TUMSIFU YESU KRISTO...!
“Furahini daima. Salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu
(1 Thes 5:16-18).
Mtume Paulo, Silvano na Timotheo walikuwa wamefanikiwa kuhubiri Injili ya Kristo huko Thesalonike na kupata wafuasi wengi. Hata hivyo, kutokana na njama za baadhi ya maadui zao, Mtume Paulo alilazimika kuondoka Thesalonike na kuelekea Atene ndani ya muda mfupi, kabla hata ya kumalizia mafundisho yake. Akiwa huko, alimtuma Timotheo aende Thesalonike ili kuwajulia hali wakristo wa kule na kufahamu kuhusu maendeleo yao. Timotheo alifanya hivyo. Kutoka Atene, Mtume Paulo alielekea Korintho. Akiwa huko, Timotheo alirudi na kumpa habari za maendeleo ya jumuiya ya wakristo wa Thesalonike. Alimtaarifu kwamba walikuwa imara katika imani na mapendo, pamoja na kwamba walikuwa wakikumbana na mateso kutoka kwa maadui wa ukristo.
Wathesalonike walikumbwa na changamoto nyingi katika kuishi imani yao. Pamoja na hayo, Mtume Paulo aliwaalika wawe na shukrani katika kila hali akisema: “Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu” (1 Thes 5:18). Imani waliyokuwa wameipokea ilikuwa sababu ya furaha, lakini vilevile ilikuwa sababu ya mateso. Mtume Paulo alikuwa ameondoka Thesalonike kabla ya kumaliza mafundisho ya kikristu, na hasa kuhusu “Ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristu.” Ni katika hali hii, walipoanza kufariki baadhi ya wakristu waliokuwa wameipokea imani, wenzao waliobaki walianza kujawa na wasiwasi. Wasiwasi wao mkubwa ulikuwa ni huu: “Hivi kesho yetu itakuwaje?”, “Hivi wenzetu waliofariki wako katika hali gani?”, “Hivi tukifa tutapata wokovu kweli, ama tunataabika bure?” Walikuwa na hamu na shauku ya kujua kesho yao.
Ni katika muktadha huu, Mtume Paulo aliamua kuwaandikia barua, ambamo ndani yake anakamilisha mafundisho aliyopaswa kuwapatia kabla ya kuondoka kutoka kwao, na zaidi sana, anawapa matumaini. Kwa kuwaalika wawe na shukrani katika kila hali, ikiwemo mateso, ni kama anawaambia: “Ndugu zangu Wathesalonike, daima tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua!”
Nikiwa nasoma Falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho, Moshi, Tanzania, siku moja wakati napekua katika mtandao wa Facebook nilikutana na picha ya Padre mmoja mlezi wetu katika seminari hiyo. Padre huyo alikuwa ameiweka picha yake na kuandika maneno haya: “Thank God for the unknown future.” Nilipoyasoma maneno haya, niliyapenda, nikayatafakari sana, na baada ya tafakari ndefu nikayachagua yawe mwongozo wangu – au kwa maneno mengine, – yawe maneno ya kunitia moyo kuendelea mbele kila iitwapo “leo.” Imepita miaka kadhaa sasa. Leo ninaomba niwashirikishe hiyo tafakari yangu ambayo nafikiri inaweza kuwa ya kufaa.
Katika maisha, daima tunatamani kuijua kesho yetu. Tunatamani kujua nini kitatokea: Iwapo tutafanikiwa au la! Iwapo tutapata kazi au la! Binti anatamani kujua kama ataolewa au la! Na kama akiolewa anatamani kujua kama atapata watoto na kujifungua salama. Wazazi wanajiuliza iwapo watoto wao watakuwa na maisha mazuri mbeleni au la, na mengine kama hayo. Nini kinawafanya baadhi ya watu kupiga ramli, kama si shauku hii ya kutaka kuwa na uhakika fulani kuhusu kesho yao? Kiufupi, kila iitwapo leo tunawaza kuhusu kesho. Kimsingi, hili ni jambo zuri na linalodhihirisha hulka yetu sisi wanadamu. Hata hivyo, mara nyingi tunapowaza sana kuhusu kesho tunajikuta tunaishia kuwa wenye wasiwasi na mahangaiko. Kesho tunaitazama kwa hofu. Hofu hii wakati mwingine hupelekea kwenye huzuni. Tungependa sana kujua ya kesho kiasi kwamba tunajikuta tunaishi leo kwa huzuni. Kabla hatujapata jibu la mwisho – ikiwa kesho itakuwa nzuri au la – tunajitangazia matokeo sisi wenyewe. Na kwa bahati mbaya sana, mara nyingi tunajitangazia kushindwa, kwa kuwa tunahisi tutashindwa!
