MAHUJAJI WA MATUMAINI NA KWARESIMA

 TUMSIFU YESU KRISTO...!

Kwaresma ni safari ya siku arobaini

Katika safari ya maisha ya Kikristo, mwamini anaitwa kuwa mhujaji; yaani, msafiri wa imani anayetembea kuelekea lengo la wokovu. Maisha yetu hapa duniani ni hija inayotuelekeza kwenye uzima wa milele, na kila mwamini anapaswa kutembea katika mwanga wa imani na matumaini. Katika Jubilei na kipindi cha Kwaresima, wito wa kuwa "Mahuja wa Matumaini" unapata maana ya kina, ukitualika waamini wote kushiriki toba, upyaisho wa maisha, na matumaini katika ahadi ya Mungu.

 

Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa maisha ya mkristo ni hija ya imani inayoelekea kwenye utimilifu wa wokovu ndani ya Mungu. Katika safari ya hija, waamini tunapitia changamoto, majaribu, na neema katika safari yetu ya kiroho. Kwaresima, ambayo ni kipindi cha toba, sala, na matendo ya huruma, huu wakati mwafaka wa kuimarisha hija yetu ya kiimani.

 

Hivyo basi, katika maisha ya kiroho, mahujaji wa matumaini ni wale wanaosafiri kuelekea katika umoja na Mungu kwa moyo wa imani, toba, na matumaini. Katika hili tunaona kuwa, matumaini ni nguvu inayoelekeza moyo wa binadamu kwa kile ambacho bado hakijafikiwa, lakini kimeahidiwa na Mungu. Hiki kilichoahidiwa kwetu ni uzima wa milele, kwa wale wote wanaokubali mwaliko wa Mungu (Mk 16:15-16).

 

Tunaweza kujiuliza kwa wakati huu kwamba, jubilei ni nini? Kwa haraka tunaweza sema, jubilei ni kipindi cha neema, msamaha, na huruma ya Mungu, kinachowaita waamini kujitakasa na kurejea kwa Baba wa mbinguni (Wal 25:10ff). Ni mwaka mtakatifu si tu kwa sababu unaanza, unaadhimishwa na unahitimishwa kwa madhehebu matakatifu, bali pia kwa sababu unachochea utakatifu wa mwaisha...Ni kipindi cha kumtafuta Kristo anayetutangazia Habari Njema (Ujumbe wa Kwaresima 2025, TEC, n. 33). Katika Maandiko Matakatifu, mahujaji walikuwa wale waliokwenda Yerusalemu kwa ibada, wakitamani kukutana na Mungu (Zab 84:5-7). Hija zao zilikuwa ishara na safari ya kiroho kuelekea maisha ya milele. Ni uhalisia ulio wazi kwetu sote kwamba, katika mwaka wa Jubilei, tunaitwa kuwa mahujaji wa matumaini kwa kujikita katika toba, upatanisho, na matendo ya huruma (mwili na roho). Yesu mwenyewe anasema: "Roho ya Bwana i juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa." (Luka 4:18-19). Kristo anatualika tumwelekee yeye na kusikiliza maana amekuja kutuhubiria habari njema. Na kabla ya hapo, anapoanza kutuhubiria anatuambia, “tubuni na kuiamini injili” (Mk 1:5). Mwaliko wa kuyapaisha maisha yetu ya kiroho.

 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Kwaresima 2025, unaoitwa "Tusafiri Pamoja katika Matumaini," unatoa tafakari ya kina, ukiwaalika waamini kuuishi wakati huu kama hija ya wongofu na uaminifu, ukikazia umuhimu wa sinodi na matumaini ya Kikristo. Papa Francisko anakumbuka safari ya watu wa Israeli kuelekea Nchi ya Ahadi, akihimiza kutafakari juu ya hali yetu wenyewe kama mahujaji maishani. “Sote tumeitwa kutembea pamoja, bila kumwacha yeyote nyuma,” akionyesha thamani ya ushirika na mshikamano ndani ya Kanisa na ulimwengu. Baba Mtakatifu kwa ujumla amebainisha mambo matatu ya msingi: kutembea, kutembea pamoja, na kutembea katika matumaini, akiwataka waamini kuonja Kwaresima kama kipindi cha kufanywa upya na kutumainia ahadi ya uzima wa milele.

