu aliuliza swali, yaani 1-2=…? Na mwalimu wetu wa hisabati alijibu kwa upole haiwezekani. Nasi tukaondoka na mantiki hiyo hiyo. Lakini tulipofika darasa la tatu, swali hilo mwalimu mwingine alituuliza darasani na tukajibu kwa kujiamini kuwa haiwezekani. Mwalimu alitabasamu kisha akaenda ubaoni akaanza kutufundisha nini maana ya kukopa na kwenda na moja kichwani (chanya na hasi). Ndipo nikajua kuwa kila kitu kina mbandala wake. Ni katika hili nilipokuwa nasoma Falsafa nilikutana na kanuni nyingi: nzuri na mbaya. Lakini hii ya falsafa ya kukopa niliipenda zaidi.
Falsafa maana yake ni nini? Neno 'falsafa' asili yake ni neno la Kigiriki 'philosophia' ambalo linaundwa na maneno mawili yaani, 'phileo' (upendo) na 'sophia' (hekima). Kwa hiyo, maana halisi ya falsafa ni 'kupenda hekima' au upendo wa hekima. Falsafa ni fikra endelevu, yenye utaratibu, na tafakari kuhusu dhana na imani mbalimbali. Kwa upande mwingine, Kukopa ni kuchukua au kupokea kitu kwa ahadi au nia ya kukirejesha. Hivyo, Falsafa ya Kukopa ni fikra inayotupeleka katika utaratibu, mantiki na tafakari ya kuchukua au kupokea kitu kwa ahadi au nia ya kukirejesha.
Ukweli ni kwamba, Kukopa ni harusi kurudisha ni matanga. Katika Maisha mtu anapokuwa na shinda hutafuta njia mbalimbali ili kutatua shida yake. Na anapokuwa mhitaji huja kwa maneno mazuri na ya kuridhisha. Lakini falsafa hii inatuambia kuwa ili mtu uweze kukopa kwa namna iliyo sahihi lazima kuwe na mambo haya matatu: Lazima kuwe na Sababu kubwa ya Kukopa (there must be grave reason); Lazima uwe na uwezo wa kurudisha kile ulichokopa (Ability to pay back) na Lazima uwe na nia ya kurudisha (willingness to pay back).
Lazima kuwe na Sababu kubwa ya Kukopa (there must be grave reason). Ilikusudi uweze kukopa, lazima kuwe na sababu kubwa ambayo kwayo bila kufanya hivyo kitu kibaya kinaweza tokea, mfano kupoteza uhai. Lakini katika ulimwengu wetu wa sasa kuna baadhi ya watu ambao hukopa kwa ajili ya kwenda kula bata (kufanya tafrija na anasa kama kituo cha njia ya msalaba namba tisa kisemavyo) Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Inaweza kuwa kwa ajili ya kununua mavazi, kula hotelini, au kwenda likizo. Tunafanya kwa hela ya mkopo. Wengine hata wamekopa kwenye vikoba kwa lengo la kukwepa kula tembele au dagaa kila siku, lakini yaliyowakuta wanajua wao. Hii sababu inatudai lazima tuwe na sababu nzito ya kutufanya tuingie katika madeni. Kama hakuna sababu ya kufanya hivyo basi tusikope. Tujifunze kusema kusema hiki sawa (ndiyo), na hiki si sawa (siyo), kwa maana linalozidi hayo linatoka kwa yule mwovu (Mt 5:37).
Lazima uwe na uwezo wa kurudisha kile ulichokopa
Lazima uwe na uwezo wa kurudisha kile ulichokopa (Ability to pay back). Ili mkopo uwe na tija lazima uwe na uwezo wa kurudisha kile ulichokopa. Kama huna uwezo wa kufanya hivyo usikope au kopa kulingana na uwezo wako. Hapa kukopa siyo pesa tu, kuna vitu vingi tunaweza kukopa. Mfano, unaenda kukodi gari ufanyie mtoko au matembezi kwa makubaliano ya kwamba, lolote litakalotokea utawajibishwa. Hii ndiyo kusema, kusikia kwa nkenge mpaka damu masikio. Watu wengi hivi leo wanaingia katika mtego huu wa kuchukua mkopo wa gari na baada ya siku chache wengine magari hayo yanapata shida kama ajali, kuharibika kusikotengenezeka tena. Lakini wengine yamewaongezea gharama ya Maisha na kuishia kuwa watumwa wa magari hayo. Sanjari na hayo, muda wa kurudisha walichokopa unapofika na hawana kitu mnyororo wa mawazo na magonjwa huwasonga na wengine imewapelekea hata kupoteza Maisha. Chezea madeni wewee‼ Kama huna uwezo wa kukopa na kulipa kile ulichokopa, acha, badala yake omba msaada.
Lazima uwe na nia ya kurudisha (willingness to pay back). Katika dunia tunayoishi, kuna watu ambao hukopa kwa lengo la kutokurudisha yaani huwa na nia ya kudhulumu na wengine kwa lengo la kuja kuomba msamaha ili wasamehewe deni, hii ni hatari. Aidha, kuna wengine ambao wanakopa kwa lengo la kutokurudisha licha ya kuwa na uwezo. Maandiko Matakatifu yanawaonya hawa kwa kusema: “Mtu mwovu hukopa bila kurudisha” (Zab 37:21a). Hii inatakusema kwamba, mtu yeyote anayekopa bila nia ya kurudisha anatenda lililo ovu moyoni mwake. Huyo ni muovu au mhalifu kama wahalifu wengine. Maana anadhamiria kudhulumu na kulaghai kwa nia thabiti. Mtu kama huyu adhabu yake ni kubwa mno.