Imani yetu kwa Kristo inatupa mwaliko wa kumtumainia Mungu, na kwasababu hiyo, kumshukuru hata kwa yale aliyotuandalia huko mbeleni. Katika kitabu chake, God or Nothing, Kardinali Robert Sarah anaandika: “Lakini ni nani anayeweza kujua mahali ambapo Mungu anatupeleka? Mwangalie Mtakatifu Paulo (Saulo): katika hasira yake dhidi ya Wakristo, je, alijua mahali ambapo angeishia alipokuwa njiani kuelekea Damasko? Na Mtakatifu Agustino, kijana mwenye matamanio mengi na mwenye shauku ya kupata heshima na kuishi maisha ya anasa, ambaye alikuwa na mgogoro wa ndani kati ya tamaa zake mbaya na matamanio yake ya kuongoka, kati ya mwili wake na roho yake, je, alielewa alichokuwa akitafuta alipoondoka Afrika kuelekea Milano? Sisi sote ni walengwa wa udhihirisho huu wa ajabu wa huruma ya Mungu. Mapenzi yake mema kwetu hayana mipaka!”
Yale maneno ya Padre: “Thank God for the unknown future” nimeamua kuyatafsiri hivi – japo si kwa tafsiri sisisi – “Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua!” Wapendwa, Saulo, ambaye aliwatesa sana Wakristo, aliongoka na kwa neema ya Mungu akawa Mtume aliyehubiri Injili ya Kristo kwa mataifa – Kanisa linamheshimu kama “Mtume wa Mataifa,” – na Mtakatifu Agustino, ambaye maisha yake ya awali hayakuwa mazuri, alipoongoka alihubiri Injili, akafanya kazi kubwa sana ya kutetea imani ya Kikristo na akaandika vitabu vingi vyenye utajiri mkubwa sana wa kifalsafa na kiteolojia ambavyo mpaka sasa vimo katika Mapokeo ya Kanisa.
Ndugu zangu, tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua na tusiiangalie kesho yetu kwa woga, bali kwa matumaini na ujasiri mkubwa. Mungu hafungwi na muda. Sisi ndio tunaoishi ndani ya muda. Kwasababu hiyo, sisi tunajua ya leo tu, lakini kwa Mungu hamna jana, leo wala kesho. Hivyo anaijua kesho ya kila mmoja wetu. “Yesu Kristo ni yuleyule: jana, leo na milele” (Ebr 13:8) na kutobadilika kwake ndio msingi wa matumaini yetu.
Wakati mwingine Mungu huziruhusu changamoto tunazopitia kwa ajili ya kuimarisha imani yetu, kufanya toba na kubadili mwenendo au mawazo yetu ili yaendane na mpango wake mtakatifu. Kielelezo kizuri kuhusu ukweli huu tunakipata katika Maandiko Matakatifu tunaposoma Kitabu cha Ayubu: “Mtu mtakatifu huyu, ambaye alikuwa tajiri na mwenye watoto wengi, alikuwa na mali nyingi sana, mali zote ambazo mtu anaweza kutamani. Lakini maisha ya Ayubu yalibadilika ghafla. Watu wenye silaha waliiba kondoo wake elfu saba, na jozi zake za ng’ombe mia tano, na ngamia wake elfu tatu. Upepo mkali ulivuma kutoka jangwani, na nyumba walimokuwa watoto wake ikaanguka na kuwaua wote. Wakaldayo waligawanyika katika vikosi vitatu, na watumishi wake waliuawa kwa upanga. Hatimaye, yeye mwenyewe akaugua. Licha ya mfululizo huu wa majanga, Ayubu alibaki bila kutetereka katika upendo wake kwa Mungu. Alisisitiza kwa uthabiti kuwa hana hatia na akakiri imani thabiti mithiri ya mwamba wa karne nyingi: “Laiti maneno yangu yangeandikwa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Laiti yangechorwa kwa chuma na risasi juu ya jiwe ili yadumu! Najua wazi Mkombozi wangu anaishi, mwishowe yeye atanipa haki yangu hapa hapa duniani. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivyo, nitamwona Mungu kwa macho yangu mwenyewe. Mimi mwenyewe nitakutana naye; mimi mwenyewe na si mwingine nitamwona kwa macho (Ayubu 19:23-27).”