Kwaresima ni safari ya siku 40 inayotuandaa kwa Pasaka

Ni katika mtazamo huu, kipindi cha kwaresma kinapata nguvu katika maisha yetu ya kikristo hasa tunapohusianisha jubilei ya mwaka huu 2025. Tunaalikwa kuona uhusiano ulipo kati ya Mahujaji wa Matumaini na Kwaresima. Kwani, kwaresma ni nini? Kiufupi, kwaresima ni safari ya siku 40 inayotuandaa kwa Pasaka, ikitualika kushiriki mateso, kifo, na ufufuko wa Kristo. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Tanzania kwa Kwaresima 2025, unaoitwa “Simameni Imara katika Imani” (1Kor 16:13) umeweka bayana kuwa Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za toba, kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma. Aidha ni kipindi chaa kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu, kupitia njia ya imani, ambayo kwayo mwanadamu anashiriki kuujenga ufalme wa Mungu, na ufalme wa upendo, wa haki na amani... (n.17). Ni kipindi cha kufunga, kusali, na matendo ya huruma (Mt 6:1-18). Katika Maandiko Matakatifu, hija ni sehemu muhimu ya safari ya kiimani. Mungu alimwita Abrahamu kutoka Uru wa Wakaldayo akamwambia: "Toka katika nchi yako, jamaa zako na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha" (Mwz 12:1). Abrahamu alikubali kuwa mhujaji kwa imani, akimtegemea Mungu pekee. Hili linabaki kuwa mwito kwa waamini wote: kuishi kwa imani na matumaini, hasa katika kipindi cha Kwaresima (Ujumbe wa Kwaresima 2025, TEC, n. 22). Kama mahujaji wa matumaini, tunapaswa kutumia Kwaresima kwa:

 

Kutubu dhambi

Maandiko Matakatifu yanatualika bayana yakisema, "Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mungu umekaribia" (Mt 3:2; 4:17). Ni ukweli kwamba, toba na uongofu wa moyo ndiyo kitu cha msingi katika maisha yetu ya ufuasi. Toba si tu kujutia dhambi, bali ni kubadilika na kumrudia Mungu kwa moyo wa dhati. Nabii Yoeli anatualika kwa maneno haya akisema: “…nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza” (Yoeli 2:12). Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa kiini cha hija yetu ya Kwaresima, kwani inatuunganisha tena na Mungu.

Kwaresima ni wakati wa kufunga, kusali na kufanya matendo ya huruma

Kujitoa kwa sala 

Yesu alijitenga nyikani kwa siku 40 akiomba na kufunga (Lk 4:1-2). Hapa Kristo anatufundisha kuwa, sala na tafakari ya Neno la Mungu ni ya muhimu katika maisha yetu ya ufuasi.  "Mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu" (Mt 4:4). Kama mahujaji wa imani, tunapaswa kukumbatia sala kwa moyo wote. Yesu mwenyewe aliingia nyikani kwa siku 40 kusali (Lk 4:1-2), hivyo nasi hatuna budi kuingia nyikani kwa moyo wa sala. Maana sala ni njia ya kumwinulia mioyo yetu na kumnyenyekea Mungu; yaani, ni tendo la unyenyekevu. Mt. Teresa wa Avila anaenda mbali zaidi na kusema, “sala ni tendo la upendo, maneno hayahitajiki”. Hivyo, anahimiza muunganiko wa ndani na wa kudumu kati ya anayesali na Mungu. Anasisitiza kwamba katika sala, tusali kwa moyo wa imani na matumaini bila kukata tamaa. Kwa kusali na kutafakari Maandiko, tunajenga mahusiano ya kina na Mungu. Ndivyo alivyofundisha Mt. Ambrose, alisema: “tunaposali tunaongea na Mungu, na tunaposoma Maandiko Matatifu, Mungu anaongea nasi”. Ni katika hali ya ukimya na ukunjufu wa moyo tunaweza kumsikiliza na kumuelewa Mungu anataka tufanye nini, hasa kwa kusoma Neno lake. Katika mantiki hiyo, Mt. Yohane wa Msalaba anasisitiza kusema kwamba: "Kadri nafsi inavyomsogelea Mungu, ndivyo inavyotakaswa kwa moto wa upendo wake." Tafakari ya mateso ya Kristo inatufundisha kuwa Kwaresima ni safari ya kujitoa kwa Mungu kwa upendo wa kweli. Yaani, kutubu ni kurudi kwa Mungu na kukiri kuwa yeye pekee ndiye chemchemi ya wokovu. Bila kuwa na majuto ya kweli, hatuwezi kuwa kweli mahujaji katika jubilei ama katika kwaresima hii. Tujitahidi kukiri na kutubu dhambi zetu.