Maandiko Matakatifu ni kweli hayakatazi au kuhukumu kukopesha pesa au kitu chochote ambacho kinafaa kufanya vile. Japo yanashauri kwamba kila mara si kitu kizuri kila mara katika Maisha yetu kuingia katika deni. Kwa sababu madeni hutufanya kuwa watumwa kwa wale wanaotupa mkopo. Kitabu cha Mithali kinathibitisha hilo, “Na mkopaji ni mtumwa wa mkopeshaji” (Mithali 22:7b). Kwa wakati huo huo, katika hali ya kawaida madeni hutuingiza kidogo kidogo katika hali ambayo tunaweza kuiita “dhambi ya lazima”, kwa maana kama umekopa na ukashindwa kurudisha au kufanya kulingana na makubaliano utaingia katika dhambi ya uongo, chuki, visasi, maseng’enyo na hata wakati mwingine kupelekea kuuana. Na hii umuanika mhusika. Kwa maana, mtu hufunua mambo mengi sana juu yake mwenyewe kwa namna anavyoshughulikia madeni aliyo nayo. Madeni hutudharirisha na kufifisha utu wetu. Tunajiona hatufai. Lakini swali msingi, ni kwa nini tunakopa bila mpangilio? Kila mmoja wetu anaweza jibu swali hili kwa namna yake.
Hata hivyo, Mtume Paulo anatuambia bayana kuwa, “Msiwe na deni la mtu ye yote; isipokuwa deni la kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria” (Rum 13:8). Aidha, William Shakespeare mwandishi Mwingereza wa tamthilia anasema wazi, “Usiwe mkopaji wala mkopeshaji; kwa sababu mara nyingi fedha hupotea na urafiki kuharibika.” Wahenga walisema, “pesa ilishaharibu undugu”. Hivyo sasa ni wakati wa kuwa tayari kuacha madeni ambayo siyo ya lazima. Wakristo tunakumbushwa kwamba Mungu anaona kila jambo na kwamba tutatoa hesabu ya jinsi ambavyo tunajiendesha wenyewe na kwa njia ambayo tunatumia mali zetu au za wengine. Ndiyo mwaliko sasa wa kuyafanya, “Mambo yote mnayofanya yafanyeni kwa upendo” (1Kor 16:14). Tufanye nini sasa ili upendo wetu uendelee kuwepo na tuiishi hii falsafa ya kukopa?
Kwanza, tujue na tupangilie matumizi ya mapato yetu. Tusikimbilie kununua vitu kwa sababu tu vimepunguzwa bei (mfano sasa msimu wa Sikukuu punguzo la bei lisiwe kivutio cha kuingia katika madeni) au kwenda kutanua kwa sababu tu wenzetu wanaenda kutanua. Tuweke na tupange bajeti zetu na tuzifuate kwa uaminifu, kinyume na hapo tutaangukia kwenye kukopa. Madeni yanaua tuache. Pili, tuepuke madeni yasiyo ya lazima. Kwa maana mkopaji ni mtumwa wa mtu anayemkopesha, je tunapenda kuwa watumwa? Ukitaka kuona chungu ya Maisha ya kukopa. Tatu, tuwe na uchungu na pesa tunayoitafuta na kuipata. Pesa ya jasho letu lazima ituume. Kitu kinapata thamani pale inapotokea mtu anajua namna alivyoipata. Mfano aliyepata kwa kuponda kokoto anajua maumivu aliyoyapata, au mkulima baada ya kuuza mazao yake anajua jinsi alivyotaabika na kulima, kupalilia na hatimaye kuvuna. Nne, tujifunze kuridhika na vitu tulivyonavyo. Kwa sababu, kama umeshindwa kushiba kwa kuchovya, huwezi kushiba kwa kukombeleza. Kwa maana, kama “Tukiwa na chakula na kitu cha kujifunika, tutaridhika na vitu hivyo” (1Tim 6:8). Pesa haziwezi kununua furaha na uradhi. Baadhi ya watu walio na furaha nyingi ulimwenguni hawana pesa nyingi. Wana pesa inayokidhi mahitaji yao na wanafurahia upendo wa familia na marafiki wao na ni rafiki za Mungu.
Kwa upande wa kiroho: Maisha, kifo na kufufuka kwa Yesu kumetulipia deni ya dhambi zetu kwa Mungu. Lakini kwa nini tunaendelea kukopa kila mara na kubaki katika deni hilo? Deni hili ni dhambi. Ama kweli sisi wanadamu tunapenda utumwa. Unapokuwa mdaiwa unakuwa mtumwa. Tunapotenda dhambi tunakuwa watumwa wa shetani na malaika wake. Tunakuwa mawakili wake. Mwaliko, ni kukwepa nafasi zote zinazoturudisha katika deni hili la kiroho. Wengi wetu tunakopa kwa kumuasi Mungu, kuabudu sanamu, kushikiria imani za kishirikina, uongo, wizi, na hata kutumia mali ya umma kwa maslahi binafsi. Wengine wanatumia shida za watu wengine kujipatia maslahi yao hii nayo ni deni, ni mkopo ni dhambi. Hata hivyo, wengi tumekuwa tukiwaza tu madeni ya kiulimwengu kama fedha na mali nyingine za kiulimwengu. Tunasahau kuwa nasi bado tunadaiwa kwa kukopa mengi. Jiulize, yaani mimi na wewe umekopa nini na bado hujakirudisha? Tujitahidi kumaliza madeni ili baraka na neema ambazo Mama Kanisa anazitoa kwa wana wake katika kipindi hiki cha Majilio na baadaye Noeli ziweze kutufaa na kutusindikiza katika mwaka ujao 2024.
Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2024.