Ni ukweli kwamba wakati kilipoandikwa Kitabu cha Ayubu bado katika Israeli hakukuwa na wazo na imani kuhusu maisha ya milele mbinguni. Wakati huo Waisraeli waliamini kwamba Mungu huwalipa wema na wabaya, kila mtu kadiri ya matendo yake, hapahapa duniani. Pamoja na hayo, Ayubu alionyesha imani na matumaini makubwa sana kwa Mungu. Alitumaini pale ambapo kulionekana hakuna tena tumaini. Alimshukuru Mungu kwa kesho ambayo hakuijua. Na nini kilitokea baada ya hayo yote? Baada ya kuwa amepoteza kila kitu na amepata ugonjwa mbaya wa ngozi, Ayubu alitembelewa na rafiki zake ambao walikuwa na nia ya kumfariji. Hawa walitoa hoja zao kulingana na mapokeo ya dini ya kiyahudi, kwamba Mungu humtunza mtu mwema na kumwadhibu mwovu. Kadiri yao, mateso ya Ayubu yalimaanisha kuwa alikuwa ametenda dhambi. Ayubu alisisitiza kuwa hakuwa ametenda dhambi na wala hakuona sababu ya Mungu kumuweka katika hali hiyo. Baada ya hayo, Mungu mwenyewe alijidhihirisha na kumhoji Ayubu bila kuyajibu maswali yake, badala yake alionyesha tu ukuu wake na hekima yake. Ndipo Ayubu alipokiri ujinga wake, kwamba alikuwa amenena bila kufikiri. Alikiri kuwa Mungu ndiye kweli Muweza wa yote. Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua: Baada ya Ayubu kuwaombea msamaha rafiki zake, Mwenyezi Mungu alimrudishia hali yake ya kwanza. Alimpatia maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali (rej. Ayubu 42:10).
Wapendwa, labda sisi hatujakumbwa na dhahama kama Ayubu. Hata hivyo, kwa upande wetu tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kujitahidi kuishi vizuri na watu wanaotuzunguka. Tupende kujifunza kwa kutafakari maisha ya watu mbalimbali. Tujiulize maswali kuhusu maisha yao ya nyuma. Swali haswa la kujiuliza ni hili: Hivi mtu huyu aliwahi kujua kama leo angekuwa mahali alipo, akiwa anaishi na hao anaoishi nao sasa? Wapendwa, iwe tunasoma na watu, ama tunaishi na watu katika vijiji na mitaa yetu, ama tunawaongoza watu katika nyadhifa mbalimbali; tujitahidi kuishi nao vizuri. Je, ndugu zake Yusufu waliwahi kufikiri kuwa ndugu yao waliyemuuza (rej. Mwa 37:26-28), ndiye ambaye angewapatia chakula wakati njaa kuu ilipoikumba Israeli hadi wakalazimika kwenda kuomba chakula huko Misri? (rej. Mwa 47:12).
Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kupenda kuona mambo mazuri yaliyomo kwenye maisha yetu na kuepuka kishawishi cha kuona mabaya pekee. Tangu wazazi wetu wa kwanza walipotenda dhambi, wanadamu wote tuna tabia ya kuona zaidi mambo mabaya kuliko kuona mazuri. Baada ya dhambi hiyo ya asili, Adamu alipoulizwa na Mwenyezi Mungu kama amekula tunda la mti ambalo alikuwa amekatazwa alijibu: “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala” (Mwa 3:12). Hakumuona tena yule mwanamke kama mwenza wake wa thamani ambaye mara ya kwanza alipomuona alimfurahia hadi akasema “Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu, na nyama kutoka nyama yangu” (Mwa 2:23). Wapendwa, tunaalikwa kushinda kishawishi cha kuona mabaya tu kwa kujitahidi kuona na kutambua neema za Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Kumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua ni kutambua kwamba wakati mwingine leo ndio ile “kesho” ambayo jana tulikuwa tukiitarajia. Je, jana (au zamani au siku za nyuma) hukuwa unamuomba Mungu akujalie mambo ambayo baadhi yake unayo leo? Hukuwa unamuomba uwe mahali ambapo upo leo? Kesho nzuri uliyoitarajia na kuiomba inawezekana imekwishafika na upo unaiishi leo. Hukuijua, na sasa imekwishafika na upo unaiishi, mshukuru Mungu!
Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kujua kuishi vizuri na kikamilifu ndani ya wakati uliopo. Ishi leo, siyo jana au kesho! Mwandishi wa kitabu cha Mhubiri alitafakari sana juu ya ufupi wa maisha ya binadamu na mambo yanayotatiza katika maisha. Wakati fulani hasiti kusema: “Mungu amekifanya kila kitu kiwe kizuri kwa wakati wake. Amempa binadamu hamu ya kujua mambo ya baadaye, lakini hajamjalia fursa ya kuelewa matendo yake Mungu tangu mwanzo mpaka mwisho” (Mhu 3:11). Baada ya hapo, anawashauri watu kufurahia matunda ya kazi zao katika wakati uliopo kwa namna inayofaa, kwa maana matunda ya kazi zao ni majaliwa ya Mungu. Wapendwa, tumshukuru Mungu wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa; wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna; wakati wa afya na wakati wa ugonjwa; wakati wa huzuni na wakati wa furaha; wakati wa msiba na wakati wa sherehe; wakati tukiwa nacho na wakati tusipokuwa nacho; wakati wa kazi na wakati wa mapumziko; wakati wa ukimya na wakati wa kuzungumza; wakati wa vita na wakati wa amani (rej. Mhu 3:1-8).
Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua! Kivipi? Kwa kuwa na matumaini kwa Mungu. Katika Injili, anawafundisha wanafunzi wake kuwa Mungu ndiye Mpaji wa vyote (Providence) na kwasababu hiyo wasiwe na wasiwasi kuhusu kesho – kwamba watakula nini ama watavaa nini (rej. Mt 6:25-34) – huku akiwahakikishia kwa kusema: “Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote” (Mt 6:32). Katika nyakati zetu hizi, watu wengi wanaishi kwa wasiwasi. Kama ilivyokuwa wakati wa Mitume, hata sisi Bwana wetu Yesu Kristo anatuuliza: “Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza muda wa maisha yake?” (Mt 6:27). Ni wazi kwamba lengo la Bwana wetu Yesu Kristo siyo kutualika tubweteke. La hasha! Mwaliko wake kwetu ni kwamba tuwe watu wenye imani na matumaini kwa Mungu tukitambua kuwa juhudi zetu zitazaa matunda kwa neema zake. Hapa nayakumbuka maneno ya Mt. Gregori wa Nisa: “Si vyema wakristo kujali sana juhudi zao za kibinadamu kiasi cha kufikiri kwamba taji zima linategemea nguvu zao. Badala yake, ni muhimu wakayatanguliza mapenzi ya Mungu katika matarajio yao ya kupewa tuzo.”
Wapendwa, tusiwe na wasiwasi. Tusiogope! “Leka kwechura!” Utamaduni ulioenea sana siku hizi na unaowatesa watu wengi ni kufikiri kupita kiasi (Overthinking). Ni muda muafaka kabisa wa kumsikiliza Bwana wetu Yesu Kristo akitwambia kwa upole: “Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo” (Mt 6:34).
Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kwenda hatua kwa hatua (“One step at a time”). Wahenga husema “haraka haraka haina baraka” na “polepole ndio mwendo.” Mara kadhaa nimetafakari kuhusu miti inayokutwa katika nchi zilizo upande wa kaskazini wa dunia (northern hemisphere). Miti hii hupukutisha majani unapoanza msimu wa baridi, na majani ya miti hii yanapoanza kuota tena huwa ni ishara ya ujio wa majira ya kiangazi. Hapa ninawiwa kufanya kile ambacho hujulikana kama personification: Kama mti ungekuwa na uwezo wa kuongea kama binadamu, na kama tungeweza kuuuliza mti mmojawapo wakati majani yake yanapopukutika: “Mti, sasa itakuwaje? Umepoteza majani yako!” Bila shaka mti ungetujibu: “Ndiyo. Lakini hiyo ni ishara nzuri, kwamba Mungu anakwenda kunipatia majani mapya na bora zaidi. Ninachotakiwa kufanya ni kusubiri.” Wapendwa, nasi tujifunze kuwa na subira wakati tunapoona kuwa kuna kitu hatuna au kuna tulichopoteza. Huenda Mungu atatupatia yale tunayoyahitaji kadiri ya mapenzi yake, endapo tutadumu katika imani na matumaini kwake. Ikiwa anaukumbuka mti ambao majani yake yalipukutika, anawalisha ndege wa mwituni, na anayastawisha maua ya porini (rej. Mt 6:26,28-30), atakosa kutukumbuka sisi? Viumbe alivyoviumba kwa sura na mfano wake? Tusimfanye Bwana atuite kwa mshangao: “Enyi watu wenye imani haba!” (Mt 6:30).
Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kuepuka kuwa mahakimu wa maisha ya watu na kuwakatisha tamaa. Tusimkatishe tamaa mtoto, ndugu, jirani, mwanafunzi, nk. na kumwambia: “Hutafika popote!” au “Huwezi lolote!” na maneno mengine kama hayo. Bila shaka tukitafakari kwa makini tutagundua kuwa wapo watu wengi sana ambao ilidhaniwa kuwa wameharibikiwa kabisa na badala yake wakafanikiwa, ama hata tumewashuhudia wakifanikiwa. Kijana mmoja aliwahi kuambiwa na mwalimu wake wa Jiografia kuwa hatafika mbali. Baada ya miaka kadhaa, kijana huyo alipofika jijini New York nchini Marekani kwa ajili ya kuanza kazi, alimtumia picha mwalimu wake iliyoambatana na ujumbe wa maandishi uliosomeka hivi: “Mwalimu, ulisema sitafika mbali. Hapa ni wapi?” Wapendwa, Mungu anaweza kuruhusu mabaya (mateso, kushindwa, umaskini, nk) kama njia ya kutengeneza mambo mema na mazuri. Kifo cha Kristo msalabani ni ushuhuda wa jambo hilo. Kesho ya kila mmoja wetu imo mikononi mwa Mungu. Sisi tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua!
Tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua kwa kuweka juhudi katika yale tunayotakiwa kufanya na kuyaweka yale yaliyo nje ya uwezo wetu mikononi mwa Mungu. Msemo wa kiingereza unasema “Do the best and God will do the rest.” Hilo linaendana na kuepuka kuishi kama vile kila kitu kinategemea nguvu zetu tu. Unapopanga mipango yako usisahau kujisemea moyoni: “Mungu akijalia,” “Kwa mapenzi ya Mungu,” nk. Hata unapoongelea mipango yako, usimsahau Mungu. Na kwa wale ambao kwa namna fulani kesho ya maisha yao imo mikononi mwa watu wengine (labda wakubwa wao), hao pia wasisahau kwamba pamoja na hilo, Mungu ndiye Bwana wa historia ya maisha yao (jana yao, leo yao na kesho yao). Hawa wamuombe Mungu awaimarishe katika utii, uvumilivu, unyenyekevu na uchapakazi. Wamuombe pia awaongoze wakubwa wao, ili katika yote mapenzi ya Mungu yatimizwe hapa duniani kama ilivyo mbinguni. Matumaini yao yasififie!
Wapendwa, niseme nini zaidi?...
Kwa hayo na mengine mengi, tumshukuru Mungu kwa kesho tusiyoijua!
Imeandaliwa na:
Frt. Avitus Mujuni,
Jimbo Katoliki Bukoba
Mei 1, 2026,
Sherehe ya Mt. Yosefu Mfanyakazi.
Pd. Emmanuel Kimambo Nhanwa,
Director of Ekinopia Studies

.jpg)