 

Kushiriki kutoa sadaka na matendo ya huruma

Maandiko Matakatifu yanatukumbusha kuwa watu tunaojali mahitaji ya wengine. Maana kwa kufanya hivyo tunapata dhawabu na tusipofanya hivyo maneno ya Kristo mwenyewe yatasikika katika dhamili zetu kwa kila mmoja wetu alivyoshiriki katika kuwahudumia wengine: 

 

“Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula; nilikuwa na kiu mkanipa kitu cha kunywa; nilikuwa mgeni mkanikaribisha; nilikuwa sina nguo, mkanivisha; nilikuwa mgonjwa mkaja kunitazama; na nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea… Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu na hamkunipa kitu cha kunywa; nilikuwa mgeni wala hamkunikaribisha; nilikuwa uchi hamkuni vika; na nilikuwa mgonjwa na gerezani nanyi hamkuja kunitazama” (Mt 25:35-43). 

 

Katika hili, Mtakatifu Yohane Krisostomo anafundisha kuwa kama: “Unataka kumheshimu Kristo? Usimpite maskini bila msaada.” Kwaresima ni fursa ya kujitoa kwa wengine kwa kutoa sadaka, kusaidia wahitaji, na kutetea haki. Ni kweli kwamba, bila kuwa watu wa haki hatuwezi kuwa mahujaji wa matumaini na kwaresima si kitu kwetu. Matendo ya huruma ni kikolezo kinachochachua na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na kimwili, na hili hujidhihirisha kwa namna tunavyowahudumia wenzetu katika jamii zetu. Tunapofanya hivyo, tunakuwa kweli mahujaji wa imani, matumaini na mapendo wanaojenga Ufalme wa Mungu.

 

Tubuni na kuiamini Injili

 

Ufufuo wa Kiroho na Matumaini

Ni ukweli kuwa, hija ya Kwaresima inafikia kilele chake katika Pasaka, tunaposhiriki ushindi wa Kristo juu ya dhambi na mauti. Mtakatifu Agostino anaeleza bayana kuwa, “Maisha yetu hapa duniani ni hija ya kuelekea kwa Mungu, na moyo wa mwanadamu hauwezi kupumzika mpaka upumzike ndani yake.” Huu ni mwaliko wa kujikana nafsi na kutimiza mapenzi ya Mungu, ambamo ndani yake tunapata ufufuko wa kiroho na tunapata tumaini tunalolingojea. Hivyo ndivyo bwana na mwalimu wetu anatufundisha kwamba ili tuwe mwanafunzi wake ni lazima kujikana, kubeba msalaba na kumfuata (Lk 9:23). Kwa kufunga na kujikana, tunajiweka huru na tamaa za ulimwengu na kumweka Mungu kuwa wa kwanza. Hapa maneno ya Mt. Tomaso wa Akwino yanapata maana anaposema: “kujikana nafsi ni mwanzo wa hekima, kwa kuwa huwezesha mtu kuona mema ya milele." Hivyo basi, kama mahujaji wa matumaini katika Kwaresima, tunapaswa kuiga mfano wa watakatifu na Baba wa Kanisa waliotufundisha jinsi ya kushiriki katika toba na uongofu wa kweli.

 

Mwisho mwishoni, kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli waliotembea jangwani kwa matumaini ya kufika nchi ya Ahadi (Kut 3:7-8), waamini wa leo tunaitwa kuwa mahujaji wa matumaini, tukitembea kuelekea utimilifu wa wokovu ndani ya Kristo. Kwaresima inatufundisha kujikana, kutubu, na kumtumainia Mungu, huku Jubilei ikitualika kusherehekea huruma na neema yake. Mt. Tomaso wa Akwino anasema: "Tumaini linatufanya tutamani mema ya milele na kujiweka tayari kuyapokea kwa neema ya Mungu." Kwa hiyo, katika Kwaresima hii, na katika Jubilei, na tuthubutu kuwa mahujaji wa matumaini kwa kujitoa kwa Mungu, kwa jirani, na kwa safari ya wokovu inayoelekea Pasaka ya milele. Kwa sababu, hija ya Kwaresima ni safari ya kurudi kwa Mungu kwa toba, sala, na matendo ya huruma. Yesu mwenyewe ni mfano wetu mkuu wa kuwa mhujaji wa imani, aliyeteseka, kufa, na kufufuka kwa ajili ya wokovu wetu. Mtume Paulo anasema: “Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona” (2Kor 5:7). Katika Kwaresima hii, na tuwe mahujaji wa imani kwa kujitoa kwa Mungu, kusali, kutubu, na kusaidia wengine. Kwa kufanya hivyo, tutajenga mahusiano ya kweli na Kristo na kufanikisha safari yetu ya kiroho kuelekea uzima wa milele.

 

NAWATAKIA KWARESIMA NJEMA NA JUBILEI YA UKRISTO 2025

 

Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa,

Chuo Kikuu cha Navarra - Hispania.

Jimbo Katoliki Shinyanga. 

@2025 Ekinopia Studies